Monday, June 16, 2025
spot_img

DK. KUSILUKA ATEMBELEA JNHPP, ASEMA WATANZANIA WANATAKA UMEME

*Awaagiza wataalamu kukamilisha kazi kwa wakati, ujenzi wafikia zaidi ya 90%

ZUENA MSUYA

Pwani

KATIBU Mkuu Kiongozi, Dk. Moses Kusiluka, amewataka wataalamu wanaojenga bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) kuukamilisha ujenzi kwa wakati ili Watanzania wanufaike na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali yao.

Agizo hilo amelitoa jana alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa JNHPP mkoani Pwani, unaotarajiwa kuzalisha megawati 2115 za umeme.

Baada ya kutembelea eneo la mradi, Dk. Kusiluka alieleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya ujenzi na aliwaambia watalaamu wanaoutekeleza kuwa Watanzania wanasubiri ukamilike haraka kwa sababu wanataka umeme wa uhakika na pia kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali yao.

“Najua kazi kubwa imefanyika, nimeamua kuja kuona ili kuamini. Kwa ujumla kazi ni nzuri sana imefanyika, ujenzi umefika zaidi ya asilimia 90, Serikali imewekeza fedha nyingi hivyo napenda kuwaambia watu wote na Watanzania kwa jumla watarajie kupata umeme wa uhakika muda si mrefu baada ya mradi kukamilika.

“Napenda kumshukuru na kumpongeza Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza ujenzi wa mradi huu kwani alipoingia maradakani, ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 35 na sasa ni miaka miwili na nusu tangu mradi umefikia zaidi ya asilimia 90 na unatarajia kuzinduliwa mwakani,” alisema Dk. Kusiluka.

Aliwapongeza wafanyakazi wote waanaotekeleza mradi huo huku akitaja Wizara ya Nishati, Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) na wadau wengine kuwa ni fahari kubwa kuona wametekeleza ujenzi wa mradi mkubwa kama huo kwa kuhusishwa na kushirikishwa kwa kiasi kikubwa.


“Ni matumaini yetu kwamba mpaka sasa vijana na wataalamu wetu wamejifunza mambo mengi sana na mara tu baada ya mkandarasi kuondoka, tunaamini Watanzania watakuwa wamepata utaalamu na ujuzi mkubwa zaidi wa kuendesha kituo cha JNHPP na kutekeleza miradi mingine ya kuzalisha umeme kama huu,” alisema.

Dk. Kusiluka alisema timu ya wataalamu wanaotekeleza mradi huo ilianza vizuri na inapaswa kumaliza vizuri na kwa wakati na aliwataka watambue Serikali imewekeza fedha nyingi za Watanzania kwenye mradi huo.


Katika ziara hiyo, Dk Kusiluka aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Faraji Kasidi Mnyep, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande na viongozi wengine.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya