RIPOTA MAALUMU
Idara ya Habari (MAELEZO)
Musanze, Rwanda
MKUU wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda amevitaka vikosi vya ulinzi na usalama vinavyoshiriki kozi ya ushirikiano imara 2023, kwa majeshi ya Nchi za Afrika ya Mashariki kuliwakilisha vema Taifa ili kujenga ushirikiano mzuri na nchi jirani.
Akizungumza jana mara baada ya ufunguzi wa kozi hiyo katika Mji wa Musanze, Rwanda Jenerali Mkunda alisema kozi hiyo iwe chachu ya kujifunza namna ya kutatua changamoto za kiulinzi na usalama katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema wananchi wa mataifa yanayounda Jumauiya ya Afrika Mashariki wanayategemea zaidi majeshi yao kuwapatia msaada wa ulinzi na uokozi pindi majanga yanapotokea.
“Unajua hakuna kitu kikubwa ambacho huwa kinarudisha na kujenga imani ya wananchi kwa majeshi yao kama kupewa msaada wa kijamii pindi wapatapo majanga. Imani yao kubwa hubaki kwa wanajeshi ambao ndio huwa wa kwanza kutoa msaada,” alisema Jenerali Mkunda.
Jenerali Mkunda pia amevitaka vikosi hivyo kudumisha udugu na ushirikiano wa majeshi kutoka Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
“Nchi yetu ya Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikisifika kwa kuwa marafiki wa kweli katika Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na dunia nzima, hivyo hakikisheni mnaendelea kuwa mfano wa kuigwa,” alisisitiza Jenerali Mkunda.
Akizungumzia umuhimu wa ushirikishwaji wa kozi hiyo kwa taasisi na mamlaka za kiraia, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema huu ni wakati muafaka wa kufanya kazi pamoja kwani pindi majanga yanapotokea, mamlaka mbalimbali zinahusika kutoa utaalamu wa kukabiliana na majanga hayo.
“Tupo tayari kufanyakazi na Majeshi ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha kuwa tunatekeleza majukumu yetu ya kihabari kusaidia kufanikisha majukumu ya kulinda amani na kurudisha imani ya wananchi pale majanga yanapotokea”,alisema Msigwa.
Kozi hiyo ya wiki mbili imefunguliwa rasmi jana, Jumapili na Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, Juvenal Marizamunda ambaye alimkabidhi bendera ya kuashiria kuanza kwa kozi, mkuu wa zoezi hilo Dk. Alice Urusaro Uwagaga Karekezi ambaye naye alikabidhi bendera hiyo kwa Mkuu wa Majeshi ya Kikanda (REMIKA), Brigedia Jenerali Julius Gambosi.
Kozi hiyo inalenga kuvijengea vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za kiraia uwezo wa kukabiliana na ugaidi, uharamia, menejimenti ya majanga pamoja na ulinzi wa amani katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Washiriki wa kozi hiyo ni pamoja na majeshi ya ulinzi, polisi, magereza, uhamiaji, zimamoto na kituo cha Taifa cha kukabiliana na mapambano dhidi ya ugaidi.
Aidha, taasisi za kiraia zilizoshirikishwa ni pamoja na zilizo chini ya sekta za habari, haki za binadamu, usawa wa kijinsia pamoja na diplomasia na ushirikiano wa kimataifa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.