Monday, December 23, 2024
spot_img

CAG – WAFANYAKAZI WAGENI HARAMU MRADI WA DART TISHIO KWA USALAMA WA NCHI

RIPOTA PANORAMA

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amesema kuwepo kwa wakazi na wafanyakazi wa kigeni haramu wa Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited, kunatishia usalama wa nchi na kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

Pia amesema, kampuni hiyo imeajiri wataalamu, wakiwemo mameneja na wahandisi ambao wanafanya kazi hapa nchini bila kusajiliwa na bodi za kitaalamu, hivyo haijulikani kama wana ujuzi, maarifa na uzoefu unaohitajika kwenye kutekeleza majukumu ya ujenzi kwa ufanisi.

CAG ameyasema hayo kwenye ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2021/22, iliyohusu ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), unaotekelezwa na Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited, katika Jiji la Dar es Salaam.

Katika ripoti hiyo, CAG ameeleza udhaifu na upungufu mwingine uliobainika kwenye mradi huo kuwa ni udhibiti usioridhisha wa muda wa kukamilisha mradi, kuchelewa kuhuisha dhamana ya malipo ya awali, ujenzi usiokithi ubora na viwango vilivyohitajika na utunzaji mbaya wa vifaa vya ujenzi, kinyume na viwango vya mkataba wa vipimo maalumu.

Ametaja udhaifu na upungufu mwingine kwenye mradi huo kuwa ni uduni wa miundo ya zege, ongezeko la gharama za ushauri la Shilingi bilioni 7.67 kutokana na mabadiliko ya usanifu na kutochukuliwa hatua za kupunguza athari za kimazingira kwa ukamilifu.

Akizungumzia kuwepo kwa wafanyakazi wa kigeni wa mkandarasi, Sinohydro Cotporation Limited ambao hawana vibali vya kazi, CAG anasema kuwa maafisa sita kati ya 11 waliochaguliwa kama sampuli wakati wa ukaguzi wake, walikuwa wanafanya kazi bila kuwa na vibali vya kazi, kinyume na kanuni za ajira.

CAG anataja nyadhifa za wafanyakazi hao wa kigeni haramu, wanaofanya kazi bila kuwa na vibali vya kazi kuwa ni meneja udhibiti ubora ambaye pia ni mhandisi mkuu, mhandisi wa barabara, mhandisi majenzi na madaraja, meneja wa karakana, mhandisi wa umeme na mtaalamu wa upimaji ardhi.

“Kifungu cha 9 (2) (a) cha kanuni za ajira za wasio raia ya mwaka 2015, kinazuia kuajiri mtu ambaye si raia mpaka awe anamiliki kibali halali cha kazi ambayo inatambulika.

“Wakati wa mapitio yangu ya nyaraka za maafisa wa ngazi ya juu wa mkandarasi (Sinohydro Corporation Limited) kuhusiana na Lot 1, nilibaini kwamba maafisa sita kati ya 11 waliochaguliwa kama sampuli, walikuwa wanafanya kazi bila vibali vya kazi kinyume na kanuni za ajira.

“Kuwepo kwa wakazi na wafanyakazi wa kigeni haramu kunatishia usalama wa nchi na kunasababisha upotevu wa mapato ya Serikali ambapo kwa mkandarasi huyu, imefikia kiasi cha Dola za Marekani 6,000, sawa na Shilingi 13,800,000, ikizingatiwa kuwa ada ya vibali vya kazi ni kiasi cha Dola za Marekani 1,000 kwa miaka miwili,” anasema CAG.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.

Kuhusu wataalamu wa kigeni wa kampuni hiyo wanaofanya kazi pasipo kusajiliwa na bodi za kitaalamu za ndani, CAG anasema kati ya maafisa 10 waliochukuliwa sampuli, wanane kati yao, ambao ni sawa na asilimia 80 ya sampuli, hawajasajiliwa na bodi za ndani za kitaalamu.

Anataja nyadhfa za wafanyakazi wa kigeni walioajiriwa bila usajili wa bodi za ndani za kitaalamu kuwa ni meneja mikataba, mhandisi wa barabara, mhandisi majenzi na madaraja, mhandisi wa udongo na vifaa, meneja wa karakana, mhandisi wa umeme, mtaalamu wa upimaji ardhi na meneja wa mazingira ya jamii.

“Kifungu cha 6.12 cha masharti ya jumla ya mkataba kinahitaji kampuni kusajiliwa na bodi za ndani kama Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, Bodi ya Usajili wa Wahandisi na bodi nyingine za kitaalamu.

“Nilifanya ukaguzi kwa kuchukua sampuli ya maafisa 10 wa ngazi ya juu wa mkandarasi kutoka katika kipande cha kwanza (Lot 1) na kubaini kwamba maafisa wanane, sawa na 80% ya sampuli hawajasajiliwa na bodi za kitaalamu za ndani,” anasema CAG.

Aidha, CAG anasema kuwa, hayo yanatokana na udhaifu wa ufuatiliaji na usimamizi wa mradi na kwamba wafanyakazi hao kutokuwa na ithibati kutoka bodi za kitaalamu za ndani kunasababisha ugumu wa kujiridhisha kama wana sifa zinazohitajika kwenye utekelezaji wa majukumu ya mradi.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya