Thursday, June 12, 2025
spot_img

BANDARI, DP WORLD NA KISA CHA NYANI HAONI KUNDULE

MCHOKONOZI

CHARLES MULLINDA

KUNA ya vita ya manyani inayopiganwa sasa hapa nchini. Ni vita ya nyani kuchekana maumbile yao ya nyuma. Maumbile ya nyani hayatofautiani lakini hakuna nyani anayeweza kuona sehemu zake za nyuma isipokuwa za mwenzake. Nyani haoni kundule.

Siku zote vita siyo kitu kizuri na hasa inapopiganwa na watu wasiokuwa na utu. Watu wasiokuwa na utu hawana tofauti na nyani kwa sababu ni jambo la kawaida kwa nyani mtoto kupigana na baba nyani. Nyani mtoto akimzidi nguvu nyani mzazi haoni shida kumpiga hadi kumuua.

Mjadala kuhusu kusainiwa kwa mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara unaohusisha Bandari za Tanzania kukabidhiwa Kampuni ya DPW kuziendesha, umegeuka kuwa vita ya aibu katika taifa letu.

Wanaopigana vita hii, baadhi yao wameamua kuwapiga wazazi wao. Wanawapiga kipigo kibaya bila kujali kuwa ni wazazi wanaolea familia yenye watoto wengi.

Hawajali kuwa wazazi; yao ni heshima tu. Hata inapobidi kutofautiana nao, taji la heshima walilonalo kichwani linawalinda hivyo ni lazima kuwafikishia ujumbe wa kutofautiana nao kwa staha. Ajabu watoto hawa wamekosa heshima na adabu.

Wazazi hawa wanapigwa lakini hawana mtetezi. Ni wazazi wetu sote, wamejikunyata tu wakipigwa na sisi tukiwaangalia. Najiuliza, wapo wapi watoto wenye misuli ya haja kwenye mikononi yao ambayo ina uwezo wa kushika kalamu kujenga hoja za nguvu za kuwatetea wazazi wetu hawa?

Masikini wazazi wetu hawa wamebaki na watoto wa hivyo hivyo; Watoto wa wazazi wetu hawa wanaojitutumua kuwalinda tunaona uwezo wao ndiyo umeishia hapo. Wazazi wetu wanaumia. Inasikitisha sana. Hata hivyo hatuna budi kuwaacha wazazi wetu na waziwanda wao kwa sababu ndiyo hao walionao ubavuni lakini tusikubali kuona nyumba ya wazazi wetu ikichomwa moto.

Ukiwasikiliza, baadhi ya watu wanaotetea Serikali kusaini mkataba wa uwekezaji katika bandari zetu utagundua hawana sababu za msingi na wanaopinga nao hawana sababu za msingi. Kutoka kwao tunasikia kelele, kejeli, kebehi na ushabiki wa kipuuzi.

Na pengine inawezekana wana hoja lakini ujengaji wa hoja zao hauingii akili. Badala ya kujenga hoja wanaporomosha matusi, mipasho na kejeli. Wanashambuliana. Huu siyo mwelekeo mzuri.

Wachache wanaojenga hoja za msingi kwa pande zote mbili wamemezwa na kundi la nyani asiyeona kundule. Hoja zao zinapotelea hewani, hazijikiti zikakita kwa walengwa hivyo wamebaki njiapanda. Pengine hili nitalijadili kwa upana wake wakati muafaka, acha nirudi kwenye hoja ya nyani haoni kundule.

Wakili Rugemeleza Nshala na Profesa Anna Tibaijuka wakipitia nyaraka wakati Baraza la Maadili kwa Viongozi wa Umma lilipokuwa likimuhoji kuhusu mgao aliopokea wa fedha za Escrow.

Nimemsikiliza vizuri wakili, Dk. Rugemeleza Nshala akizungumzia suala la bandari na hata jana alipoutangazia umma kuwa maisha yake yapo hatarini. Madai haya ni mazito, Wakili Nshala ni Mtanzania, ni binadamu, haina shaka amekwaza watu wengi kwa matamshi yake ya hovyo lakini asitokee mtu wa kujipa uhakimu juu ya maisha yake. Watanzania ni watu wa amani, tupingane kwa hoja badala ya kutishiana maisha.

Haraka nakubaliana na Wakili Nshala kuwa anayo haki kama Mtanzania kutoa mawazo yake kuhusu jambo lolote lile lakini sikubali hata kidogo kuwa wakili huyu anayo haki ya kutumia lugha chafu, kukebehi na kuchochea hasira za wengine anapotoa mawazo yake.

Sikubaliani na Wakili Nshala katika ukosaji wake kuhusu ndoa ya TPA na DPW kumwita Rais wa Tanzania msaliti na mhaini. Sitaki wakili huyu awe na tamaa ya kumwelekeza Rais wa Tanzania kumpigia simu anayemuita Sheikh kumweleza kuwa Tanzania mambo si shwari tena.

Kumwita Rais wa Tanzania mhaini na msaliti; tena maneno hayo machafu yakitolewa na msomi wa kiwango wa PHD ni makosa makubwa, ni utovu wa nidhamu. Ni kauli ambayo haipaswi kutolewa na Mtanzania. Ni lazima tumkataze wakili huyu kumchezea Rais wa Tanzania.

Kwa wananchi; kumvika Rais uhaini na usaliti kwa taifa lake, kwa maneno laini tunaweza kusema ni kuwajengea picha kuwa nembo yao ya Taifa la Tanzania haipaswi kuwepo tena; na kwa Rais mwenyewe ni kumchokonoa, ni kumchokoza kwa makusudi, kumchafua, kumvunjia heshima na kumvisha kila aina ya ubaya.

Wanaomzunguka Rais, kwao ni kutafuta mishipa yao ya hasira na kuichoma sindano rungu. Wakili huyu ana ajenda gani hasa? Hivi angekuwa Julius Nyerere, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete au Dk. John Magufuli angethubutu kuwachezea hivi? Nashindwa kuota nikimsikiliza Wakili Nshala akimwita hayati Mkapa msaliti na mhaini au hayati Dk. Magufuli.

Tanzania hatujafika hatua ya kusema kwamba hakupo shwari, hivyo kwa Wakili Nshala kuonyesha tamaa ya kutaka Rais apige simu Dubai kutoa taarifa kuwa nchi anayoiongoza haiko shwari ni kuwachokoza Watanzania na Rais wao. Hapana, Wakili Nshala Watanzania hawapendi ugomvi, wanachukia kuchokozwa.

Tusipomkataza sasa Wakili Nshala anaweza kutufikisha mahali pabaya. Sitaki Wakili Nshala awaite masheikh mbumbumbu na watu ambao uelewa wao wa mambo ni zero. Hata kama masheikh walikosea lakini kosa lao halihalalishi yeye naye kufanya kosa la kuwadharau na kuwadhalilisha. Hiki anakichokifanya wakili huyu ni kuibua hasira dhidi ya masheikh hao. Ni kutafuta ugomvi.

Kuwatuhumu Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kuwa waliwatuma masheikh hao kusema waliyoyasema ni kuwakosoe adabu viongozi hao kwa sababu nina hakika, uhakika wa tuhuma hizo, Nshala hana.

Ninatamani Wakili Nshala kwa elimu yake, hadhi yake, akiwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika awe mfano wa kuigwa kuheshimu mamlaka na kuchagua maneno ya kuzungumza.

Wakili Nshala kumuona Rais mpaka aliyemwita wa mwisho ni wezi wa kura ni kuwatukana Watanzania waliopiga kura kumchagua. Nasisitiza, waliopiga kura kumchagua.

Profesa Anna Tibaijuka akiwa mbele ya Kamati ya Maadili kwa Viongozi wa Umma akisikiliza tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Kwa Wakili Nshala kujigamba kwenye mitandao ya kijamii kuzipiga kavu kavu ni kujidhalilisha, ni kuonyesha alivyo na tabia ya ugomvi. Kwa mtu wa hadhi ya wakili, kujisifia ugomvi ni kijifedhehesha. Sitaki Wakili Nshala atafute ugomvi makusudi. Sitaki kuona wakili anayefikiria kuingia msituni, huo ni uasi. Watanzania hatuko hivyo, mambo ya msituni ni ya magaidi, Nshala ni mtu mzuri tu asijipe sifa ya ugaidi.

Lakini ukimtizama kwa macho matatu Wakili Nshala anaposhambulia vikali utiaji saini mkataba unaobishaniwa sasa unamuona nyani asiyeliona kundule.

Macho matatu yanapomwangalia Wakili Nshala akikosoa vikali mkataba ule, yanamuona akimtetea kwa nguvu zake zote Profesa Anna Tibaijuka, Mbunge wa zamani wa Muleba Kusini aliposimama mbele ya Sekretarieti ya Maadili na kusomewa mashtaka ya kutumia wadhifa wake wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushawishi, kuomba na kupokea fedha Shilingi bilioni 1.617 kutoka kwa James Rugemalira.

Macho yanamuona Wakili Nshala akisimama haraka baada ya kumaliza kusomwa kwa hati ya mashtaka dhidi ya Profesa Tibaijuka na kusema wanayakataa mashtaka yote. Kanusho hilo lilimlazimu Jaji Hamis Msumi kumuongoza kwa lugha laini na ya upendo kuwa; “Hii siyo mahakama ya kisheria, taratibu zetu siyo za kimahakama, hivyo ni vizuri kuyafikiria hayo.”

Anaonekana vizuri Wakili Nshala akimpambania Profesa Tibaijuka licha ya kuelezwa kuwa kwa Profesa Tibaijuka kupokea kiasi kikubwa cha fedha kama hicho kwa wadhifa aliokuwa nao wa uwaziri ni ukiukwaji wa sheria za viongozi wa umma; na hata Profesa Tibaijuka alipoiambia Sekretariati hiyo kuwa alichota Shilingi milioni 10 za mboga kwenye fedha alizopewa na Rugemalira, hakumuacha, ‘alikufa naye.’

Wakili Nshala alipokuwa akimtetea Profesa Tibaijuka kupokea fedha za skandali ya Escrow, hakutukanwa na mtu licha ya kuwepo hisia mbaya miongoni mwa jamii dhidi ya aliyekuwa akimtetea.

Kwake Wakili Nshala ilikuwa haki yake kumtetea Profesa Tibaijuka licha ya uchafu uliokuwa ukimuandama lakini anaona kosa kwa wenye tabia kama zake wanaotetea sasa mkataba wa bandari. Nyani haoni kundule.

Wakili Nshala haiishi kwa wenye tabia kama zake za lugha ya matusi, anakwenda mbali zaidi, anamtukana Rais huku kivuli cha ‘dhambi’ ya milioni 10 za manunuzi ya mboga ya Profesa Tibaijuka aliyoyatetea kwenye Sekretarieti ya Maadili kikingalipo.

Sasa anawaponza wenzake kwani uhusiano wa Profesa Tibaijuka na Nazir Karamagi, mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya TICTS iliyonyang’wanya ulaji bandarini ni wa pete na kidole hivyo picha ya wazi inayokuja ni kwamba anatumika kwa maslahi ya TICTS na kwa sababu anajua kucheza na vifungu vya sheria, anamvua mzazi kilembe kichwani kwa lugha za matusi ili kumkoroga.

Itoshe tu kusema kuwa Wakili Nshala ajitazame upya. Autumie usomi wake wa sheria kuchambua vifungu vya mkataba kueleza udhaifu uliomo badala ya kutukana Rais na kuchokoza Watanzania wengine.

Inawezekana wanaomuwasha sasa Wakili Nshala kiasi cha kututangazia kuwa maisha yake yako hatarini kwa sababu anawashwa sana ni chawa ambao kula yao inategemea uchawa wao. Anaowatukana wala hawana habari naye.

Chawa ni kawaida yao kunyonya damu na uchafu, ndiyo maisha yao. Wakili Nshala asiruhusu chawa kunyonya damu na uchafu wake hadi adhoofike. Atakuwa anajiangamiza mwenyewe.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya