RIPOTA PANORAMA
SARAFU ya Tanzania inatarajiwa kupanda thamani baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuanza kununua na kuhifadhi dhahabu inayozalishwa hapa nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba alipokuwa akiwasilisha Bajeti ya Serikali, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24, bungeni jijini Dodoma, Juni 15, mwaka huu.
Dk. Nchemba alisema, tayari Serikali imekwishakamilisha taratibu za kununua dhahabu kupitia BoT kwa ajili ya kuanzisha akiba ya dhahabu ya Taifa.
“Hatua hii itawapatia wachimbaji bei nzuri zaidi na kuimarisha sarafu yetu,” alisema Dk. Nchemba.
Aidha, Dk. Nchemba alisema Serikali inaendelea kugharamia uanzishwaji wa vituo vya madini ili kuongeza thamani na kudhibiti utoroshaji wa madini.
“Jumla ya vituo vipya 40 vimefunguliwa na Serikali ya Awamu ya Sita na hivyo kufanya vituo vya madini kufikia 93,” alisema.
Dk. Nchemba alisema, Serikali inaendelea kujenga vituo cha umahiri katika shughuli za madini vilivyoko Songea, Mpanda na Chunya na imenunua madini ya Tanzanite yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.2.

Alisema tayari Serikali imekwishanunua mitambo mitano ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini na pia imenunua mitambo miwili ya kuzalisha mkaa kwa kutumia makaa ya mawe.
“Katika mwaka wa fedha ujao, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya madini ili iweze kuchangia zaidi kwenye uchumi wa nchi yetu. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itaongeza kasi ya kufanya tafiti za madini ya kimkakati na madini mengine.
“Aidha, Serikali itaanzisha minada ya madini nchini ili kuwezesha wachimbaji wa madini ya vito ikiwemo Tanzanite kuyafikia masoko ya kimataifa yenye bei halisi na kuvutia uongezaji thamani madini.
“Vilevile, hatua hiyo itasaidia kutangaza uwepo wa madini hayo hapa nchini na kuhamasisha uongezaji thamani madini katika mnyororo mzima wa uongezaji thamani,” alisema Dk. Nchemba.
Waziri huyo pia alisema, tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa viwanda vya kusafisha dhahabu na inaendelea kuweka vivutio kwa viwanda hivyo ili viweze kupata malighafi za kutosha.
Alisema, Serikali imepunguza mrahaba wa madini yanayouzwa kwenye viwanda vya kusafisha dhahabu kutoka asilimia sita hadi nne na inaendelea kuchambua sera, sheria na taratibu za kiutawala na za kikodi ili kuwezesha dhahabu inayozalishwa hapa nchini isafishwe kabla ya kuuzwa nje.