RIPOTA PANORAMA
SERIKALI imetoa kauli ikifafanua idadi kubwa inayotajwa kufikia watu 763, ya wajumbe wa Tanzania waliokwenda Dubai kushiriki mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Mobhare Matinyi amesema kelele na mijadala inayoendelea sasa kwenye makundi mbalimbali ya kijamii kuhusu wingi wa wajumbe wa Tanzania waliokwenda kushiriki mkutano huo, zinatokana na kukosa taarifa.
Matinyi ameiambia Tanzania PANORAMA Blog iliyomuuliza kuhusu wingi wa wajumbe kwenye msafara wa Tanzania katika safari ya Dubai wakiwemo wapishi na makatibu muhutasi kuwa, atatoa taarifa kuhusu jambo hilo lakini taarifa ya awali imekwishatolewa na Ofisi ya Makamu ya Rais.
Taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Makamu wa Rais inasomeka hivi ‘Tanzania inashiriki mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi nchini Dubai.
‘Mkutano huo umeanza Novemba 30 hadi Disemba 12, 2023 Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo washiriki wakiwemo wakuu wa nchi na serikali zaidi ya 81,000 kutoka nchi takriban 190 wanahudhuria mkutano huo.
‘Ikumbukwe kwamba jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tanianchi zinahusisha wadau mbalimbali ikiwemo serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, vijana na watoto hivyo idadi kubwa ya watanzania ilionyesha nia ya kushiriki katika mkutano huo wa kimataifa ambapo jumla wa watanzania 763 walijiandikisha kwa nia ya kushiriki.
“Kati ya idadi hiyo, watanzania 391 walijiandikisha kutoka wizara na taasisi za serikali wakati 372 walijiandikisha kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, sekta binafsi, vijana na watoto.
‘Hata hivyo idadi ya watanzania walioshiriki kutoka serikalini ni 66, ambapo 56 wanatoka Tanzania Bara na 10 kutoka Zanzibar ambayo ni sawa na asilimia 8.7 ya watanzania waliojiandikisha.
‘Aidha, sehemu kubwa ya washiriki inatoka katika sekta binafsi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na vijana na watoto ambayo ni 340 sawa na silimia 91.3.
‘Baadhi ya washiriki kutoka wizara na taasisi za serikali wamefadhiliwa na mashirika ya kimataifa, aidha washiriki kutoka sekta binafsi, taasisi za kiraia, vijana na watoto wanashiriki kwa gharama zao wenyewe.
‘Hii inaonyesha mwamko wa watanzania kuhusiana na masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi.’

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi nchini Dubai.
Tanzania PANORAMA Blog imemuuliza maswali haya hapa chini Msemaji Mkuu wa Serikali, Matinyi ambayo ameahidi kuyatokea majibu.
‘Kuna mjadala mkali na ambao umezua taharuki kuhusu wingi wa idadi ya watu waliokwenda Dubai pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa mambo ya mazingira. Naomba kupata kauli rasmi ya serikali.
Mosi: Idadi ya watu/ujumbe wa Tanzania waliokwenda kwenye mkutano huo ni wangapi?
Pili: Watakuwa Dubai kwa siku ngapi? Tatu: Gharama za usafiri, malazi na chakula ni kiasi gani? Nne: Ni kweli kwamba kuna wapishi na makatibu muhutasi kwenye msafara huo?
Tano: Ipo hoja kwamba ukubwa huo wa msafara haukuzingatia hali halisi ya uchumi wa nchi/ hali ngumu ya maisha ya wananchi. Nini kauli ya serikali kuhusu hoja hii?
Sita: orodha inayosambaa mitandaoni ikionyesha ukubwa huo wa msafara inatizamwa na baadhi ya watu kuwa wapishi na ‘ma secretary’ hawakuwa na umuhimu wa kuwepo kwenye msafara huo. Nini kauli ya serikali kuhusu hili?
Akijibu, Msemaji Mkuu wa Serikali, Matinyi alisema ‘kelele hizi haziko Informed. Nitakueleza.’
ENDELEA KUPERUZI TANZANIA PANORAMA BLOG KUPATA KAULI RASMI YA SERIKALI KUHUSU WINGI WA WAJUMBE WA TANZANIA WALIOKWENDA KWENYE MKUTANO HUO UNAOENDELEA DUBAI.