RIPOTA PANORAMA
MIAKA 75 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR) inatarajiwa kuazimishwa kwa mdahalo wa kitaifa wa kutafakari ukuaji na hali ya ulinzi na haki za binadamu nchini.
Mdahalo huo wa siku mbili unaandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Shule ya Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSoL) na unatarajiwa kufanyika Novemba 23 na 24, mwaka huu katika Ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Taarifa kwa umma iliyotolewa hivi karibuni na mratibu wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Idara ya Utetezi Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Paul Kisabo inaeleza kuwa mgeni rasmi katika mdahalo huo atakuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku.
Wakili Kisabo ameeleza katika taarifa yake kuwa mdahalo huo unalenga kuwaleta pamoja watetezi wa haki za binadamu, viongozi wa serikali, wanazuoni, wanataaluma, wanasiasa na jamii ya kimataifa.
Anataja pia taasisi za kidini, asasi za kiraia na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali; makundi ambayo yataketi pamoja kuakisi ukuaji na ulinzi wa Haki za Binadamu nchini.
Wakili Kisabo anaeleza kuwa wakati wa mkutano huo kutakuwa na mawasilisho ya mada mbalimbali kuhusu ujumbe wa kufikiri juu ya safari ya haki za binadamu nchini Tanzania, tulikotoka, tulipo sasa na tuendako.
Anawataja watoa mada katika mdahalo huo kuwa ni Mary Rusimbi, Zlatan Milisic, Wakili Harold Sungusia, Dk. Hellen Kijo Bisimba, Dk. Veronica Bucheni, Jenerali Ulimwengu, Padre Charles Kitima, Dk. Richard Mbunda na Christine Garou.