RIPOTA PANORAMA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amemwandikia barua ya kujiuzulu wadhifa wake huo mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.
Vyanzo vya habari vya uhakika vya Tanzania PANORAMA Blog vilivyoko ndani ya CCM vimeeleza kuwa Chongolo aliwasilisha barua yake kwa Mwenyekiti Samia Novemba 27, 2023.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vilivyoko ndani ya CCM, Chongolo ameeleza sababu ya kujiuzulu wadhfa huo ni kuchafuliwa kwenye mitandao ya kijamii siku chache zilizopita.
“Kwenye barua yake hiyo ameandika hivi; Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza nitumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi na Chama Cha Mapinduzi kwa kuniamini, kunilea na kunivumilia wakati wote wa uongozi wangu.
“Mheshimiwa Mwenyekiti utakumbuka kuwa April 30, 2021 niliteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuwa Katibu Mkuu wa CCM. Uteuzi wangu ulitokana na mapendekezo yako, upendo wako na uongozi wako wenye mapenzi mema kwangu, kwa chama na taifa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti siku chache zilizopita nimechafuliwa kupitia mitandao ya kijamii. Hali hiyo imenikumbusha wajibu wa kiongozi kuwajibika kwa maslahi ya chama wakati wote unapotuhumiwa au kuhisiwa kufanya jambo lolote kinyume na kanuni, taratibu, miiko na tamaduni za chama chetu.
Mheshimiwa mwenyekiti naomba uridhie ombi langu kwako la kujiuzulu,” chanzo chetu kinanukuu sehemu ya barua hiyo.
Kinaeleza zaidi kuwa katika barua yake hiyo, Chongolo ameeleza kutambua kuwa uimara wa CCM unatokana na uongozi wa Rais Samia unaolenga kukuza na kustawisha hali ya maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi.
“Mheshimiwa Mwenyekiti sipo tayari kuona Chama Cha Mapinduzi kinachafuka kwa kuhusisha au kunasibisha nafasi yangu ya Katibu Mkuu na uvumi wa matendo, tabia au mienendo ninayochafuliwa nayo.
Mheshimiwa mwenyekiti kwa unyenyekevu mkubwa naomba uridhie ombi langu,” chanzo chetu kinaikariri zaidi barua hiyo.
Inaelezwa Chongolo amehitimisha barua yake hiyo ya kung’atuka kwa kumuombea Rais Samia kwa Mungu amuepushe na amrinde dhidi ya hila, husda na watu wote wenye nia ovu dhidi yake, CCM, serikali na taifa.
Aidha, inaelezwa kuwa Chongolo ameahidi kuendelea kuwa mwana CCM mtiifu wakati wote.