RIPOTA PANORAMA
WANAFUNZI 22,039, waliojiunga kidato cha kwanza mwaka 2018 kwenye Shule za Sekondari za Mamlaka za Serikali za Mitaa 19, walikatisha masomo kwa sababu ya kupata mimba, umbali mrefu kutoka kwenye makazi yao hadi shuleni, malezi ya familia na sababu binafsi.
Sambamba na hilo, wanafunzi 238,141 wa shule za umma waliofanya mitihani ya Taifa ya kidato cha nne, mwaka wa masomo 2021 katika mamlaka 96 za Serikali za Mitaa, 12,094 kati yao ambao ni sawa na asilimia 12 kati ya waliofanya mitihani hiyo, walipata sifuri.
Wanafunzi wengine 129,094, ambao ni sawa na asilimia 54 ya waliofanya mitihani ya Taifa ya kidato cha nne, mwaka wa masomo 2021, walipata daraja la nne hivyo kufanya jumla ya wanafunzi waliofeli kuwa 155,185 ambao ni sawa na asilimia 66 ya waliofanya mitihani.
Haya yamo kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya mwaka 2021/22 ambayo ukaguzi wake ulihusisha ufanisi wa kiutendaji katika sekta ya elimu.
Ripoti hiyo inaonyesha wanafunzi 19,945 kati ya wanafunzi 78,786 waliosajiliwa kujiunga na darasa la kwanza kati ya mwaka 2015 na 2021 katika halmashauri 11, hawakuhitimu darasa la saba.
“Mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa 2021/22 hadi 2025/26 unaeleza lengo la uandikishaji kwa ngazi ya elimu ya msingi kuwa asilimia 100 na kwa elimu ya sekondari (kidato cha I-IV) umepangwa kuwa asilimia 48.
“Uwekezaji unaondelea wa Serikali katika sekta ya elimu umesaidia kuongeza uandikishaji wa wanafunzi kwa ajili ya elimu ya msingi na kulichangiwa zaidi na kutolewa kwa elimu bila malipo kutoka msingi hadi kidato cha nne.
“Katika halmashauri 11, nilibaini kuwa kati ya 2015 hadi 2021, wanafunzi 19,945 (25%) waliosajiliwa 2015 hawakuhitimu darasa la saba. Pia nilibaini katika mamlaka 19 za Serikali za Mitaa, wanafunzi 22,019 sawa na asilimia 28 kati ya 82,236 waliojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 hawakufanikiwa kufanya mitihani na kupata cheti cha kuhitimu kidato cha nne,” inasomeka ripoti.
Kwa mujibu wa tathmini yake CAG kuhusu matokeo ya mitihani ya elimu ya sekondari katika shule za umma, anaeleza kubaini kuwa kati ya wanafunzi 238,141 waliofanya mitihani ya Taifa ya kidato cha nne, mwaka wa masomo 2021 katika mamlaka 96 za Serikali za mitaa, asilimia 12 kati ya hao walipata sifuri.
Ripoti inazidi kuonyesha kuwa, asilimia 54 ya wanafunzi waliofanya mitihani hiyo mwaka wa masomo 2021, walipata daraja la nne hivyo kufanya jumla ya wanafunzi waliofeli kwa mwaka huo wa masomo kuwa asilimia 66.
“Hali hii inamaanisha kwamba mazingira magumu ya kujifunzia katika shule za umma ambayo ni magumu kumuwezesha mwanafunzi na mwalimu kufikia matokeo mazuri ni ya kiwango cha juu.
“Kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi waliofeli katika shule za sekondari kunaathiri lengo la Serikali kupitia elimu bure la kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora,” inasomeka ripoti.
CAG anapendekeza Serikali kuboreshe mazingira ya shule za sekondari za umma pamoja na hali ya kazi za walimu kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kulipa madai ya walimu kwa wakati, sambamba na kuhakikisha shule za umma zina walimu wa kutosha, wenye sifa na uwezo.