Tuesday, June 17, 2025
spot_img

‘KOMBORA’ LA LISSU LAIIBUA MWIBA HOLDINGS

RIPOTA PANORAMA

KAMPUNI ya Mwiba Holdings Limited imekanusha kumiliki eneo la ekari milioni sita katika hifadhi ya mbunga za wanyama iliyopo Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Shinyanga.

Imesema madai kuwa inamiliki pande hilo kubwa la ardhi ndani ya eneo la hifadhi yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu, kwenye mikutano ya hadhara ya kisiasa iliyofanyika Agosti 11, 25 na 26 mwaka huu katika miji ya Sirari, Shinyanga na Kahama ni ya uongo na uzushi.

Imesisitiza kwamba Lissu ameisingizia Kampuni ya Mwiba Holdings Limited na Thomas Dan Friedkin, ambaye ni mmiliki wake na imetishia kukimbilia mahakamani kuwashtaki wanaosambaza taarifa hizo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na kampuni hiyo Septemba 4, mwaka huu na kusainiwa na mkurugenzi wake, Abdulkadir Luta Mohamed; haimiliki eneo lolote kwenye maeneo ya hifadhi hapa nchini bali ina mikataba miwili ya upangaji na mkataba mmoja wa uwekezaji.

Lissu, akiwa kwenye mikutano ya hadhara katika miji ya Sirari, Kahama na Shinyanga aliwaambia maelfu ya wanachama, wafuasi na mashabiki wa Chadema kuwa Kampuni ya Mwiba Holdings Limited inamilikiwa na tajiri wa kimarekani anayeitwa Thomas Dan Friedkin, na kwamba katika mtandao wake, yapo maelezo kuwa anamiliki ekari milioni sita katika maeneo ya hifadhi ya Tanzania.

“Kama una bando kwenye simu yako, google Mwiba Holdings utagundua yafuatayo. Ni kampuni ya tajiri mmoja wa Marekani, anaitwa Thomas Dan Friedkin. Kila mtu anaweza kuandika mwiba si ndiyo? Mwiba wa Kiswahili.

“Mwiba Holdings ni kampuni inayomilikiwa na huyu tajiri wa kimarekani, anaitwa Thomas Dan Friedkin. Kwa mnaopenda mpira ni mmiliki wa timu ya AC Rome ya Italia. Sasa ukifungua huo mtandao wake, ukienda kwenye hayo maelezo ya kampuni yake na ya kwake mwenyewe utakutana na maneno yanayosema kwamba huyu Thomas Dan Friedkin anamiliki ekari milioni sita katika maeneo ya hifadhi ya Tanzania.

“Ekari milioni sita….ukanda wote huu wa usukumani kuanzia Meatu mpaka Busega na mpaka Bunda na Tarime na Serengeti kuna vita kubwa inaendelea dhidi ya wananchi na hifadhi. Wananchi wanauawa, mifugo yao inanyang’anywa, inataifishwa, mingine inapigwa risasi na askari wetu. Wananchi wanateswa.

“Hii vita ya hifadhi, wananchi wanatakiwa waondolewe kwenye maeneo yao halafu kuna tajiri wa kimarekani amepewa ekari milioni sita za hifadhi. Kama una mtandao naomba uangalie haraka haraka usije ukasema natunga tunga,” alisema Lissu.

Ingawa katika hotuba yake hiyo, Lissu hakutaja pande hilo kubwa la ardhi lilitolewa kwa kampuni hiyo na awamu gani ya uongozi;  Taarifa ya kanusho la Kampuni ya Mwiba Holdings Limited inaeleza kuwa jumla ya eneo lote ambalo imepangishwa katika Wilaya ya Meatu ni ekari 21,604 na siyo ekari milioni sita kama ilivyodaiwa na iliyowaita wazushi. Kisha inasomeka zaidi kuwa;

Thomas Dan Friedkin

Wamiliki, akiwemo Thomas Dan Friedkin na uongozi wa Mwiba Holdings Limited wanakanusha taarifa za uongo zilizotolewa kwenye mikutano ya hadhara ya kisiasa iliyofanyika Agosti 11, 15 na 26, 2023 huko Sirari, Shinyanga na Kahama zilizodai kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeipa Kampuni ya Mwiba Holdings Limited umiliki wa ekari milioni sita za eneo la hifadhi ya mbuga za wanyama lililopo wilayani Meatu, mkoani Simiyu.

“Ukweli ni kuwa Kampuni ya Mwiba Holdings Limited haimiliki eneo lolote kwenye maeneo ya hifadhi nchini Tanzania. Katika Wilaya ya Meatu, Mwiba Holdings Limited ina mikataba miwili ya upangaji na mkataba mmoja wa uwekezaji kama ifuatavyo;

“Mikataba miwili ya upangaji wa ranchi za wanyamapori: wa kwanza Mwiba Holdings imeingia na Halmashauri ya Kijiji cha Makao na wa pili imeingia na Halmashauri ya Kijiji cha Mwangudo. Ranchi zote hizi kisheria zinamilikiwa na vijiji vya Makao na Mwangudo, mtawalia.

“Mkataba mmoja wa uwekezaji kwenye kitalu cha uwindaji cha kitalii ambacho Mwiba Holdings Limited imeingia na jumuiya ya uhifadhi wa wanyamapori ya makao makuu. Kitalu hiki kinamilikiwa na vijiji saba; Makao, Ginano, Mwabagimu, Saapa, Mwangudo, Iramba – Ndogo na Mbushi,” inasomeka taarifa hiyo.

Aidha, taarifa inaeleza zaidi kuwa Kampuni ya Mwiba Holdings haijaingia mkataba wowote (moja kwa moja au kupitia kwa mtu au taasisi nyingine) na Serikali ya Awamu ya Sita na kwamba mikataba yote ya upangaji na uwekezaji iliyotajwa imekuwepo kwa muda mrefu na iliongezewa muda mwaka 2018 na 2019 wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Inahitimishwa taarifa hiyo kwa onyo linalowataka wote wanaozusha na kusambaza taarifa za uzushi na uongo kuacha mara moja vinginevyo kampuni hiyo italazimika kuchukua hatua za kisheria.

Mnyukano huu baina ya Lissu na Kampuni ya Mwiba Holdings Limited umeibuka huku kukiwa bado na kumbukumbu ya kashfa kubwa iliyopata kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, ikizihusisha kampuni za bilionea Friedkin na ukwepaji mkubwa wa kodi ya Serikali na ubaguzi wa kimaslahi baina ya wafanyakazi wazawa na wageni wa kampuni za bilionea huyo zilizopo hapa nchini.

Kukiwa bado kuna sintofahamu kuhusu hatma ya tuhuma nzito zilizopata kuelekezewa kampuni za bilionea Friedkin, Tanzania PANORAMA itaripoti kwa kina sakata la kampuni za bilionea huyo, ikiwamo Mwiba Holdings Limited na uchunguzi uliopata kufanywa na Serikali hapo awali na kubaini madudu ya kutisha katika kampuni hizo zikiwemo za ufisadi na uhujumu uchumi kabla ya viongozi wake kupokonywa hati za kusafiria kutokana na mlolongo wa kashfa nzito.

          

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya