Thursday, July 17, 2025
spot_img

LHRC YALAANI MAUAJI YANAYODAIWA KUFANYWA NA POLISI

RIPOTA PANORAMA

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani mauaji ya mlinzi wa  Baa ya Boardroom, Razak Azan (29) iliyopo Sinza, Jijini Dar es Salaam.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Dk. Anna Henga imeeleza kuwa tukio la mauaji ya Azan aliyepigwa risasi na maafisa wa polisi waliokuwa wakifanya msako usiku wa Novemba 29, 2023 ni la kusikitisha na linarudisha nyuma imani ya wananchi kwa vyombo vya dola.

Katika taarifa yake hiyo, Wakili Henga ameeleza kuwa polisi ni walinzi wa raia na mali zao, wanapogeuka kuwa wavunjifu na wakiukaji wa haki za binadamu, inasikitisha na kufikirisha.

“Kwa miaka mitatu mfululizo, LHRC imekuwa ikipokea matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu yanayotokana na maafisa wa vyombo vya dola kutumia nguvu kupita kiasi.

“Kwa mwaka 2022, LHRC ilikusanya matukio 10 ya mauaji yanayotokana na maafisa wa vyombo vya dola kutumia nguvu kupita kiasi, ambayo ni tukio moja zaidi ukilinganisha na matukio yaliyokusanywa mwaka 2021,” amesema Wakili Henga katika taarifa yake.

Amesema matukio ya aina hiyo yanayofanywa na maafisa wa vyombo vya dola yanaonyesha umuhimu wa kuanzishwa kwa chombo huru cha kiraia cha kuangalia utendaji kazi wa maafisa wa vyombo vya dola.

Wakili Henga amesema chombo hicho kitasaidia kurejesha au kuongeza imani ya umma kwa vyombo vya dola na kuongeza uadilifu na uwajibikaji miongoni mwa maafisa wa vyombo vya dola.

“Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi kwa vyombo vya habari kuwa askari walimjeruhi inakinzana na taarifa kuwa askari hao ndio waliosababisha kifo cha marehemu Razak,” amesema.

Wakili Henga amesema LHRC inatoa rai kwa mamlaka husika kuchukua hatua kali na kuziweka wazi ili watuhumiwa wa tukio hilo wafikishwe mbele ya sheria na kukomesha vitendo vya aina hiyo ambavyo vimekuwa kama desturi kwani vinakiuka haki za binadamu hususan haki ya kuishi.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya