RIPOTA PANORAMA
ZEGE inayotumika kujengea barabara zitakazotumiwa na Mabasi Yaendeyo Haraka, kutoka Mbagala wilayani Temeke hadi katikati ya Jiji la Dar es Salaam haina kiwango kinachotakiwa kujengea barabara hizo.
Hayo yamo kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka 2021/22 inayofichua hatari ya zege hiyo kuwa chini ya kiwango.
CAG anasema hatari ya zege hiyo kukosa kiwango kinachotakiwa kujengea barabara hizo, ni barabara kupata nyufa za usinyao na joto na pia upungufu wa uwezo wa tabaka la juu la lami kwenye barabara.
Kwa mujibu wa CAG, mkandarasi wa mradi huo ambaye ni Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited, na mhandisi mshauri wa mradi ni dhaifu.
CAG anasema miundo ya zege iliyopimwa kwenye ukaguzi wake haikidhi kiwango kinachohitajika cha uwezo wa zege na anatoa mfano wa zege iliyotumika kujenga ngazi za upande wa kulia wa daraja la juu la waenda kwa miguu la Mbagala, na vizuizi vya ajali upande wa kushoto na kulia katika makutano ya barabara ya juu ya Kilwa na Mandela kuwa haina kiwango kinachohitajika.

Mabasi Yaendayo Haraka yakipita katika barabara iliyojengwa kwa ajili ya magari hayo
“Niligundua kuwa baadhi ya miundo ya zege iliyopimwa haikutimiza kiwango kinachohitajika cha uwezo wa zege. Kwa mfano, uwezo wa ngazi upande wa kulia wa daraja la juu la waenda kwa miguu Mbagala, ilikuwa 22 N/mm2 kati ya 40N/mm2.
“Na uwezo wa vizuizi vya ajali upande wa kushoto na kulia vya makutano ya barabara ya juu ya Kilwa na Mandela vilikuwa 28 na 30 mtawalia ukilinganisha na 40 N/mm2 inayohitajika,” anasema.
CAG anasema zege hiyo kutowiana na kiwango kinachohitajika, kulidhibitisha udhaifu katika mfumo wa uhakiki na udhibiti wa ubora wa mhandisi mshauri na mkandarasi mtawalia.
Anasema miundombinu iliyopimwa ambayo haijatimiza uwezo wa kiwango kinachohitajika iko hatarini kupata nyufa za usinyao na joto na upungufu wa uwezo wa tabaka la juu.
CAG anaigeukia Menejimenti ya Wakala wa Barabara (TANROADS) akipendekeza kwayo kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo ya mhandisi mshauri kwa mkandarasi ili uthibiti wa ubora na viwango vya uhakiki wa ubora wa unene wa tabaka ya lami na unene wa lami nene uzingatiwe na pia mhandisi mshauri kumsimamia mkandarasi kulingana na masharti ya mkataba.