RIPOTA PANORAMA
MKUTANO Maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoshirikisha wadau wa vyama vingi vya siasa, leo unaketi kujadili umuhimu wa R nne katika shughuli za kisiasa nchini.
Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Baraza la Vyama vya Siasa, unaoketi kwa siku tatu katika Ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Mlumbi wa mada hiyo ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA,) Profesa Mohamed Makame Haji.
Ratiba inaonyesha kuwa Mlumbi Profesa Haji katika mada hiyo atazungumzia umuhimu wa maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya wa Taifa ambayo ni falsafa ya Rais Samia katika uongozi wake.
Mada hiyo itajadiliwa kwa siku nzima ya leo na washiriki wa mkutano huo maalumu na Tanzania PANORAMA Blog itaripoti hatua kwa hatua mwenendo wa mjadala kabla ya kuhitimishwa na Profesa Haji.
Jana, baada ya kufunguliwa kwa mkutano huo na Rais Samia, mada ya kwanza iliyowasilishwa ilikuwa mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kufanyia kazi mambo yanayohusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
Profesa Rwekaza Mukandara ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Mstaafu na Mhadhiri Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndiye alikuwa Mlumbi katika mada hiyo.
Pamoja na mada hiyo, mada nyingine iliyowasilishwa jana ni utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi ambayo Mlumbi wake alikuwa mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kabla ya Profesa Mukandara kuhitimisha majadiliano ya mada hizo.
Mkutano Maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa unaowashirikisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi nchini unafanyika Jijini Dar es Salaam baada ya Rais Samia, Mei 26, 2023 kumuelekeza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuuandaa ili kuwapa fursa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kutathimini mapendekezo ya Kikosi Kazi, kulichofanyia kazi masuala yanayohusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa.