MWANDISHI MAALUMU
SERIKALI imewapiga marufuku walimu na madaktari kusimamia miradi ya ujenzi inayotekelezwa na serikali katika maeneo yao ya kazi.
Marufuku hiyo ya Serikali imetangazwa hivi karibuni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa vyumba viwili vya maabara katika Shule ya Sekondari Rudi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kibakwe, mkaoni Dodoma.
Simbachawene ambaye alikuwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi katika Jimbo la Kibakwe alisema, walimu na madaktari hawapaswi kusimamia miradi ya ujenzi kwa sababu hawana taaaluma ya ujenzi.
Aliitaka Halmashauri ya Mpwapwa kuacha kuwatumia watumishi wa kada hizo kwa sababu ni matumizi mabaya ya rasilimali watu na ni chanzo cha utekelezaji wenye viwango duni vya ujenzi.
“Kwa sasa majengo yetu yanajengwa na walimu na madaktari badala ya kujengwa na wahandisi wa ujenzi, hili halikubariki hata kidogo.
“Makamu mwenyekiti wa halmashauri ajirini wataalamu wa ujenzi hata kwa ajira ya mkataba ili waweze kusimamia ujenzi. Haiwezekani miradi yetu isimamiwe na walimu na madaktari ambao sio wahandisi wa majengo,” alisema Simbachawene
Aidha, Simbachawene aliwataka madiwani wa Halmashauri ya Mpwapwa kujiepusha na tabia ya kuchukua tenda za miradi ya ujenzi inayotekelezwa ndani ya halmashauri hiyo.
Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Richard Maponda alisema maekezo yaliyotolewa na Simbachawene yatasimamiwa kikamlifu.