ABDUL NONDO
Miswada mitatu imesomwa kwa mara ya kwanza kwenye mkutano wa 13 wa bunge ulimalizika Novemba, 2023 Jijini Dodoma. Miswada hiyo ni wa sheria ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani; sheria ya tume ya taifa ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa.
Hii inatoa fursa kwa wananchi, vyama vya siasa, wadau na wana demokrasia kuchambua, kujadili na kubainisha maeneo yenye upungufu kabla ya Januari/ Februari 2024, ambapo itasomwa kwa mara ya pili.
Ni muhimu sana wadau, vyama vya siasa na wananchi wote kutumia muda wetu kubainisha upungufu katika miswada hii kuliko kuishia kulalamika tu kwamba hakuna kilichofanyika.
Ni fursa yetu kutumia muda huu kuonesha upungufu na tupaze sauti bunge lisikie na serikali isikie upungufu uliopo ili ufanyiwe marekebisho kabla miswada hii haijapitishwa.
Nimejaribu kupitia maeneo kadhaa machache yenye upungufu katika miswada miwili, muswada wa sheria ya tume ya uchaguzi na muswada wa sheria ya uchaguzi. Naanza na muswada wa sheria ya tume ya uchaguzi.
MUSWADA WA SHERIA YA TUME YA UCHAGUZI
Muswada wa sheria ya tume ya uchaguzi umetungwa kwa mujibu wa katiba ya 1977, ibara ya 74(1) inayozungumzia uwepo wa tume ya uchaguzi. Sheria hii ina upungufu kadhaa.
Abdul Nondo
Kifungu cha 7(1) cha muswada wa tume ya uchaguzi. Kifungu hiki kimetaja sifa ya mwenyekiti wa tume na makamu mwenyekiti, (awe Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani /wakili miaka 10. Kifungu cha 7(2) kimetaja sifa za wajumbe wa tume.
Kifungu hakijataja sifa ya kutokuwa mwanachama wa chama cha siasa au kiongozi wa chama cha siasa. Sheria ilipaswa iguse na kuweka sharti hili kama ilivyoainishwa kwenye katiba, ibara ya 74(3)d.
Tumekuwa na majaji wengi ambao ni makada wa chama. Kutokuweka kifungu hiki ni kutengeneza mwanya. Haitoshi kusema mjumbe wa tume awe raia muaminifu bila kuweka sharti la kutokuwa mwanachama au kujihusisha na chama cha siasa.
Ni kama kuruhusu wajumbe wa tume wakatumikie vyama vyao na kutii maagizo ya vyama vyao.
Kifungu cha 9(3) cha muswada wa tume ya uchaguzi. Mkurugenzi wa uchaguzi atakuwa katibu wa kamati ya usaili, kamati yenye jukumu la kufanya usaili wa wajumbe wa tume ya uchaguzi na kupendekeza kwa rais majina.
Ukisoma tena kifungu cha 18(1) kinasema kutakuwa na mkurugenzi wa uchaguzi atakayechaguliwa na rais baada ya kupendekezwa na tume ya uchaguzi.
Kipi kinaanza? kwa sababu tume ya uchaguzi inampendekeza mkurugenzi wa uchaguzi kwa rais; upatikanaji wa tume hiyo unatokana na kamati ya usaili ambayo mkurugenzi wa uchaguzi ni katibu wa kamati hiyo ya usaili.
Kipi kinaanza? mkurugenzi wa uchaguzi katokea wapi kuwa katibu wa kamati ya usaili kabla ya tume ya uchaguzi kupatikana na kumpendekeza kwa rais kwa uteuzi? (Swali hili ni sawa na swali la yai na kuku kipi kilianza?)
Nakubaliana na mapendekezo ya mwanaharakati wa demokrasia, katiba na haki za binadamu, Deus Kibamba anaposema kunapaswa kuwe na chemba mbili ndani ya tume ya uchaguzi yaani bodi na menejimenti.
Mwenyekiti wa bodi awe mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ambapo bodi ndio itapaswa kufanya mchakato wa kuajiri mkurugenzi wa tume kwa mchakato wa wazi, watu kuomba na sio lazima mkurugenzi wa uchaguzi atokane na watumishi wa umma kama ilivyoainishwa kwenye muswada wa sheria ya uchaguzi kifungu cha 8(1)(2).
Wapiga kura
Huyu mkurugenzi ndio atakuwa mtendaji mkuu na ataongoza menejimenti katika utendaji wa kila siku kwa sababu mkurugenzi wa uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 20(1)(3) cha muswada wa tume ya uchaguzi, ndio mtendaji mkuu wa tume na msimamizi mkuu na anaweza kukasimishwa majukumu na tume kwa mujibu wa kifungu cha 11(2) cha muswada wa tume ya uchaguzi.
Hivyo, bodi ya tume ya uchaguzi ndio inapaswa kumsimamia mkurugenzi na menejimenti yake (dhana ya Principal-Agency Model au Principal -Agent Model).
Kifungu cha 9(3) cha muswada wa tume ya uchaguzi kifutwe, mkurugenzi hapaswi kuwa katibu wa kamati ya usaili, kufanya hivyo ni vigumu tume itakayopatikana kumsimamia.
Kifungu cha 21(1) muswada wa tume ya uchaguzi. Mtumishi aliyeteuliwa, aliyeazimwa na tume katika kipindi cha kutekeleza majukumu yake atachukuliwa kama mtumishi wa tume.
Ni jambo la kushangaza tume ya uchaguzi kuendelea kuazima watumishi. Na hili limejidhihirisha wazi kwenye muswada wa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi, kifungu cha 6(1) kinachotaja wakurugenzi wa jiji, manispaa, miji, halmashauri atakuwa msimamizi wa uchaguzi jimbo na kata.
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu imeshatoa hukumu Mwezi Juni, 2023 katika kesi iliyofunguliwa na Mwanaharakati Babu Chacha Wangwe kuzuia wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi na mahakama ilitoa miezi 12 (mwaka mmoja) kwa serikali kufanya marekebisho ya sheria ya uchaguzi.
Hawa wakurugenzi ni makada wa CCM, hawana uhalali wa kusimamia chaguzi zetu. Ni hoja dhaifu na isiyo na mashiko kusema uanachama wao unaondoka kupitia muswada wa sheria ya uchaguzi, kifungu cha 6(6) kwamba atajivua uanachama wake kwa kula kiapo mbele ya hakimu.
Miaka yote hawa wamekuwa wakila viapo ila wamekuwa wakisaidia chama chao na mwenyekiti wa chama chao ambaye ndio mteule wao.
Wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi itafanya uchaguzi kuvurugika sababu tume yenyewe haiwezi kumuwajibisha mkurugenzi wa halmashauri ambaye ni msimamizi wa uchaguzi kwa sababu mamlaka ya uteuzi na nidhamu ni rais ambaye ni mwenyekiti wa chama chake hivyo MaDED hawawezi tenda haki na usawa. Kifungu hiki kurekebishwe.
Tume ya uchaguzi iajiri watumishi wake ngazi ya kila wilaya kwa ajira za muda na za kudumu. Ajira zitangazwe watu waombe kwa uwazi, usaili ufanyike na iache kutumia wakurugenzi wa halmashauri. Pia tume ya uchaguzi iwe na ofisi zake kila mkoa na wilaya.
Kifungu cha 22 cha muswada wa sheria ya tume ya uchaguzi kinazungumzia fedha za uendeshaji wa shughuli za tume zitatoka katika bajeti ya serikali, yaani chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Ndio wapange waipe shilingi ngapi tume na lini waiombee fedha tume kutoka mfuko wa hazina. Hii haifai na inadhoofisha uhuru wa tume ya uchaguzi katika kutekeleza majukumu yake.
Fedha ya kuendesha shughuli za tume zitoke kwenye mfuko mkuu wa serikali (Consolidated Fund) ambapo ni fedha zenye uhakika, zenye taratibu nzuri na ambazo haziguswi zikiingizwa huko kuliko hivi sasa tume ya uchaguzi kupewa fedha kama hisani ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kifungu cha 23, muswada wa sheria ya tume ya uchaguzi kinasema tume itashauriana na waziri wa masuala ya utumishi kuandaa muundo wa utumishi wa sekretariati ya tume.
Kifungu hiki wazi wazi kinaonesha tume kuendelea kupokea maagizo na kuingiliwa na idara zingine za serikali. Uhuru huo upo wapi? Hii ni kinyume na kifungu cha 6(1) cha muswada wa tume ya uchaguzi.
Kifungu cha 8(2)(i)( ii) na (3) cha muswada wa tume ya uchaguzi kinatoa mamlaka kwa rais kumuondoa mjumbe wa tume ya uchaguzi baada ya kushauriwa na kamati ya uchunguzi.
Upungufu upo kwenye sababu za kumuondoa huyo mjumbe.
Imetaja kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake sababu ya maradhi au sababu nyingine yeyote. Sababu nyingine yeyote ndio sababu gani?
Imetaja tena tabia mbaya, tabia mbaya nini? Tafsiri ya tabia mbaya anatoa nani? Sababu ni neno ambalo ni subjective, kila mtu ana tafsiri yake.
Mjumbe anaweza kuwa na misimamo dhidi ya wengine katika kutenda haki na usawa akaambiwa ana tabia mbaya hivyo uhuru wa wajumbe ukitikisika tafsiri yake tume haiwezi kuwa huru, ulinzi kwa watumishi wa tume (security of tenure) ni muhimu sana.