Saturday, April 19, 2025
spot_img

‘JANUARY, MAHARAGE WASHTAKIWE KWA WIZI, UHUJUMU UCHUMI’

RIPOTA PANORAMA

PENDEKEZO la kushitakiwa mahakamani, aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), Maharage Chande, limewasilishwa bungeni.

Pamoja nao, Mkurugenzi wa Kampuni ya Arab Contractors yenye kandarasi ya ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, naye jina lake limependekezwa kuunganishwa kwenye mashtaka hayo ya wizi na uhujumu uchumi.

Pendekezo hilo lilitolewa bungeni Novemba 3, 2023 na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Joelson Mpina alipokuwa akichangia Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/2022.    

Akichangia, Mpina aliliomba Bunge liiagize Serikali iwashtaki Waziri Makamba, Maharage, iliyokuwa Bodi ya Tanesco na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Arab Contractors kwa makosa ya kula njama, kuiibia serikali na uhujumu uchumi.

Sambamba na hilo, Mpina alisema serikali ihakikishe Shilingi bilioni 327.93 ambazo ni fedha za umma zinalipwa na Kampuni ya Arab Contractors kwa kuchelewa kukamilisha kazi ya ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere kama ilivyotamkwa kwenye mkataba.

“Kwa kuwa Serikali haina majibu ya msingi kuhusu hoja hiyo ya CAG kutoza faini ya ucheleweshaji, kiasi cha Shilingi bilioni

327.93 kwa mkandarasi, Kamp;uni ya Arab Contractors na kwa kuwa bunge lilishaiagiza serikali kutoza faini hiyo muda mrefu lakini waziri amekaidi maagizo ya bunge (ushahidi wa hansard) hali inayoonyesha kuna njama baina ya watumishi wa umma na mkandarasi kuwaibia watanzania.

“Hivyo basi, kwa kuwa hoja hii haikuletwa na kamati, naomba kuongeza mapendekezo mapya mawili, kwamba bunge liiagize serikali kufanya yafuatayo;

“Aliyekuwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande na iliyokuwa Bodi ya Tanesco na Mkurugenzi wa Kampuni ya Arab Contractors, wakamatwe na washtakiwe kwa makosa ya kula njama na kuiibia serikali na makosa ya uhujumu uchumi,” alisema Mpina.

Luhaga Mpina

Katika mchango wake huo, Mpina alisema taarifa ya kamati iliyowasilishwa bungeni haikuzungumzia tozo ya fidia ya ucheleweshaji wa mkataba wa ujenzi inayopaswa kulipwa na mkandarasi, inayofikia Shilingi bilioni 327.93.

Alisema wakati kamati ikiacha kuzungumzia hilo, taarifa yamajumuisho ya majibu ya serikali na mpango kazi wa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG, ukurasa wa 606, hoja namba 8 katika aya ya 4.3; Serikali inaeleza Manejimenti ya Tanesco ilitoa nyongeza ya muda bila kuzingatia sheria na mkataba (ex gratia time.)

Kwamba mkandarasi anatakiwa kuzingatia sheria na mkataba kukamilisha kazi vinginevyo alipaswa kuanza kutozwa faini Juni 15, 2023.

Anaeleza zaidi kuwa katika ukaguzi wake CAG hakukuta jitihada zozote zinazofanywa na Manejimenti ya Tanesco kudai tozo ya fidia ya ucheleweshaji wa mwaka mmoja wa mradi.

“Tozo ya fidia ya ucheleweshaji ya asilimia 5 ya thamani ya mradi imewekwa katika kifungu cha 8.7, kifungu kidogo cha 2.5,” alisema.

Alisema wakati Tanesco akiacha kudai fidia hiyo, imekuwa ikiilipa faini na adhabu zote kampuni ya Arab Contractors inapokiuka mkataba na kutoa mfano wa kukosekana kwa umeme eneo la ujenzi wa mradi.

“Waziri wa Nishati na Menejimenti ya Tanesco hawana mamlaka kisheria kufuta mapato ya nchi, kiasi cha Shilingi bilioni 327.93. Wabunge tulihoji hapa bungeni sababu za kutotozwa faini hii, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na

Kamati ya Nishati kwa nyakati tofauti tofauti ziliripoti bungeni kuwa ucheleweshaji wa mradi ulisababishwana uzembe wa mkandarasi.

“Nini kilichowasukuma Waziri wa Nishati na Menejimenti ya Tanesco kutoa ex gratia time kwa kampuni iliyozembea?

Aliyekuwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Januari Makamba katika jitihada za kumlinda Mkandarasi, Kampuni yaArab Contractors isilipe faini hiyo kwa nyakati tofauti, ndani ya Bunge (ushahidi wa hansard…)

Maharage Chande

“Alieleza kuwa ucheleweshaji huo ulisababishwa na Uviko-19, kuchelewa kufika kwa Crane na kupinga hadharanimuda aliyopewa mkandarasi katika mkataba akisema ulikuwa mfupi mno, asingeweza kukamilisha ujenzi.

“Maelezo ambayo yalikinzana na taarifa ya kitaalamu iliyotolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Injinia Leonard Masanja katika Kamati ya Bajeti. Pia Maelezo hayo yalipingwa vikali na wabunge lakini bado waziri akaenda kutoa Ex Gratia time kwa mkandarasi,” alisema Mpina.

Pendekezo la Mpina kutaka Waziri Makamba, Maharage na wenzao washtakiwe kwa wizi na uhujumu uchumi limekuja ikiwa ni takribani miezi nane sasa tangu CAG alipokabidhi ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2021/2022 kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambayo pamoja na mambo mengine mengi ilieleza wazi kuwa Serikali inapaswa kulipwa tozo ya fidia hiyo na mkandarasi kwa ucheleshaji wa mkataba.

“Kifungu cha 8.7 cha masharti ya jumla kinaeleza kuwa, iwapo mkandarasi atashindwa kuzingatia kifungu kidogo cha 2.5 (muda wa kukamilisha kazi) mkandarasi atalazimika kulipa fidia (madai ya mwajiri) ya ucheleweshaji wa kukamilisha kazi.

“Tanesco haikutoa tahadhari ya mapema kwa mkandarasi juu ya ucheleweshaji wa mradi na kusababisha kutotoza toza au fidia za ucheleweshaji kwa mkandarasi tangu kipindi cha kumaliza mradikilipopita, yaani tarehe 14 Juni, 2022.

“Mkandarasi alitakiwa kulipa fidia ya asilimia 0.1 ya bei ya mkataba kwa kila siku iliyochelewa, sawa na Sh. 6,558,579,983.50.

“Fidia ya juu zaidi ya ucheleweshaji ilipaswa kuwa asilimia 5 ya bei ya mkataba (Sh.6,558,579,983,500.28) sawa na Sh. 327,928,999,175.01. Hii ingeweza kusaidia athari zilizosababishwa na ucheleweshaji wa mradi na gharama zilizoongezeka kutokana na mfumuko wa bei,” inasomeka ripoti ya CAG.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya