Tuesday, September 9, 2025
spot_img

KASHFA YA BIL. 123 ZA VISHIKWAMBI VYA SENSA YAMNYAMAZISHA PROF. MKENDA

RIPOTA PANORAMA

KASHFA ya manunuzi ya vishikwambi 300,000 vilivyonunuliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi, kwa gharama ya Shilingi bilioni 123.78, imemnyamazisha Waziri, Profesa Adolf Mkenda.

Kashfa hiyo inahusu kukiukwa kwa taratibu za zabuni, kubadilisha vigezo vya ubora wa vishikwambi, kufichwa kwa bei ya sokoni na kutozingatiwa kwa muda wa zabuni.

Katika mlolongo huo wa kashfa, imo pia ya kutofautiana kwa taarifa za zabuni, kutokuwepo kwa hati ya dhamana ya vishikwambi na pia, wizara kuvitoa vishikwambi hivyo bila nyaraka sahihi huku ikifunika tarehe ya makabidhiano.

Kashfa hii imo kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikari (CAG), kwa mwaka 2021/2022 ambayo imebainisha dosari katika ununuzi wa vishikwambi 300,000 uliofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Tanzania PANORAMA Blog imemfikia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na kumweleza kuwa inayo maswali machache inayoomba ayapokee na kuyatolea majibu au ufafanuzi; naye kwa haraka na bila kusita aliitikia kwa kimombo “OK”

Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza, Tanzania PANORAMA Blog ilipompatia maswali hayo Profesa Mkenda, aliyapokea kisha akanyamaza kimya kabisa. Hata alipotafutwa na kukumbushwa tena na tena kujibu, hakujibu wala kupokea simu.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, Machi, 2022 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilipewa jukumu la kununua vishikwambi 300,000 kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti, 2022 kupitia zabuni nambari ME.024/2021/22/HQ/G/34.

“Wizara ilianzisha mchakato wa zabuni ikialika wazabuni 14 kuishiriki. Zabuni hiyo iligawanywa katika sehemu sita, kila moja ikiwa na vishikwambi 50,000. Wizara ilisaini mkataba na wazabuni watatu kuleta vishikwambi 300,000 vyenye thamani ya Shilingi bilioni 123.78, bei ya awali ikiwa Shilingi bilioni 104 na kodi ya ongezeko la thamani Shilingi bilioni 18,992,” anasema CAG katika ripoti yake.

Akiainisha dosari alizozibaini kwenye ukaguzi wake, anasema muda wa kuwasilisha vishikwambi ulikuwa siku 40 baada ya kusainiwa kwa mkataba, hata hivyo wazabuni waliochaguliwa walipitishwa bila ushindani.

CAG anasema wajumbe wa bodi ya zabuni ambao kupendekeza wazabuni siyo kazi yao, walijipa kazi hiyo na kupendekeza wazabuni wanne kati 14, na wawili kati ya hao ndiyo walioshinda zabuni hiyo.

Anaendelea kusema CAG kuwa, wajumbe hao wa bodi ya zabuni wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia walibadilisha vigezo vya ubora wa vishikwambi kwa kuondoa vifaa vya kutunzia umeme (power bank) bila kuwasiliana na idara tumizi.    

“Idara ya manunuzi ya wizara ilishindwa kuainisha bei za soko la vishikwambi, hivyo huenda vilinunuliwa kwa bei ya juu ikilinganishwa na bei ya soko. Wazabuni walipewa siku mbili tu za kujibu nyaraka za zabuni badala ya 14 huku wazabuni 10 kati ya 14 wakiwasilisha kwa wakati,” anasema CAG.

Akiendelea kuainisha dosari hizo, CAG anasema alibaini kutofautiana kwa taarifa kati ya bei ya zabuni zilizojumuishwa na VAT na nyingine hazikuwa na taarifa za VAT; “Tofauti zilizopatikana kati ya bei za zabuni zinazojumuishwa na VAT katika taarifa ya ufunguzi wa zabuni na ripoti ya tathmini ambapo zabuni hazikueleza hali ya VAT isipokuwa zabuni moja.

“Idara tumizi haikuhusika katika kamati na wajumbe waliteuliwa bila mapendekezo ya idara tumizi. Hakuna ushahidi wa hati ya udhamini uliotolewa kwa vishikwambi vilivyonunuliwa kinyume na matakwa ya mkataba ulioainisha makubaliano ya hati ya miaka miwili,” anasema CAG na kuongeza kuwa:

“Wizara ilitoa vishikwambi 209,480 kwa ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), bila nyaraka sahihi au tarehe ya wazi ya makabidhiano na ripoti ya hali baada ya zoezi la sensa.”

Anasema hayo yanayoonyesha mchakato wa ununuzi uliathiriwa na kwamba thamani bora ya fedha inaweza kuwa haijafikiwa.

     

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya