Friday, July 18, 2025
spot_img

JAJI NTALE KUSHTAKIWA NDANI, NJE YA NCHI

RIPOTA PANORAMA

WAKILI Mpale Kaba Mpoki anakusudia kumfungulia kesi nane, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Mawakili, Jaji Ntale Kilekamajenga katika mahakama za ndani ya nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Wakili Mpoki alisema anakusudia kufungua kesi dhidi ya Jaji Ntale, katika Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.

Alisema sambamba na uamuzi huo, pia anakusudia kuandika barua kwa mwangalizi maalumu wa Umoja wa Mataifa (UN) wa mwenendo wa majaji na mawakili kueleza kilichotokea siku alipohukumiwa kutofanya kazi ya uwakili kwa muda wa miezi sita.

Jaji Mpoki alisema atatoa taarifa kwa mwangalizi maalumu wa watetezi wa haki za binadamu wa Umoja wa Afrika (AU) ili aangalie uhalali wa kitendo alichofanyiwa na Jaji Ntale na kamati yake.

Akizungumzia kesi anazokusudia kumfungulia Jaji Ntale, alisema anakusudia kukata rufaa Mahakama Kuu chini ya kifungu  cha 24 cha sheria ya mawakili, kupinga uamuzi wa Jaji Ntale wa kufungia leseni yake ya uwakili.

“Na katika kutekeleza azma hiyo, kama sheria inavyotaka tumekwishaipelekea kamati hiyo kusudio letu la kukata rufaa pamoja na kuomba mwenendo ili kutuwezesha kukata rufaa.

“Ninaamini kwamba nitapata hiyo nakara ya hukumu na mwenendo siku chache zijazo kwa sababu kutokana na yaliyojiri siku ile, kitendo hicho hakikuchukua hata dakika 20 au 10 kwa hiyo naamini kitu chochote ambacho kitaandikwa hakitazidi karatasi tatu.

“Hivyo naamini katika kipindi cha siku saba, nitakuwa nimepata hivyo vitu tulivyoomba.

“Na endapo tutakuwa hatujapata nakara ya hukumu katika hizo siku saba, maelekezo ambayo nimewapa mawakili wangu ni kwamba wafungue kesi ya mapitio kuomba amri ya ‘mandamus.’

Aliwataja mawakili wanakaomuwakilisha kwenye rufaa yake hiyo kuwa ni Dk. Rugemeleza Nshala na Stephen Mwakibolwa.

Wakili Mpoki alisema atafungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Mawakili, Jaji Ntale kwa kukiuka haki yake ya kufanya kazi.

Wakili Mpale Mpoki

“Uwakili ni kazi yangu, mtu akikufungia bila sababu ya msingi, bila kufuata utaratibu anakiuka hicho kifungu cha katiba. Lakini ikumbukwe kwamba kazi ndiyo inanifanya mimi niishi.

“Kwahiyo ukinifungia kufanya kazi kwa sababu ambazo unazijua wewe ina maana unataka nisiwe na maisha,” alisema Wakili Mpoki.

Aliitaja kesi nyingine anayokusudia kufungua ni ya kupinga baadhi ya vifungu katika sheria ya mawakili vinavyokiuka haki ya msingi ya mawakili.

“Nakusudia kufungua kesi nyingine ya kikatiba kupinga baadhi ya vifungu katika sheria ya mawakili ambavyo vinakiuka haki ya msingi ya mawakili.

“Sheria hiyo ni ya kizamani sana, haiendani na tamko la haki za binadamu ambalo lipo katika katiba yetu na kwa misingi hiyo haitakiwa kuwepo katika vitabu vya sheria.

“Huwezi kuwa na kamati ambayo mlalamikaji anajigeuza hapo hapo anakuwa mwendesha mashtaka, anakuwa mwamuzi. Tutapeleka kesi ya kikatiba kupinga vifungu kandamizi ambavyo vipo katika hiyo sheria ya mawakili,” alisema Wakili Mpoki.

Katika mlolongo huo wa kesi anazokusudia kufungua, atakayofungua Mahakama ya Haki Afrika Mashariki kupinga kusimamishwa uwakili.

“Naamini kitendo hiki hakiendani na ibara ya 6d ya mkataba wa ushirikiano wa Afrika Mashariki ambao unasisitiza kwamba moja kati ya ‘fundamental objective,’ (malengo ya msingi) ni kulinda haki za binadamu kama zilivyoainishwa katika tamko la haki za binadamu la Afrika,” alisema.

Aidha, Wakili Mpoki anakusudia kupeleka malalamiko kwenye tume ya maadili ya utendaji kazi za majaji inayoundwa chini ya sheria namba 4 ya mwaka 2011.

Alisema malalamiko yaje ni ya kupinga mwenendo wa Jaji Ntale na kuonyesha kuwa alikiuka maadili na kiapo chake cha ujaji.

Jaji Kilekamajanga Ntale

Wakili Mpoki alisema katika malalamiko yake hayo ataambatanisha viapo vya mawakili wote waliokuwepo kwenye kamati siku aliposimamishwa uwakili.

“Wataelezea siyo tu kitendo cha mimi kufungiwa, lakini vitu kadhaa ambavyo vilitokea kabla hatujaanza mwenendo siku hiyo,” alisema na kuongeza kuwa;

“Nakusudia kutumia nguvu zangu zote katika kipindi hiki cha miezi sita, kuwashawishi wanachama wa Chama cha Sheria Tanganyika (TLS) kuitisha mkutano mkuu maalumu kwa kufuata utaratibu uliowekwa, kifungu cha 22 cha sheria ya kuanzishwa Chama cha Wanasheria Tanganyika.

“Uitishwe mkutano mkuu maalumu wa wanasheria wote Tanzania ambao utakuwa na ajenda moja tu, nayo ni kujadili vitendo vilivyofanywa kinyume na sheria na katiba na Mwenyekiti wa Tume ya Maadili  ya Mawakili. Nafanya hivyo kwa sababu kitendo cha mimi kusimamishwa siyo kitendo dhidi yangu ila ni shambuliio dhidi ya mawakili wote.

“Ni shambulio dhidi ya taaluma, ni shambulio dhidi ya uhuru wa mawakili. Nitaomba wanachama wa Chama cha Sheria Tanganyika watoe uamuzi tuendelee vipi na huyu jaji aliyefanya kitendo cha kinyama,” alisema.

Kesi ya mwisho anayotarajia kumfungulia Jaji Ntale alisema ni kesi ya madai na atamdai fidia kwa kumsimamisha kufanya kazi ya uwakili.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya