Tuesday, December 24, 2024
spot_img

NGOs 16 ZAPAZA SAUTI UKIUKWAJI HAKI ZA BINADAMU

RIPOTA PANORAMA

MASHIRIKA Yasiyokuwa ya Kiserikali (NGOs)16 yamewanyooshea kidole baadhi ya viongozi na watumishi wa serikali kwa kukiuka haki za binadamu, utawala wa sheria na katiba..

Pia yamelalamikia kupuuzwa au kudharauliwa kwa maamuzi na amri za mahakama kunakofanywa na baadhi ya viongozi na watumishi wa serikali.

Akisoma taarifa ya mashirika hayo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mkuu wa Idara ya Utetezi Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Paul Kisabo alisema yanatoa wito wa kuheshimiwa kwa amri za mahakama na yanalaani vitendo vya kudharau amri halali za mahakama.

Wakili Kisabo alisema mashirika hayo yanatoa wito wa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa watumishi wa mahakama wanaoshiriki kuhujumu na kuwafilisi wafugaji kwa kutoa amri za kutaifisha na kuuza mali bila kufuata taratibu za kisheria.

“Tunalaani vikali kukiukwa haki za mifugo katika Wilaya ya Ngorongoro na maeneo mengine nchini ambapo mifugo imekuwa ikikamatwa, kuuzwa au kutaifishwa kinyume cha sheria na katiba ya nchi.

“Tunatoa wito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwaelekeza watumishi wa serikali hasa katika maeneo lalamikiwa kuheshimu maamuzi na amri za mahakama kwani amri za mahakama zinapaswa kuheshimiwa na kila mtu.

“Tunatoa wito kwa TANAPA na Jeshi la Polisi kuacha mara moja ukamataji wa mifugo kwenye maeneo ambayo kuna zuio la mahakama na waache kuwasumbua wafugaji kwani nao wana haki ya kumiliki mifugo kama mali halali kwa mujibu wa ibara ya 24 ya katiba ya nchi,” alisema Wakili Kisabo.

Mkuu wa Idara ya Utetezi Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Paul Kisabo

Akiendelea, Wakili Kisabo alisema mashirika hayo yanalaani kitendo cha watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutesa mifugo kwa kuwanyima malisho na maji kama njia ya kuwalazimisha wamiliki kulipa faini kwa kuhofia mifugo yao kufa.

Alisema mashirika hayo yanatoa wito kwa watumishi wa hifadhi za taifa kuacha tabia ya kuswaga mifugo na kuiingiza hifadhini kwa lengo la kutoza faini, kutaifisha na kuiuza na pia serikali kuchukua hatua za kisheria kwa watumishi na viongozi waliokiuka amri za mahakama.

“Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa mauaji yaliyotokea Mbarali, kutoa taarifa kwa umma na kuchukuliwa hatua kwa wahusika kwa mujibu wa sheria.

“Tunatoa wito wa jumla kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutekeleza maamuzi mbalimbali ya mahakama kisheria, mfano maamuzi ya mahakama za ndani, za kikanda na kimataifa.

Mifugo

“Maamuzi hayo ni kama kesi ya Rebecca Gyumi, Maria Mushi, Mjomba Mjomba, kesi ya THRDC, LHRC na MCT iliyoamriwa na Mahakama ya Afrika Mashariki mwaka 2019, THRDC na LHRC iliyoamriwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, kesi ya Mchungaji Mtikila, kesi ya Jebra Kambole na kesi ya Bob Wangwe ya wakurugenzi wa uchaguzi zilizoamriwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na nyingine nyingi,” alisema Wakili Kisabo.

Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali yaliyotoa tamko hilo ni Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),  Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC),  Shirika la Uraia na Msaada wa Kisheria (CILAO), Mtandao wa Mashirika ya Kifugaji (PINGOs Forum), Ujamaa Community Resource Team (UCRT) na Shirika la Kukuza Haki za Binadamu (OPH).

Mengine ni Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Shirika la Uhifadhi wa Mifumo ya Asili na Jadi (TEST), Shirika la Maendeleo Jumuishi wilayani Ngorongoro (IDINGO), Jukwaa la Ardhi Tanzania, Shirika la Kuinua na Kusaidia Maisha ya Wafugaji (PALISEP), Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), Green Planet Initiative (GPI) na Pan African Lawyers Union (PALU).

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya