Tuesday, August 26, 2025
spot_img

KIGOGO ATOKOMEA NA NISSAN PATROL YA MRADI

RIPOTA PANORAMA

KIGOGO Mwandamizi wa Serikali, (jina linahifadhiwa kwa muda kwa sababu hajazungumza) ametokomea na gari la kisasa la mradi wa uhifadhi, aina ya Nissan Patrol Wagon, lenye namba za usajili 02 JU 0484, lililotolewa kama msaada na Taasisi ya Frankfurt Zoological Society (FZS) kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA)

Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vya Tanzania PANORAMA Blog zimeeleza kuwa, kigogo huyo ametokomea na gari hilo mwezi Juni, mwaka huu baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya kutembelea hifadhi.

Inaelezwa kuwa, hadi sasa, ikiwa ni zaidi ya miezi mitatu tangu alipotokomea nalo, maafisa wa TANAPA wako kimya wakiogopa kumuomba alirejeshe kwa kile kinachodaiwa kuwa kigogo huyo hagusiki.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, gari hilo la kisasa lililotolewa na FZS kama msaada kwa TANAPA kwa ajili ya shughuli za uhifadhi lilikabidhiwa kwa mamlaka hiyo Disemba 20, 2022 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

“Hilo ni moja ya magari ya kisasa kabisa waliyopewa TANAPA kama msaada na Kampuni ya Frankfurt Zoological Society kwa ajili ya shughuli za uhifadhi. Yapo mawili hayo magari moja lipo Serengeti na yalitolewa msaada pamoja na yale ya TAWA. Huyo bwana mkubwa alipokuja kwenye ziara hifadhini, akapewa ili atumie kwenye hiyo ziara yake hifadhini lakini pasipo kutegemea, alipomaliza ziara akatokomea nalo mpaka leo.

“Alikuwa kwenye ziara Juni 18, 2023 ndiyo akapewa kwenda hifadhini, tangu hapo halikurudi, TANAPA wanaogopa kumuuliza kwa sababu hagusiki na ukimgusa umegusa pabaya, sasa linaoneka Dar es Salaam kwenye kumbi za starehe, mara liko Mkuranga, kiujumla hadithi ni ndefu na yenye kusikitisha kwa mtu huyo ambaye sasa ana nafasi nyeti serikalini,” alisema mmoja wa watoa taarifa wetu.

Taarifa za awali zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zilieleza kuwa gari hilo limeibiwa na alipoulizwa Meneja Mawasiliano wa TANAPA, Catherine Mbena alikanusha kwa kueleza kuwa katika data base yao, hakuna gari lililoibiwa.

“Imefanyaje?… wapi…imeibiwa maana yake nini? unamaanisha gari yetu imeibiwa? nitumie details za hiyo gari nifuatilie,” alisema Mbena na muda mfupi baada ya kutumiwa maelezo ya gari hiyo alipiga simu na kusema.

“Issue ni nini (anataja jina) issue uliyonayo ni ipi? gari yetu haijapotea. Mmepata hizo taarifa polisi? hamna gari yoyote iliyopotea, kama haijapotea ipo. Kwenye data base yetu hakuna gari iliyoibiwa wala kupotea. 

“Wewe ungekuja moja kwa moja kuwa mbona gari yenu labda imekuwa moja, mbili, tatu. Sasa kama una swali tofauti na la kuibiwa uliza?” alisema Mbena.

Alipoulizwa iwapo magari yote yaliyotolewa na FZC kwa ajili ya shughuli za uhifadhi yapo kwenye mradi kama inavyotakiwa, alisema hilo sasa ndiyo swali na kuomba muda atafute majibu.

Aliporejea kujibu, alisema “aisee, naomba tu nikwambie kwamba hakuna gari iliyoibiwa. magari yetu yapo na naomba niishie hapo tafadhali,” alisema Mbena kabla ya kukata simu.

Tanzania PANORAMA Blog imemtamfuta kwa simu yake ya kiganjani kigogo anayetajwa kutokomea na gari hilo lakini hakupokea mwito wa simu na hata alipotumiwa maswali kwenye simu yake, hakujibu.

Taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa baada ya kigogo huyo kubaini kuwa Tanzania PANORAMA Blog inafuatilia mahali ilipo gari hilo na uhusika wake wa kuliondoa kwenye eneo la mradi, sasa anafanya jitihada za kulirudisha huku akimtaja mmoja wa makatibu wakuu kuwa ndiye aliyemruhusu kulichukua kwa matumizi yake binafsi.

SOMA TANZANIA PANORAMA BLOG UPATE UNDANI ZAIDI WA MKASA HUU

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya