Friday, May 16, 2025
spot_img

BARABARA ZA DART ZAJENGWA CHINI YA VIWANGO

RIPOTA PANORAMA

MRADI wa ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka (DART), kutoka Mbagala wilayani Temeke hadi katikati ya Jiji la Dar es Salaam, eneo la Kariakoo na eneo la Kivukoni kuelekea Zanzibar, unatekelezwa chini ya ubora wa viwango vinavyohitajika.

Utekelezaji duni wa mradi huo unaziweka barabara zinazojengwa na mkandarasi; Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 159.32, ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 285 kwenye hatari ya kuharibika haraka na pia zikiwa na uduni wa kubeba mzigo wa muundo wa barabara zenyewe.

Haya yamefichuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti ya ukaguzi iliyoikabidhi kwa Rais Samia Samia Suluhu Hassan, mwezi Machi, mwaka huu ikiwa inaeleza kinaga ubaga udhaifu wa mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Sinohydro Corporatin Limited na Wakala wa Barabara (TANROAD) kushindwa kuhakikisha mkandarasi huyo anasimamiwa vizuri na mhandisi mshauri.

CAG ameibua ‘madudu’ haya huku Rais Samia Suluhu Hassan; zaidi ya mara moja, akiwa amekwishatoa maelekezo kwa mamlaka za usimamizi wa miradi mikubwa, inayotekelezwa kwa gharama kubwa na Serikali kuisimamia vizuri huku akiwataka wakandarasi kuitekeleza kwa ubora wa viwango vinavyotakiwa.

Kwa mujibu wa CAG, ujenzi wa barabara hizo unahitaji unene wa milimita 200 ya lami nene kwa njia za magari yaliyochanganyika lakini badala yake zimejengwa chini ya unene wa milimita 185 za tabaka la lami nene.

“Michoro ya ujenzi wa kazi za barabara inahitaji unene wa milimita 200 ya lami nene “dense bitumen macadam” (DBM) kwa njia za magari yaliyochanganyika kwenye Barabara ya Kilwa.

“Jedwali la mwongozo wa viwango vya barabara linabainisha kiwango cha ukomo cha upungufu wa milimita 15, yaani isiwe chini ya unene wa milimita 185 kwa daraja la unene wa lami na unene wa safu/tabaka linahitaji kuhakikiwa kila baada ya mita 25 au zaidi.

“Hata hivyo, tathmini yangu ilibaini kwamba asilimia 12 ya alama za data (data points) za barabara nilizokagua, sawa na alama 318 kati ya 2,631 zilikuwa na kiwango cha chini cha unene wa milimita 185 za tabaka la lami nene (DBM),” anasema CAG kwenye ripoti na anaendelea kueleza athari za kukiukwa kwa unene wa tabaka la lami unaohitaji.

“Alama hizi zinaweza kusababisha sehemu dhaifu katika mfumo wa lami. Kasi ya uharibifu wa mfumo wa barabara ni kubwa sana wakati safu ya lami ya DBM ni nyembembe.

“Hata hivyo, kadri unene wa safu ya lami unavyoongezeka, ndivyo uwezo wa kubeba mzigo wa muundo wa barabara unavyoongezeka, ambayo inamaanisha kuwa barabara itaharibika pole pole na ubora wa kuendesha utaendelea kuwa juu,” anasema CAG katika ripoti.

Akiendelea kuainisha udhaifu aliougundua kwenye mradi huo, CAG anasema ukosefu wa unene wa DBM nje ya kipimo kilichoruhusiwa unaonyesha udhaifu katika mfumo wa udhibiti wa ubora wa mkandarasi na mfumo wa hakikisho wa ubora wa mshauri.

Anasema, inaonyesha pia kuwa TANROADS ilishindwa kuhakikisha mkandarasi anasimamiwa vizuri na mhandisi mshauri ili kuthibitisha unene uliowekwa wa lami nene kama ulikidhi vigezo vilivyowekwa.

Katika barabara hiyo hiyo, CAG anaendelea kueleza kuwa vipimo vya mradi wa barabara ya mchanganyiko wa magari katika Barabara ya Kilwa, ilihitaji unene wa tabaka la lami mnato (Binder cource) ya milimita 80, lakini iliyowekwa inaanzia milimita 36 hadi milimita 187, ambayo kwa wastani ni milimita 78.

“Vipimo  vya mradi wa barabara ya mchanganyiko wa magari katika Barabara ya Kilwa ilihitaji unene wa tabaka la lami mnato (Binder course) ya milimita 80, lakini hali halisi ilibaini kuwa unene ulianzia mm 36 hadi mm 187, ikiwa ni unene wa wastani wa milimita 78.

“Takribani asilimia 19 kati ya alama 2,681 zilizochunguzwa, karibu alama 503 au asilimia 19 kati ya alama 2,631 zilizochunguzwa zilikuwa nyembembe kuliko kizingiti cha unene wa chini ya milimita 70. Alama hizi zinaweza kusababisha sehemu dhaifu katika mfumo wa lami …. Kwa hiyo, kiwango cha huduma ya muundo wa lami kitategemea ubora wa lami. Unene wa safu ya lami una athari kubwa kwenye muundo wa uharibifu wa utendaji wa lami,” anasema CAG.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere

Aidha, CAG anasema kuwa, kwa mujibu wa viwango vya kawaida kwa kazi za barabara, unene wa tabaka la lami unapaswa kuchunguzwa angalau kila mita 25 kando ya mstari wa kati, mbadala kushoto na kulia ya barabara lakini jambo hilo halifanyika kikamilifu.

Anasema ukosefu wa unene wa safu la ‘binder course’ katikati ya barabara zilizotajwa, unaashiria udhaifu katika mfumo wa udhibiti wa ubora wa mkadarasi na mfumo wa uhakikisho wa ubora wa mshauri wa mradi.

USIKOSE KUPERUZI TANZANIA PANORAMA BLOG, KESHO USOME ‘MADUDU’ ZAIDI YA MKANDARASI WA BARABARA ZA DART, YALIYOANIKWA NA CAG.  

      

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya