Monday, September 8, 2025
spot_img

KIKWETE, FRIGENTI WATEMBELEA SHULE ZA MSINGI DAR ES SALAAM

ANDREW CHALE

Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Laura Frigenti leo wametembelea Shule za Msingi Maji Matitu iliyoko Mbagala na Mikongeni iliyoko Gongo la Mboto, Jijini Dar es Salaam. 

Pamoja nao, waliambatana na Naibu Waziri, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Juma Kipanga na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI,) Deo Ndejembi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais Mstaafu Kikwete mapema kabla ya kuanza kwa ziara hiyo imeeleza kuwa imefanyika siku tatu kabla ya mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi wa GPE utakaofanyika Zanzibar, wiki ijayo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, madhumuni ya ziara hiyo ni kukagua shule ambazo shirika hilo linazifadhili.

Taarifa imeeleza kuwa shirika hilo limefadhili ujenzi wa madarasa nane na matundu 20 ya vyoo katika Shule ya Msingi Maji Matitu na katika Shule ya Msingi Mikongeni limechangia ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Kikwete ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na GPE kuboresha sekta ya elimu hususan kwa wasichana na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi na mikakati ya kuiendeleza sekta hiyo.

Rais Mstaafu, Jakaya kikwete na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), Laura Frigent wakikagua vifaa vya kifunzia vya wanafunzi katika ziara yao ya kutembelea shule zinazofadhiliwa na shirika hilo, leo.

Kikwete ambaye ni mwafrika wa kwanza kuongoza GPE, amesema hadi sasa shirika hilo limeipatia Tanzania Dola za Marekani Milioni 332 (takriban Shilingi 834,980,332,000.00) ambazo ni msaada kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Frigenti ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kusaidia sekta ya elimu hususan katika nchi zenye uhitaji, akisisitiza kwamba changamoto nyingi za kimaisha zinaweza kuepukika endapo wananchi watapatiwa elimu bora.

Frigenti ameeleza kuridhishwa kwake na matumizi ya fedha ambayo GPE imekuwa ikitoa kwa Tanzania na aliahidi kuendeleza uhusiano mzuri uliopo na uliodumu kwa miaka 10 sasa.

Ameisifu serikali kuendeleza elimu kwa kujenga miundombinu bora na kuweka mkazo kwa kila mtoto kupata elimu.

Novemba mwaka huu, GPE ilisani makubaliano na serikali ya kutoa Dola za Marekani milioni 85 (takriban Shilingi 213, 775, 085, 000.0) kwa ajili ya kusaidia mafunzo ya walimu.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), Laura Frigent akizungumza na wanafunzi alipofanya ziara ya kukagua shule zinazofadhiliwa na shirika analoliongoza, leo (Picha zote na Andrew Chale)

Kikwete, akiwa Mwenyekiti wa GPE ataongoza vikao vya bodi ya shirika hilo huko Zanzibar vinavyotarajiwa kuanzia Disemba 4 hadi 6 ikiwa ni mara ya kwanza kwa shirika hilo la kimataifa kufanya vikao vyake vya bodi barani Afrika.

GPE iliyoanzishwa mwaka wa 2002, ni shirika linalosimamiwa na Benki ya Dunia na shughuli zake ni kufadhili maendeleo ya elimu ya msingi na utendaji wa sera za nchi zinazoendelea. 

Majukumu ya GPE ni pamoja na kusaidia serikali za nchi zinazoendelea kufanya mabadiliko ya kimfumo na kuoanisha rasilimali na ufadhili ili kutoa elimu bora kwa watoto wote, kuinua viwango vya kujifunza na kukabiliana na changamoto mpya.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya