RIPOTA PANORAMA
MWANAHARAKATI wa masuala ya ushawishi, mawasiliano na madai ya katiba mpya, Rosemary Mwakitwange amesema mwenendo wa wanasiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 hauna manufaa kwa watanzania.
Amesema maneno na matendo ya wanasiasa wa chama tawala na wa upinzani yanashawishi zaidi kuamini kuwa uchaguzi mkuu ujao ni wa wanasiasa na vyama vyao lakini hauna maslahi kwa taifa wala wananchi wenyewe.
Akizungumza jana Jijini Dar es Salaam, Mwakitwange alivinyooshea kidole moja kwa moja vyama vya siasa vyenye wafuasi na mashabiki wengi kuwa vimebadilisha msimamo wa kudai katiba mpya.
Alisema vyama hivyo vimebadili msimamo wa kutoshiriki uchaguzi mkuu hadi ipatikane katiba mpya na badala yake sasa vinauhadaa umma kuwa vimefanya utafiti na matokeo ya utafiti huo yanaonyesha watu wanataka vishiriki uchaguzi mkuu ujao.
“Vyama vya siasa vinategemea wapigakura kama wewe na mimi, vinatuona kwamba ni mtaji wake, vinatutaka, vinatushawishi, vinajali hisia zetu kwa sababu vinategemea kura zetu, huko ambako kura zinaheshimika.
“Lakini sisi kiuhalisia ni tofauti. Kama chama cha siasa sijui CCM, Chadema ana hamu na wewe, anajalihisia zangu mimi na wewe leo, lakini hatumlazimishi ajali, wanaweza wakaendelea wakafanya wanavyotaka.
“Mimi hiyo hainikondeshi lakini historia itabaki kwamba sikupiga kura na uchaguzi huu wananchi hawakuchaguana. Ni uchaguzi wa vyama siasa na siasa,” alisema Mwakitwange.
Alisisitiza kuwa katika mazingira ya sasa, uchaguzi hauna manufaa kwa watanzania na kwamba hatua ya vyama vya siasa vya upinzani ambavyo ni vikubwa kubadili msimamo wake sasa kunaonyesha kila dalili kuwa vimeahidiwa kupata maslahi binafsi.
Mwakitwange alieleza kushangazwa kwake na vyama hivyo vikubwa vya upinzani kukimbilia kushiriki uchaguzi huku vikiwashawishi wananchi wakati vinajua mazingira yaliyopo siyo rafiki kulinda kura za wapigakura.
Alisema mazingira ya sasa ya kufanya siasa nchini yanapaswa kubadilika kwa kutoa uhuru kwa watu kutobanwa kuwa wanachama wa chama cha siasa ili kuwa wagombea katika chaguzi mbalimbali nchini.
Mwakitwange alisema wanasiasa wa upinzani waache kuutumia umma vibaya kusaka madaraka na badala yake watangulize maslahi ya umma mbele.