Tuesday, December 24, 2024
spot_img

DEMOKRASIA SI FUJO NA MATUSI- RAIS SAMIA

RIPOTA PANORAMA

RAIS Suluhu Hassan amesema kuwepo kwa vyama vingi na mawazo mbadala hapa nchini hakumaanisha kuwepo vurugu, fujo, kauli zenye ukakasi na vitisho zenye kuamsha hisia na kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.

Hayo ameyasema jana katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia ya vyama vingi unaojadili mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais Samia kufanyia kazi mambo yanayohusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa na hali ya siasa nchini.

Mkutano huo wa siku tatu ulifunguliwa jana na Rais Samia na unafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JNICC.)  

Alisema malengo makuu ya kuwapo kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa ni kuongeza kasi ya kuleta maendeleo kwa watu hivyo ni vema vyama vya siasa vinapofanywa shughuli zake kuzingatia hilo.

“Tumeweka vyama vingi, tulikuwa na nia ya kupanua demokrasia na kutoa wigo mpana kwa wananchi kuwa na uchaguzi lakini kupata fikra mbadala kwenye uendeshaji wa Serikali na si vinginevyo.

“Fursa ya kuwa na jukwaa la kutoa mawazo mbadala isiwe kibali cha kuendesha siasa za chuki na uhasama, na zinazokwamisha maendeleo ya wananchi.

Tukiendesha siasa za namna hiyo tutakuwa tunakwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, kwani hata katika nchi ambazo ndiko mfumo huu wa demokrasia ulikoasisiwa, kipaumbele hutolewa kwa ukomavu wa siasa ili kuendana na shughuli za maendeleo ya watu kuliko malumbano ya kisiasa wakiamini kwamba siasa ni nyenzo tu ya kuleta maendeleo,” alisema Rais Samia.

Alisema kwa kuzingatia hayo, kipaumbele kinapaswa kuwa maendeleo kwani siasa itachangia kwenye kuleta maendeleo.

Rais Samia aliwashauri viongozi wa kisiasa kutumia fursa ya kuwepo kwa vyama vingi vya siasa kuwaonyesha wananchi mambo watakayofanya ili kuongeza kasi ya maendeleo.

Baadhi ya washiriki wa mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa wakishiriki mkutano huo jana katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC)

“Siasa si kulumbana, siasa si matusi, siasa si kusema uongo. Huko nje kuna msemo wanasema ukitaka kusikia uongo nenda kwa wanasiasa. Lakini sio kweli, siasa sio kusema uongo. Siasa si lugha za dhihaka, maneno ya kashfa, kuchochea watu wasishiriki katika shughuli za maendeleo na kutotii sheria. Siasa si uchonganishi baina ya wananchi na Serikali yao.

“Siasa za aina hii hazina tija yoyote bali ni ukiukwaji wa kanuni za demokrasia ya ushindani. Tumeweka vyama vingi kuwe na demokrasia ya ushindani, sasa tukifanya haya hayana tija bali ni kukiuka kanuni za demokrasia ya ushindani,” alisema.

Rais Samia alisifu utamaduni uliopo wa wanasiasa na wadau wa siasa kukaa meza moja kuzungumza mambo yanayohusu maslahi ya Taifa.

“Utamaduni huu hutekelezwa katika nchi yetu kwa namna na ngazi mbalimbali. Kwa mfano katika ngazi ya mkoa kuna vikao vya Baraza la Ushauri la Mkoa na katika ngazi ya wilaya kuna vikao vya Baraza la Ushauri la Wilaya.

“Kwa hiyo hizo ni ngazi za vikao hivyo vya mashauriano. Katika vikao hivyo vyama vya siasa na wadau wengine hualikwa kushiriki na kutoa maoni yao,” alisema.

Rais Samia alisema lengo la utaratibu huo ni kuwashirikisha Watanzania kupitia viongozi wao wa taasisi zilizosajiliwa kuchangia mawazo katika uendeshaji wa nchi huku ikitambulika kuwa wananchi ni wadau muhimu na wana nafasi ya kutoa maoni yao katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.

Aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Baraza la Vyama vya Siasa kuendeleza utamaduni huo wa kidemokrasia.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya