TERESIA MHAGAMA NA GODFREY LULINGA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amewasha mitambo ya kusambaza umeme katika vijiji vya Mubaba na Nyantakara vilivyopo Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera.
Biteko aliwasha mitambo hiyo hivi karibuni akiwa katika ziara ya kwanza ya kikazi mkoani Kagera tangu alipoteuliwa kushika wadhfa wa Naibu Waziri Mkuu.
Akizungumza na wananchi, mkandarasi na viongozi wa maeneo hayo, Biteko aliagiza sehemu zinazotoa huduma za kijamii, zikiwemo shule, visima vya maji na vituo vya afya zipewe kipaumbele cha kupelekewa umeme.
“Haileti maana umeme kufika katika eneo fulani kama watoto wanasoma gizani, haileti maana umeme kufika hapa halafu akinamama wanajifungulia gizani wala haina maana umeme kufika hapa wakati kuna vyanzo vya maji tunashindwa kuwapelekea maji.
“Ndio mana Rais wetu anataka mfikiwe na umeme ili usaidie kuboresha huduma na
kuchagiza shughuli za uchumi,” alisema Biteko.
Alitoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme na kuwakemee watu wanaoiba miundombinu yake ikiwemo nguzo na mafuta ya transfoma.
Biteko alimtaka mkandarasi kufanya kazi kadri ya mkataba wake unavyoelekeza na changamoto atakazokutana nazo azifikishe kwa viongozi.
Pia aliigiza REA kuwaondoa wakandarasi ambao hawafanyi kazi kwa mujibu wa mikataba yao.
Wakati huo huo, Biteko alieleza dhamira yake ya kusimamia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kudhibiti changamoto ya kukatika mara kwa mara kwa umeme ndani ya kipindi cha miezi sita.
“Agizo hili la Mheshimiwa Rais tutalisimamia na tutahakikisha shida hii
tunayoiona ndani ya kipindi cha miezi sita tunaipunguza kwa kiasi kikubwa
ili Watanzania wapate umeme wa uhakika,” alisema Biteko
Kuhusu nishati safi ya kupikia alisema Serikali ina mpango wa kuwawezesha wananchi kupunguza matumizi ya kuni na mkaa wa asili ambao una athari kwa afya.
Aliigiza REA kuandaa mpango wa kugawa mitungi ya gesi kwa wananchi kwa sababu lengo la Serikali ni kuwawezesha watanzania kutumia nishati safi.