RIPOTA PANORAMA
ZAIDI ya Shilingi milioni 600 zilizochangwa na wananchi, wafanyabiashara na kampuni mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ghorofa baada ya kuungua kwa vyumba nane vya madarasa ya Shule ya Sekondari ya Lindi, zinadaiwa kuyeyuka zikiwa mikononi mwa viongozi wa serikali.
Taarifa ya kuyeyuka kwa mamilioni hayo imetolewa na wananchi na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi huku Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Lindi, Ramadhani Diville na Mkurugenzi wa Halmshauri ya Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele wakikosa kauli kuhusu jambo hilo.
Kwa mujibu wa wananchi na madiwani waliozungumza na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu kuyeyuka kwa fedha hizo, Shule ya Sekondari ya Lindi ambayo inachukua wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita iliungua moto mwaka 2016.
Wameeleza kuwa katika ajali hiyo ya moto, vyumba nane vya madarasa, viti na meza 300 na matundu ya vyoo 24 viliteketea kwa moto na baadaye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea shule hiyo ili kujionea uharibifu uliotokea na akiwa shuleni hapo aliendesha harambee iliyolenga kujenga jengo jipya la ghorofa.
Imeelezwa kuwa katika harambee hiyo, wakazi wa Lindi, wafanyabiashara na kampuni mbalimbali walitoa michango ya fedha taslimu na ahadi zaidi ya Shilingi milioni 600.
Kwamba Kampuni ya Saruji ya Dangote ilichangia mifuko ya saruji 900. Pia ulitolewa mchango wa rangi lita 4000, nondo na mabati na kila nyumba katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ilichanga Shilingi 10,000.
Mmoja wa waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Lindi, mwaka 2016 (jina lake limehifadhiwa) ameiambia Tanzania PANORAMA kuwa fedha zilizopatikana kwenye harambee hiyo zilianza kuwekewa mizengwe mapema wakati wa kuzifungulia akaunti benki.

Mojawapo ya madarasa ya Shule ya Sekondari ya Lindi lililoungua moto
Amesema, uliibuka mvutano baina ya wajumbe wa bodi ya shule, uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi kuhusu jina la akaunti na baada ya kutoelewana, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilichukua jukumu la kuratibu, kukusanya na kutunza fedha na michango yote.
Amesema tangu mwaka 2016, Waziri Mkuu Majaliwa alipochangisha fedha hizo hadi sasa, kulichojengwa ni msingi tu na kila wananchi wanapowauliza viongozi wao, hawana majibu.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Lindi, Ramadhani Divelle alipoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu madai kuwa Shilingi milioni 600 na vifaa mbalimbali vya ujenzi vilivyochangwa wakati wa harambee ya Waziri Mkuu Majaliwa vimeyeyuka alisema yeye hawezi kulizungumzia suala hilo bali aliulizwe mkurugenzi wa halmashauri.
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele na kumuuliza lakini naye alisema hawezi kulizungumzia bali watafutwe waliokuwa wanasimamia harambee hiyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele
“Shule iliungua 2016 na kama unavyosema harambee ilifanyika, ilikuwa inaratibiwa na watu nje ya halmashauri kwa hiyo nakushauri uwatafute ambao walikuwa wanaratibu mimi hapo sina ‘comment,” amesema Mnwele.
Alipoulizwa Mnwele waliokuwa wanaratibu harambee hiyo ni akina nani, alikataa kuwataja na kuitaka Tanzania PANORAMA iwatafute kwa njia zake.
Mnwele alisema kuwa mwaka 2018 serikali ilipeleka Shilingi milioni 721 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa shule hiyo kongwe kama ilivyo kwa shule nyingine kongwe nchini lakini kuhusu fedha na michango mingine ya harambee ya Waziri Mkuu Majaliwa hana la kusema.
Hata hivyo, taarifa kutoka Lindi zimeeleza kuwa Shilingi milioni 721 zilizotolewa na serikali zilikarabati madarasa na nyumba za walimu ambavyo havikuungua wakati wa ajali ya moto lakini madarasa yaliyoungua hayakuguswa na fedha na vifaa vimeyeyuka.


