RIPOTA PANORAMA
RAIS Samia Suluhu Hasaan amewataka Watanzania watambue kuwa duniani kuna nchi Moja tu inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Taifa huru.
Amesema Taifa Huru la Tanzania limejengwa katika misingi ya amani, upendo na mshikamano na linaoongozwa kwa misingi ya Katiba na Sheria zilizotungwa na Bunge na sio utashi wa mtu au utashi wa mataifa mengine.
Hayo ameyasema jana katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia ya vyama vingi Vya siasa unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam ukiwa na ajande ya kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais Samia kufanyia kazi masuala yanayohusu demokrasia ya vyama vingi.
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha kwamba duniani kuna nchi moja tu inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Taufa huru. Na wenye Taifa hilo ni sisi tuko hapa. Uendeshaji wa Taifa hili utatokana na sisi tuliopo hapa.
“Hali kadhalika ni muhimu kutambua kwamba demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini kwetu itakuwa na maana kama tukidumisha amani, utulivu na umoja wa Taifa letu. Pamoja na ukweli kwamba uhuru ni sehemu muhimu ya demokrasia, lakini utii wa sheria una nafasi kubwa katika kuhakikisha uhuru wa kila mtu unaheshimiwa,” alisema Rais Samia.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia aliwataka wanasiasa na wadau wa siasa kuzingatia kuheshimiana wakiwa katika kazi za kisiasa na hata katika maisha ya kawaida.
“Mtu kumheshimu mtu mwingine au Serikali kumheshimu mtu. Na hapa nataka nizungumzie kidogo aliloniomba mwanangu, Mwenyekiti wa TCD, kwamba yule mwenzetu msamehe basi aje awe na sisi. Tunasema demokrasia ni kuheshimu Sheria.
“Unapoheshimu Sheria ndipo demokrasia inapokuwa lakini pia ndipo inapoleta heshima. Heshima ya mtu inakuja kwa kuheshimu Sheria za nchi. Unapovunja Sheria za nchi heshima yako haitoheshimiwa, Serikali haitokuheshimu,” alisema Rais Samia.
Alisisitiza kuwa ni muhimu mtu kujua anapotumia uhuru wake; unapoishia inaanza heshima ya mtu mwingine hivyo kila mmoja anapofanya shughuli zake kupima na kuzingatia hilo.
“Lakini lazima ujue kwamba unapotumia uhuru wako, mwisho wa uhuru wako inaanza heshima ya mtu mwingine. Kwa hiyo vyote hivyo lazima tuvipime ili tunapofanya shughuli zetu twende navyo hivyo. Isingekuwa uvunjifu wa Sheria leo isingemlazimu kuomba hapa kuwa yule mwenzetu muachie na hivi na hivi.
“Lakini unapovunja Sheria, unajivunjia heshima na Serikali inashindwa kukuheshimu. Naomba tufanye kazi kwa kuheshimu Sheria. Waswahili wanasema, mtaka nyingi nasaba hufanya nini? … ingawa kusameheana napo kupo. Kusameheana napo…,” alisema.
Rais Samia alisema ili kuifanya demokrasia inawiri ni lazima matakwa ya Sheria yaheshimiwe na aliwakumbusha viongozi wenzake wa kisiasa kuwa; wao ndiyo wanatumiaji wa sheria hizo hivyo inapotokea changamoto kwenye sheria hizo, wasisite kutoa maoni yao na Serikali itayasikia.
Aliviasa vyama vya siasa na asasi za kiraia kuheshimu Sheria ili uhuru na amani vitamalaki.
Aidha, alisema ametaarifiwa kuwa kuna vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa na vingine zaidi ya 10 vimeomba usajili.