Thursday, July 17, 2025
spot_img

SHAMBA LA WAZIRI MKUU MAJALIWA LAMPA ‘NDIMI MBILI’ DED LINDI

RIPOTA PANORAMA

KUNA utata kuhusu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kumiliki shamba ambalo hajaliendeleza, lenye ukubwa wa ekari 100 lililopo Mtaa wa Tandangongoro, Kata ya Tandangongoro, Manispaa ya Lindi.

Taarifa kuwa Waziri Mkuu Majaliwa anamiliki shamba hilo, zilitolewa kwa umma Novemba 27, 2023 kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram za Halmashauri ya Manispaa ya Lindi; na pamoja naye wakitajwa watu 437.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi aliwatangazia wananchi waliopatiwa mashamba kwa ajili ya kilimo cha korosho katika Mtaa wa Nandimba, Mkanga,Tandangongoro, Chikonji, Ruaha, Mnali, Sinde, Masasi ya Leo, Mto Mkavu, Nanyanje, Likabuku na Jangwani kati ya mwaka 2017 hadi 2022 kuwa wamekosa sifa ya umiliki wa mashamba hayo.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manisaa ya Lindi, Dk. Stanford Mwakatage ilieleza kuwa watu hao walipewa mashamba hayo kwa masharti ya kuendeleza kwa kupanda miti ya mikorosho ndani ya mwaka mmoja hivyo kwa tangazo alilolitoa lenye orodha ya majina 437 likitangulia jina la Waziri Mkuu Majaliwa, wamepoteza sifa ya kuwa wawekezaji wa mashamba hayo kwa mujibu wa mkataba.

Taarifa hiyo iliondolewa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya halmashauri hiyo kabla ya Juma Mnwele, ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kutoa taarifa nyingine akieleza kuwa taarifa ya awali iliyohusisha jina la Waziri Mkuu Majaliwa ni upotoshaji hivyo ipuuzwe.

Katika taarifa yake mpya, Mnwele alieleza kuwa taarifa inayodaiwa kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi si sahihi kimantiki na maudhui na kwamba siyo ya kwao na haihusiani na msimamo wa Manispaa ya Lindi hivyo ni batili.

Mnwele alieleza kuwa taarifa kamili kuhusu wananchi wenye miliki ya mashamba itatolewa.

Tanzania PANORAMA Blog imemtafura Mnwele na kumuuliza kilichotokea hadi taarifa aliyoikanusha ikawekwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya manispaa anayoingoza na pia kuhusu taarifa kamili aliyoahidi kuitoa, naye akijibu alisema mitandao yao ilidukuliwa na wadukuzu wa mitandao.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Alisema taarifa iliyohusisha jina la Waziri Mkuu Majaliwa ameiaknusha kwa sababu ilisambazwa nje ya uelewa wake na walipitia kwenye mitandao nao na kuona kuna wavamizi wa mitandaoni walivamia kurasa zao, hivyo watatoa taarifa rasmi ambayo wanaisimamia sasa.

Alipoulizwa kama Dk. Mwakatage ambaye alisaini taarifa aliyoikanusha ni mtumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mnwele hakijibu swali hilo na badala yake alizidi kusisitiza uhatari wa wadukuzi wa mitandaoni na kutoitambua taarifa hiyo.

Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza Mnwele kama Waziri Mkuu Majaliwa ana shamba alilopewa na Manispaa ya Lindi; kwanza alikubali kwa kueleza lina mikorosho mikubwa sana kisha akakanusha akisema Waziri Mkuu Majaliwa hana shamba katika Manispaa ya Lindi.

Dk. Mwakatage ametafutwa kwa simu yake ya kiganjani ili kuzungumzia sakata hilo lakini iliita bila kupokelewa na Waziri Mkuu Majaliwa naye alipotafutwa kwa simu yake kiganjani ili kupata kauli yake, iliita bila majibu.

Haya yanatokea sasa huku kukiwa na migogoro mingi ya ardhi katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ambapo wananchi wamekuwa wakipaza sauti zao kuwa wananyanyang’anywa maeneo yao na viongozi na au kulipwa fidia isiyostahili maeneo yanayochukuliwa.

Tanzania PANORAMA Blog itaripoti kwa uhakika mtu aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mnwele wakati taarifa ya watu waliokosa sifa za umiliki wa mashamba ilipotolewa, iwapo ukurasa wa mtandaoni ukidukuliwa, mmiliki wake anaweza kuendelea kuutumia ukiwa umedukuliwa na madai ya Waziri Mkuu Majaliwa kuwa na shamba lenye ukubwa wa ekari 100 aliloshindwa kuliendeleza.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya