Wednesday, December 25, 2024
spot_img

MAJALIWA AONYA WANAUME WAKWARE

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewaonya wanaume wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi wa kike na kusababisha waache masomo baada ya kuwapa mimba.

Onyo hilo alilitoa Septemba 22, 2023 alipokuwa akisalimiana na wananchi wa Kamachumu, mkoani Kagera akiwa njiani kuelekea eneo la Nshamba kukagua miradi ya maendeleo na mipango ya maendeleo.

“Hapa Kamachumu iko changamoto ya wanafunzi wa kike, ndoto zao zinafifishwa. Niwatangazie wanaume, achana kabisa na matamanio ya mtoto wa kike. Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza kwa kumlinda mtoto wa kike na hii haimaanishi kwamba hamlindi mtoto wa kiume.

“Rais wetu ametoa fedha nyingi za kujenga shule za sekondari kwa hiyo Halmashauri tengeni fedha za mapato ya ndani kujenga mabweni kwani mnao uwezo huo. Makusanyo yenu yako juu, mnakusanya Shilingi bilioni saba kwa mwaka kwa hiyo mkitenga kila miezi mitatu mtaweza kujenga haya mabweni,” alisema Majaliwa.

Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, mtu akikutwa na kosa la kumpa mimba mwanafunzi anastahili kifungo cha miaka 30 gerezani.

“Mwache mtoto wa kike asome kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. Mtoto wa mwenzio ni wa kwako, ni mwanao, siyo mkubwa  mwenzako,” alisema.Majaliwa.

Akiwa njiani kuelekea Magalini kukagua Soko la Kimataifa la Dagaa, Majaliwa alisalimiana wakazi wa Nshamba na kuwaelezea mpango wa Serikali kusogeza huduma za kijamii kwenye sekta zote.

Majaliwa ambaye yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu, pia alikagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Ndolage na kuagiza ujenzi wake ukamimilike ifikapo Novemba, 2023.

“Nimekagua ujenzi wa majengo mapya, naona kazi ni nzuri. Hawa mafundi waendelee na kasi hii na ujenzi ukamilike ifikapo Novemba kama mlivyoahidi ili Disemba, 2023 tuanze usajili wa wanafunzi na Januari, mwakani vijana wetu waanze masomo,” alisema.

Majaliwa alisema ili kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana, Rais Samia ameagiza kuimarishwa vyuo vya ufundi stadi nchini ili vijana waweze kupata stadi na kujiajiri.

“Chuo hiki kinaweza kuchukua vijana wa ngazi zote hata wa chuo kikuu. Hapa wakija wanakuja kupata ujuzi iwe ni wa kuchomelea nondo au kusuka kwani mtu anaweza kuwa na digrii yake lakini hawezi kuchomelea nondo,” alisema Majaliwa.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore alisema Serikali ilitoa Shilingi millioni 903.5 kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho kwa kuongeza miundombinu ya majengo ili kufikia viwango vya chuo cha wilaya.

“Upanuzi wa chuo unahusisha ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80, moja la wavulana na jingine la wasichana, bwalo la chakula lenye uwezo wa kuhudumia watu 200, karakana ya umeme, karakana ya uungaji na uundaji vyuma, nyumba ya mkuu wa chuo na jiko,” alisema.

Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Juni, 2023 na sasa umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2023.

“Upanuzi wa chuo hiki utawezesha kuanza kudahili wanafunzi wa bweni kwani hivi sasa chuo kinatoa mafunzo kwa wanafunzi wa kutwa pekee kwa kuwa hakina miundombinu muhimu kama mabweni, bwalo, jiko na nyumba za watumishi,” alisema.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya