*Yawaomba radhi kwa ukatili iliofanya Vita ya Majimaji
RIPOTA PANORAMA
UJERUMANI imewaangukia watanzania ikiwaomba radhi kwa ukatili iliofanya wakati wa Vita ya Majimaji iliyopiganwa kuanzia mwaka 1905 hadi mwaka 1907.
Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Dk. Frank-Walter Steinmeier ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu, amewaomba radhi watanzania leo kwa ukatili waliofanyiwa na wajerumani akiwa mkoani Songea alikotembelea makumbusho ya Vita ya Majimaji.
Rais Steinmeier amesema ipo haja ya kutafuta majibu ya maswali magumu kuhusu vita hiyo ili kujenga uhusiano mzuri baina ya Tanzania na Ujerumani.
Amesema amejifunza historia ya Vita ya Majimaji na akiwa kwenye makumbusho hiyo aliweka shada la maua kwenye kaburi la halaiki la mashujaa 66 walionyongwa na wajerumani wakati wa Vita ya Majimaji na pia aliweka shada la maua kwenye kaburi la kiongozi wa vita hiyo, Nduna Songea Mbano.
Nduna Songea Mbano
“Vile vile, ana kwa ana, ninaomba msamaha kwa mambo yote ambayo wajerumani waliwatendea mabibi na mababu zenu hapa,” amesema Rais Steinmeier.
Ameeleza furaha yake kujifunza historia ya shujaa Nduna Songea Mbano kwa undani na kukutana na familia yake; na kwamba ameguswa na namna watanzania wanavyohuzunishwa na historia ya mashujaa wao na jinsi ilivyoathiri kizazi cha sasa.
Rais Steinmeier amesema wajerumani wanaoifahamu historia ya Vita ya Majimaji ni wachache hivyo anaibeba kwenda nayo kwao, Ujerumani akawaeleze watu wake historia ya matukio yaliyotokea nyuma ili kuendelea kujenga na kuboresha historia njema ya Tanzania na Ujerumani huko tuendako.