RIPOTA PANORAMA
Moshi
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Makore Kisare akikata utepe kuashiria ufunguzi wa jengo jipya la utoaji huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) kwenye Hospitali ya TPC inayomilikiwa na Kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Moshi. (Picha na mpiga picha wetu)
HOSPITALI ya TPC na Hospitali ya Rufaa ya KCMC zinakamilisha utaratibu wa ushirikiano wa wataalamu wake wa afya unaolenga kuboresha huduma za kitabibu.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na meneja wa hospital hiyo, Razaro Urio wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la kisasa la huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) ambao mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makore.
Mpango wa ushirikiano huo baina ya Hospitali ya TPC yenye hadhi ya nyota nne inayomilikiwa na Kiwanda cha Sukari cha TPC na Hospital ya Rufaa ya KCMC utawahusisha madaktari bingwa, madaktari wanafunzi wa shahada ya pili ya udaktari na shahada ya uuguzi.
Urio alisema ushirikiano huo utaiwezesha Hospitali ya TPC inayotoa huduma kwa wananchi wanaoishi jirani na Kiwanda cha Sukari cha TPC na maeneo jirani hasa Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara kutoa huduma za kitabibu za kiwango cha juu .
Alisema zaidi ya Shilingi bilioni moja zimetumika kwa ajili ya upanuzi wa hospital hiyo pamoja na ukarabati wa majengo ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma.
“Kiasi hicho cha pesa pia kimetumika kujenga majengo mapya, kuboresha yaliyopo, kununua vifaa tiba na vya kutolea huduma.
“Ujenzi umehusisha wodi ya daraja la kwanza, wodi maalumu kwa ajili ya magonjwa ambukizi na jengo la mama na mtoto.
“Pia kuboresha wodi zote ikiwamo wodi ya kina mama, wodi ya wanaume, wodi ya watoto na kununua vifaa muhimu vya kutolea huduma ikiwamo gari la wagonjwa, mashine kwa ajili ya chumba cha upasuaji, ‘Utra Sound machine’, kiti cha huduma ya meno, kuongeza wataalamu wa tiba bobevu na kuboresha jengo hilo la OPD,” alisema Urio.
Aidha, Urio alisema Kiwanda cha TPC kimefadhili ujenzi wa zahanati tano katika Vijiji vya Mserekia, Loondoto, Mawala, Kiyungi, Chemchem sambamba na kuboresha zahanati ya Kijiji cha Mikocheni.
Alisema lengo la ufadhili huo ni mkakati wa kiwanda kufikisha huduma katika vijiji vilivyo mbali na Kiwanda cha TPC.
Wakati huo huo, menejimenti ya Kiwanda cha TPC imefungua milango kwa wakandarasi wake kutumia hospitali hiyo kutibu watumishi wao kwa kutumia fao la SHIB lililopo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Utaratibu huo utawezesha wananchi zaidi ya 4,500 kupata huduma kwenye hospitali hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Makore Kisare alipongeza juhudi zinazofanywa na kiwanda hicho katika nyanja mbali mbali ikiwamo utioaji huduma za afya kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho .
Alisema Serikali inathamini mchango unaotolewa na Sekta Binafsi kuwahudumia wananchi na kwamba suala la afya ni moja ya kipaumbele cha Serikali.
Alisisitiza Serikali kwa kutambua umuhimu wa suala la afya, imetoa Shilingi bilioni 1.8 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Kata ya Mabogini.
Alisema pia imetoa Shilingi milioni 870 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma katika Kituo cha Afya cha Uru Kusini, Shilingi milioni 500 kwa Kituo cha Afya Kahe na Shilingi milioni 500 katika Kituo cha Afya Marangu.
Mbali na kuwekeza kwenye Sekta ya Afya, kiwanda hicho kimekarabati majengo ya zamani na kujenga mapya kwenye shule ya awali, msingi na sekondari kwenye vijiji vilivyo ndani ya eneo la kiwanda hicho na maeneo ya jirani.