RIPOTA WA WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi na wataalamu wa mamlaka za Serikali za Mitaa kuweka nguvu zaidi katika kuwaendeleza vijana ili washiriki kikamilifu shughuli za kiuchumi na kuwapata ujuzi na mbinu za ujasiriamali.
Majaliwa alitoa agizo hilo Agosti 8, mwaka huu alipokuwa akifunga kongamano la vijana lililofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.
Alisema vijana wanapaswa kupatiwa mbinu na ujuzi wa ujasiriamali ili waweze kuchangamkia fursa zilizo mbele yao.
Aliagiza kila mkoa kuandaa mpango mahsusi wa kuhamasisha vijana kufanya shughuli zenye staha na kuwavutia vijana wengi kushiriki shughuli za kiuchumi.
Majaliwa alizitaka taasisi na mifuko ya uwezeshaji kwa vijana zitangaze fursa zilizopo na zitumie mbinu mbalimbali zikiwemo redio za kijamii kuwafikia walengwa.
“Kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki kuwapa taarifa, kuwaongoza na kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za kukuza mitaji yao.
“Halmashauri zihakikishe vijana walio tayari kujihusisha na shughuli za uwekezaji wanapata taarifa za fursa za mitaji. Nyote mlimsikia Mheshimiwa Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango akisisitiza kuhusu kutoa taarifa kwa walengwa,” alisema Majaliwa.
Aidha, Majaliwa aliitaka mikoa iandae utaratibu wa kutoa elimu mtambuka kwa vijana ili wapate stadi za maisha na kufanya maamuzi sahihi na kusisitiza na utunzaji wa mazingira na mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI, maadili, uzalendo, mapambano dhidi ya dawa za kulevya na rushwa kupewa kipaumbele.
Alieleza imani yake kwa vijana walioshiriki kongamano hilo kuwa wameiva na wako tayari kwa kazi hivyo watumie maarifa waliyoyapata kuchangamkia fursa zilizopo ndani na nje ya Mkoa wa Dodoma na zaidi kuwa wadadisi kubaini na kuchangamkia fursa hizo.
”Mmeshapata maarifa mengi kupitia kongamano hili, wakati umefika sasa mnakwenda kutumia maarifa hayo kwa vitendo. Mikoa nayo iandae utaratibu wa kutoa elimu kuhusu masuala muhimu na mahsusi ya mtambuka kwa vijana ili wapate stadi za maisha na kufanya maamuzi sahihi.
“Nitoe wito kwenu vijana kuitumia fursa hii muhimu na adhimu mliyoipata katika kongamano hili kuanzisha na kuendeleza miradi yenu na baadaye kuondoa tatizo la ajira na umaskini kwa nchi yetu. Muhimu ni kuthubutu, kuchukua hatua, kuanza kidogo na kukua,” alisema.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema kongamano hilo la siku mbili limeshirikisha vijana zaidi ya 3,000 kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dodoma limelenga kuwawezesha vijana kutambua fursa za kiuchumi zilizoko na kuzichangamkia