ANDREW CHALE
Kilimanjaro
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) litatoa huduma ya bure ya intaneti kwa washiriki watakaopanda mlima Kilimanjaro katika kipindi cha kampeni ya ‘twenzetu Kileleni 2023’ ambao ni msimu wa tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro mwakilishi wa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, John Yahaya amesema TTCL inaunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuimarisha umoja na mshikamano nchini.
“Washiriki wote watakaopanda mlima Kilimanjaro katika kipindi hiki cha kampeni ya twenzetu kileleni watapata fursa hiyo ya intaneti bure wafikapo kila kituo katika mlima huo ili kutambua umuhimu wa maadhimisho haya ya miaka 62 ya uhuru wa nchi yetu,” amesema Yahaya.
Amesema uwepo wa huduma hiyo ni fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjari ndani na nje ya nchi yetu na itahamasisha watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya mlima huo na maeneo mengine ya utalii.
Yahaya amesema washiriki zaidi ya 200 watapanda mlima huo kwa ushirikiano na Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA) na Kampuni ya ZARA Tours kuanzia leo asubuhi.
Aidha, Yahaya amesema shirika hilo limeendelea kutekeleza mkakati wake wa kuimarisha mawasiliano kwa kuweka miundombinu ya kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kutoa huduma ndani na nje.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Shirika ka Hifadhi za Taifa (TANAPA), Jenerali Mstaafu, George Waitara amewataka watanzania kujivunia mlima huo kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo hasa kipindi hiki cha kuelekea kwenye maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya ZARA Tours, Ibrahim Juma amesema zaidi ya watu 200 kutoka mashirika na taasisi mbalimbali watapanda mlima huo kupitia kampuni yake ZARA.
“Tutakuwa na mabalozi 17, lakini pia mashirika mengine mbalimbali yamehamasika na wanashiriki msimu huu wa tatu wa Twenzetu Kileleni2023.” amesema Juma.