Monday, December 23, 2024
spot_img

WANAOISHI CHINI YA MSTARI WA UMASIKINI ULIOKITHIRI, WAKILA ELFU 33 KWA MWEZI WAPUNGUA

RIPOTA PANORAMA

ASILIMIA 8 ya Watanzania wanaishi chini ya umasikini uliokithiri, wakitumia chini ya Shilingi 33,748 kwa mwezi kwa mahitaji ya chakula cha mtu mzima.

Kwa upande wa Watanzania wanaoishi chini ya kiwango cha umasikini wa mahitaji ya  msingi, wanaotumia chini ya Shilingi 49,320 kupata mahitaji yao, wapo asilimia 24.4

Takwimu hizi za hali ya umasikini, zimetolewa bungeni, jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, Juni 15, 2023 alipokuwa akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24.

Alisema, kiwango cha umasikini wa chakula uliokithiri kwa Watanzania, kimepungua kutoka asilimia 9,7 mwaka 2011/12 hadi kufikia asilimia nane mwaka 2017/18, huku Watanzania wanaoshi chini ya kiwango cha umasikini wa mahitaji ya msingi nao wamepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 26.4 mwaka 2017/18.

“Hali ya umasikini ambapo pamoja na utajiri tulionao na hatua kubwa iliyopigwa, nchi yetu bado ina wananchi masikini. Kiwango cha umaskkini cha mahitaji ya msingi kitaifa kinapimwa kwa kuangalia wanakaya wanaoishi kwa kutumia chini ya Shilingi 49,320 kwa mwezi kwa mtu mzima kwa ajili ya kupata mahitaji ya msingi.

“Vile vile, kiwango cha umasikini uliokithiri (umasikini wa chakula) unapimwa kwa kuangalia wanakaya wanaoishi kwa kutumia chini ya Shilingi 33,748 kwa mwezi kwa mtu mzima, hivyo kushindwa kumudu kupata chakula chenye kalori 2,200 zinazotakiwa kwa mtu mzima kwa siku.

“Utafiti wa mapato na matumizi ya kaya wa mwaka 2017/18, ulionyesha kuwa asilimia 26.4 ya Watanzania wanaishi chini ya mstari wa umasikini wa mahitaji ya msingi, hali hii imepungua kutoka asilimia 28.2 kwa mwaka 2012.

“Tanzania imefanikiwa kupunguza kiwango cha umasikini uliokithiri, kutoka asilimi 9.7 kwa mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka 2017/18. Hata hivyo kiwango cha umasikini kimeendelea kupungua lakini siyo kwa kasi ya kuridhisha hivyo bado kuna Watanzania masikini,” alisema Dk. Nchemba.   

Alisema nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), zinatekeleza mipango mbalimbali inayolenga kupunguza umasikini wa mahitaji ya msingi na umasikini uliokithiri na kwa upande wa Afrika Mashariki, viwango vya juu vya umasikini vinatofautiana miongoni mwa nchi wanachama.

Dk. Nchemba alisema, Tanzania imepiga hatua kubwa ya kupambana na umasikini ingawa bado kasi ya kupungua kwa umasikini ni ndogo.

    

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya