Wednesday, June 25, 2025
spot_img

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAJIKANYAGA

RIPOTI PANORAMA

SKANDALI inayomuhusu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa (TAMISEMI), kutokomea na gari la mradi wa uhifadhi lilitolewa msaada kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Taasisi ya Frankfurt Zoological Society (FZS), haina chembe ya uzushi wala uongo.

Taarifa ya kukanusha habari hiyo, iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele inamfanya msemaji huyo kuwa na ndimi mbili kwa sababu alichokikanusha ndicho alichokitolea ushuhuda yeye (John Mapepele) kwa Tanzania PANORAMA Blog alipothibitisha Waziri Mchengerwa kutokomea na gari hilo.

Katika taarifa yake hiyo aliyoitoa leo na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii, Mapepele anaeleza kuwa wizara inakanusha habari iliyoripotiwa na Tanzania PANORAMA Blog kuwa ni uzushi na uongo na kwamba hakuna gari lolote la wizara lililopotea na kwamba ingetokea hivyo wizara ingeishatoa ripoti kwa vyombo husika.

Sehemu ya tamko hilo la Mapepele inasomeka hivi “Pia Wizara inapenda kufafanua kuwa gari linalozungumziwa ni gari la Taasisi ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA), gari hilo awali liliazimwa wizarani kwa utaratibu wa kawaida na kwa barua yenye kumb Na. A. B. 307/402/01/38 limeombwa kutumika kwa muda Ofisi ya Rais – TAMISEMI na kufuata taratibu zote za Serikali.

Kwa taarifa hii, wizara inasisitiza umma kupuuza habari hizo ambazo kwa sasa hatua kali za kisheria zinachukuliwa kwa wahusika.

Tanzania PANORAMA Blog tunasisitiza kuwa habari kuhusu Waziri Mchengerwa kutokomea na gari aina ya Nisaan Patrol – Wagon V8 GID haina chembe ya uzushi wala uongo na ilithibitishwa na Msemaji wa Waziri wa Maliasili na Utalii, John Mapepele katika mazungumzo ya simu ya zaidi ya dakika 40 aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog; na aidha hajairipoti kuwa limepotea bali Waziri Mchengerwa katokomea nalo.

Katika mazungumzo hayo Mapepele alisema siyo Waziri Mchengerwa peke yake bali wapo mawaziri wengi na viongozi wengi ambao wanapoteuliwa kuwa mawaziri na viongozi na kukuta magari waliyopangiwa siyo mazuri, huwa wanachukua ya taasisi kuyatumia.

Mapepele alisema alichokifanya Waziri Mchengerwa kinafanywa na mawaziri, makatibu wakuu na viongozi wengine wengi lakini alichokosea Waziri Mchegerwa ni kutolirudisha gari hilo baada ya kuhamishwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda TAMISEMI.

Pamoja na mambo mengine mengi, Mapepele alipoulizwa iwapo ana ufahamu wowote kuhusu kiapo cha maadili kwa viongozi wa umma alibaki kubung’aa na kusema sasa Waziri Mchengerwa anapaswa kulirudisha gari hilo alilotokomea nalo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya