Wednesday, June 25, 2025
spot_img

WAZIRI MKUU APIGWA BUTWAA FEDHA ZA UMMA ZINAVYOTAFUNWA KIGOMA

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

Kigoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza kushangazwa kwake na matumizi mabaya ya fedha za umma katika Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Kigoma.

Akizungumza na viongozi wa dini, Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma, Ijumaa, Septemba 22, 2023 katika  ukumbi wa NSSF, Kigoma Mjini, Majaliwa alisema fedha zinazotolewa na Serikali zinakaa kwenye akaunti kwa muda mrefu kisha zinatolewa na kupelekwa kusikojulikana.

Alisema Manispaa ya Kigoma ilipokea Sh. milioni 500 kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambazo zilikaa kwenye akaunti kwa muda mrefu kabla ya kutolewa na hazijulikani zilitumika kwa kazi gani.

“Kuna kiasi kingine cha Shilingi milioni 447 kilitumwa Kigoma, wakati zinaandaliwa kutoka Mkurugenzi akazuia. Hongera Mkurugenzi na uendelee kuzizuia, sisi tunamfuatilia Mkurugenzi aliyekuwepo kwa sababu anajua zile Shilingi milioni 500 zilitokaje,” alisema Majaliwa.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma inakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo matumizi mabaya ya fedha, makusanyo kidogo sababu ya malumbano, mawakala kukaa na fedha mikononi badala ya kuzipeleka benki, Baraza la Madiwani kukosa taarifa za fedha na kutumia fedha za miradi kulipana posho.

“Kuna watu wamejilipa Shilingi milioni 11 zikiwa ni posho ya safari ya Dodoma. Pia wametumia Shilingi milioni sita kufanya service ya gari, hili ni gari la aina gani? Wengine wametumia Shilingi milioni tisa kwenye sherehe za siku ya mtoto wa Afrika na wengine wamejilipa Shilingi milioni 14. 8 kwenda kwenye sherehe za Nane Nane Tabora, hivi mlikaa siku ngapi huko?

“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti   kwa muda halafu zinapotea, hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi TAMISEMI ili tuone huo mnyororo unaenda wapi,” alisema Majaliwa.

Alisema fedha zinazotoka Serikali Kuu huwa zinatumwa na maelekezo mahsusi ya  kwamba zinaenda kufanya shughuli gani; na za makusanyo ya ndani maamuzi ya matumizi yake ni lazima yafanywe na baraza lote la madiwani. 

Majaliwa alisema ipo tume ya TAMISEMI ilikwenda kufanya uchunguzi kwenye halmashauri hiyo kuhusu matatizo hayo na aliitaka ikamilishe kazi yake haraka na kuiwasilisha kwa Waziri wa Nchi, OR TAMISEMI.

“Tume ikamilishe kazi haraka, akabidhiwe Waziri. Namwagiza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa akipokea taarifa ya tume hiyo, aje Kigoma achukue hatua,” alisema.

Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwaasa watumishi wa halmashauri zote mbili waache makundi kwani yanasababisha migongano na kuzorotesha utoaji huduma kwa wananchi.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya