Thursday, July 17, 2025
spot_img

2023/24 – BAJETI YA KUJITEGEMEA KWA ASILIMIA 70

RIPOTA PANORAMA

TANZANIA itajitegemea kwa asilimia 70 katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2023/24 inayotarajiwa kuwa Shilingi trilioni 44.39.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba ametangaza hatua hiyo kubwa kwa Taifa leo, bungeni jijini Dodoma alipowasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Akisoma bajeti hiyo, Dk. Nchemba amesema Shilingi trilioni 31.38 ambazo ni sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote kwa mwaka wa fedha 2023/24, zitatokana na mapato ya ndani.

Amesema kiasi hicho cha mapato ya ndani kimepangwa kupatikana kutoka kwenye makusanyo ya kodi, yanayokadiriwa kuwa Shilingi trilioni 26.73 ambazo zitakusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) na Shilingi trilioni 4.66 kutoka kwenye mapato yasiyokuwa ya kikodi.

Dk. Nchemba amesema Serikali inatarajia kukopa Shilingi trilioni 5.44 kutoka kwenye soko la ndani; kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 3.54 ni kwa ajili ya kulipa hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Shilingi trilioni 1.90 ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Amesema pembeni ya fedha hizo, Serikali inatarajia kukopa Shilingi trilioni 2.10 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa lengo la kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kuhusu matumizi, Dk. Nchemba amesema Serikali imepanga kutumia Shilingi trilioni 44.39 kwa matumizi ya kawaida na ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kulipa deni la Serikali na gharama nyingine za mfuko mkuu.

“Katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imepanga kutumia jumla ya Shilingi trilioni 44.39 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya kiasi hicho, Shilingi trilioni 30.31 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha Shilingi trilioni 12.77 kwa ajili ya deni la Serikali na gharama nyingine za mfuko mkuu.

“Shilingi trilioni 10.88 kwa ajili ya mishahara ikiwemo nyongeza ya mishahara, upandishaji wa madaraja na ajira mpya na Shilingi trilioni 1.14, ni ruzuku ya maendeleo kwa ajili ya kugharamia elimu ya msingi na sekondari bila ada pamoja na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu,” amesema Dk. Nchemba.

Dk. Nchemba amesema matumizi mengineyo yametengewa Shilingi trilioni 5.52 na aidha; matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Shilingi trilioni 14.08; ikijumuisha gharama za utekelezaji wa miradi mbalimbali katika ngazi ya Serikali Kuu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.   

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya