Sunday, September 7, 2025
spot_img

WAZIRI MKUU MAJALIWA ATAKA USHIRIKIANO MIRADI YA MAJI

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameielekeza Wizara ya Maji kuendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya maji kukamilisha miradi yote inayoendelea kutekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Pia, Majaliwa amesema Wizara ya Maji itengeneze na kutekeleza mwongozo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuimarisha uwekezaji katika sekta ya maji kwa kushirikiana na wadau wote muhimu.

Majaliwa alitoa maelekezo hayo jana, Juni 13, 2023 alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye uzinduzi wa mpango wa nchi wa WaterAid (2023-2028) na maadhimisho ya miaka 40 ya Shirika la WaterAid Tanzania. Hafla hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Alisema Serikali inatambua mchango wa Shirika la WaterAid katika kutekeleza programu ya maendeleo ya sekta ya maji kwa awamu zote za utekelezaji wake.

“Na leo kupitia maadhimisho haya, sina budi kuwapongeza Shirika la WaterAid Tanzania kwa kutimiza miaka 40 ya kazi nzuri mnayofanya ya kushirikiana na Serikali kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa,” alisema.

Majaliwa aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali nchini, na alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao na itazingatia makubaliano, miongozo na taratibu zote ili kuhakikisha kwamba wanatekeleza miradi mingi zaidi mijini na vijijini kwa maslahi ya Watanzania.

Kadhalika, Majaliwa alizitaka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kutenge fedha za kutosha kutekeleza mwongozo wa mpango kabambe wa afya wa halmashauri (CCHP).

“Hii itasaidia kupatikana kwa huduma muhimu za maji safi na salama, vyoo bora na vifaa vya kunawia mikono zinatekelezwa kwenye vituo vyote vya elimu na afya hapa nchini,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mary-Prisca Mahundi alisema makisio ya bajeti ya mpango wa nchi wa WaterAid (2023-2028) ni Shilingi bilioni 45.87 ambapo kuna ongezeko la Shilingi bilioni 9.07 ikilinganishwa na mpango uliopita.

Alisema fedha zilizotengwa kwenye mpango mpya zitatumika kuboresha sekta ya maji katika maeneo ya huduma endelevu, jumuishi na salama ili kuleta mabadiliko makubwa. “Nitumie fursa hii kuwapongeza WaterAid Tanzania kwa kutekeleza mpango wao uliopita,” alisema.

Aidha, Mahundi aliwashukuru wadau wote wa maendeleo wanaochangia kufanikisha utekelezaji wa miradi ya sekta ya maji kwa kuwa michango yao ya kifedha na kitaaluma ni muhimu katika kuendeleza na kuboresha utoaji huduma.

Awali, Mkurugenzi Mkaazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga alisema shirika hilo katika kipindi cha miaka 40 tangu lianze kazi nchini, limeshirikiana na Serikali kuwafikishia huduma za maji watu milioni nane, ambapo watu 800,000 walipatiwa vyoo bora na watu milioni 26 walihamasishwa masuala ya usafi wa mazingira wanayofanyia kazi katika mikoa 11 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema katika utekelezaji wa kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani, WaterAid kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo watahakikisha kampeni hiyo inafanikiwa na maji yanapatikana.

Akizungumzia kuhusu mkakati mpya wa WaterAid uliozinduliwa jana, Mzinga alisema utazingatia maeneo makuu mawili ambayo ni kufikia huduma endelevu, jumuishi na salama za maji, vyoo na usafi binafsi kwenye maeneo lengwa ya kijiografia pamoja na kutoa kipaumbele cha maji, vyoo bora na usafi binafsi katika sekta ya afya ili kuboresha afya ya umma.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya