KAMPENI ya kudai madeni wadaiwa sugu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), yenye mambo nane muhimu inaendelea nchi nzima.
NHC lilizindua kampeni hiyo Agosti, mwaka huu; na ilianzishwa kutokana na kusuasua kwa wapangaji kulipa madeni wanayodaiwa na Shirika la Nyumba la Taifa.
Kampeni hiyo yenye mambo nane muhimu, yanalenga kuwezesha kukusanywa kwa madeni na moja ya mambo hayo ni kuwatangaza katika vyombo vya habari wapangaji ambao ni wadaiwa sugu.
Mpaka sasa NHC linawadai wapangaji wake Shilingi bilioni 23, ambazo kama lingezipata, zingewezesha kufanyika kwa shughuli mbalimbali za shirika ikiwemo ujenzi wa nyumba.
Taarifa ya kuzinduliwa kwa kampeni hii iliyotolewa Agosti 15, 2023 na Meneja Habari na Mawasiliano wa NHC, Muungano Saguya ikiwa na kaulimbiu ya ‘LIPA MADENI YAKO KWA MAENDELEO YA SHIRIKA NA TAIFA LETU,’ alieleza bayana kuwa, imeanzishwa baada ya kuisha kwa miezi mitatu iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha kikao cha Bunge, Julai 2023 alipoagiza wadaiwa wote wawe wamelipa madeni yao ndani ya miezi mitatu.
Aidha, kuanza kwa kampeni ya kukusanya madeni ya wapangaji, kunatokana na umuhimu wa shirika kuwa na fedha za kutekeleza miradi yake.
Kampeni hiyo ni mwendelezo wa jitihada za shirika za kukusanya madeni; ikitanguliwa na kampeni ya awali iliyowezesha kukusanywa kwa madeni ya kodi, Shilingi bilioni 5 kati ya Shilingi bilioni 28 ambazo NHC linawadai wapangaji wake wenye malimbikizo ya kodi za nyumba.
Akizungumza wakati wa kuzinduliwa kwa kampeni hiyo Agosti, mwaka huu, Saguya aliwaambiwa waandishi wa habari na wahariri wautangazie umma na wapangaji wa nyumba za NHC kuwa shirika hilo limeingia mikataba na wapangaji ya kuwaruhusu kulipa madeni yao kwa awamu; kila mpangaji anayodaiwa na kama ana changamoto za ulipaji ndani ya muda uliowekwa, ahakikishe anaweka utaratibu madhubuti wa kulipa madeni yake.
Kati ya mambo muhimu yaliyotajwa na Saguya kubebwa katika kampeni hiyo ni wapangaji waliopo kwenye nyumba (active tenants) ambao watashindwa kulipa kodi na malimbikizo yao ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu kuanza kwa kampeni, watakuwa wameonyesha kuwa hawahitaji nyumba walizopanga na shirika litavunja mikataba yao ya upangaji na kuwaondoa kwenye nyumba kwa mujibu wa sheria.
Kwamba, kwa wapangaji ambao walishapewa notisi mbalimbali za kulipa kodi wanayodaiwa, utekelezaji wa notisi hizo unaendelea kama notisi zinavyoelekeza hivyo shirika linawasihi watekeleze wajibu wao ili kuepuka usumbufu utakaojitokeza kwa kushindwa kutimiza wajibu huo.

Aliyekuwa Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula (katikati) Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah (kulia kwake) wakiwa na baadhi ya wapangaji wa nyumba za NHC.
Saguya alieleza zaidi kuwa NHC limeanzisha utaratibu mpya unaowataka wapangaji wapya kulipa amana ya pango (security deposit) ya miezi mitatu kabla ya kuingia na kuanza kuishi kwenye nyumba za shirika hilo. Kwamba utaratibu huo mpya utasaidia shirika kuzitumia amana (deposits) hizo pale wapangaji wanapoacha madeni na kuondoka kwenye nyumba..
Kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba na ambao hawajakamilisha kulipa amana ya pango inayotakiwa, alisema hao wameandikiwa barua na kupewa muda wa mpaka Disemba 31, 2023 wa kukamilisha kulipa amana za pango (security deposit), vinginevyo shirika litalazimika kusitisha mikataba yao ya upangaji.
Kwa mujibu wa Saguya, jambo la kuzingatiwa na wadaiwa wote ni kwamba shirika limeingia makubaliano na CREDIT INFO BUREAU ambayo itapeleka majina ya wadaiwa sugu wa NHC katika taasisi za kifedha ili wasikopeshwe na taasisi hizo.
Tahadhali iliyochukuliwa na NHC ili kuliepusha na madeni ya mara kwa mara iliyoelezwa na Saguya ni kuanzishwa kwa utaratibu wa kutotoa mkataba mpya kwa mpangaji ambaye atakuwa na rekodi mbaya ya kulipa kodi kwa wakati na kwa wapangaji waliopo, wanapaswa kufahamu kuwa Watanzania wengi wamekuwa wakiomba kupanga kwenye nyumba za NHC.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah
Kwa wadaiwa sugu watakaokaidi maelekezo ya shirika, Saguya alisema hao watakuwa wameruhusu shirika kuwatangaza katika vyombo vya habari ili mashirika na makampuni mengine yasiingie kwenye makubaliano ya kibiashara na mtu au kampuni inayodaiwa.
Mbali na hayo, Saguya alieleza kuwa ili kuhakikisha kodi na malimbikizo ya madeni ya NHC yanalipwa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Hamad Abdallah ameunda kamati ya menejimenti ambayo itakuwa na kazi ya kufuatilia madeni yote yanayodaiwa na shirika.
Kampeni hii ya NHC inafanyika chini ya kauli mbiu isemayo; LIPA MADENI YAKO KWA MAENDELEO YA SHIRIKA NA TAIFA LETU.