RIPOTA PANORAMA
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na wanachama wake, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusitisha uondoshaji wananchi katika Kata ya Ngorongoro kuwapeleka Kijiji cha Msomera ili kutoa nafasi kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza.
Ombi hilo la THRDC na wanachama wake limo katika mapendekezo ya watetezi wa haki za binadamu kuhusu hali ya haki za binadamu katika Kijiji cha Msomera na Tarafa za Ngorongoro, Loliondo na sehemu ya Tarafa ya Sale.
Kwa mujibu wa taarifa ya THRDC na wanachama wake iliyotolewa hivi karibuni, imeiomba serikali kutoa nafasi ya kuandaa kwa pamoja mpango wa uhamaji kwa hiari wa muda mrefu na mfupi wenye kuzingatia misingi ya haki za binadamu na shirikishi.
Pamoja na hilo, THRDC na wanachama wake waliofanya ziara katika Kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga na Tarafa za Ngorongoro, Loliondo na sehemu ya Tarafa ya Sale zinazounda Wilaya ya Ngorongoro iliyopo Mkoa wa Arusha kwa ajili ya kufuatilia hali ya haki za binadamu na mifugo, wameishauri serikali kuwachukulia hatua watumishi wa umma wanaotisha wananchi wanapodai haki zao.
Taarifa inaeleza kuwa ziara hiyo iliyofanyika kuanzia April hadi Septemba, 2023 baada ya serikali kutwaa eneo la vijiji 14, lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,502 mwezi Juni, 2022 na kisha kulitangaza kuwa pori tengefu na baadaye kuwa Pori la Akiba la Pololeti, ilibaini wananchi katika Kijiji cha Msomera wanakabaliwa na changamoto ya maji chumvi ambapo THRDC na wanachama wake wanaiomba serikali iitatue.
Mapendekezo mengine yaliyo kwenye taarifa hiyo ni serikali kuharakisha upatikanaji wa shule mpya ya Msingi la Mkababu na ujenzi wa bweni kwa wanafunzi wa sekondari.
Aidha, THRDC na wanachama wake wametoa rai kwa wananchi kudumisha amani na kuzingatia njia za kimahakama kudai haki zao, wananchi kufanya mikutano na kujadiliana namna ya kutatua changamoto zao za huduma za kijamii na kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo waliyopewa.

Rais Samia Suluhu Hassan
Taarifa inaainisha maombi mengine kuwa wadau wa maendeleo wachangie miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kijiji cha Msomera na inawahimiza watetezi wa haki za binadamu na asasi za kiraia kuendelea kufuatilia hali ya haki za binadamu katika Kijiji cha Msomera.
Pia inawataka kuendelea kuishauri Serikali kuhusu namna bora ya kutatua changamoto katika Kijiji cha Msomera na Tarafa ya Ngorongoro na inawasihi waandishi wa habari kuacha kueneza propanga za chuki na uongo dhidi ya wananchi wa maeneo hayo na kwamba wananchi wenyeji wa Ngorongoro wameitaka serikali ipitie mchakato wa ulipaji fidia kwa kuwa sio shirikishi na hauko wazi.