RIPOTA PANORAMA
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limetakiwa kurejesha Shilingi bilioni 1.95 ambazo ukaguzi wa matumizi yake haukuthibitika.
Aliyependekeza fedha hizo zirejeshwe ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambaye ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/22, inasema TANAPA lilishindwa kuthibitisha usahihi na uhalali wa malipo ya fedha hizo.
“Hifadhi za Taifa Tanzania imepata hasara ya Shilingi bilioni 1.95 kama malipo ambayo matumizi yake hayakuweza kuthibitishwa. Ninapendekeza manejimenti ya Hifadhi za Taifa Tanzania kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa,” anasema CAG.
Ripoti hiyo pia inaonyesha jinsi TANAPA lilivyolipa wafanyakazi wake posho inayozidi viwango vilivyoainishwa kwenye miongozo ya malipo ya aina hiyo; na pia inafichukua kuwa, TANAPA liliwalipa wafanyakazi wake mamilioni hayo mkononi badala ya kuyapitishia benki.
Ripoti hiyo ya ukaguzi maalumu uliofanywa na CAG kwa TANAPA, inasema shirika hilo lilibainisha utekelezaji wa majukumu na malipo mbalimbali yaliyofanyika kupitia hati za malipo 40, ambazo usahihi na uhalali wake haukuweza kuthibitika.
“Ukaguzi wangu ulibaini kuwa Hifadhi za Taifa Tanzania, ilibainisha utekelezaji wa majukumu na malipo mbalimbali yenye jumla Shilingi bilioni 1.95 yaliyofanyika kupitia hati za malipo 40, lakini usahihi na uhalali wa malipo hayo haukuweza kuthibitishwa kutokana na kukosekana kwa nyaraka sahihi za viambatanisho, licha ya kuorodheshwa kwa majina ya waliolipwa.
“Mbali na utekelezaji usiothibitishwa wa majukumu hayo, jumla ya Shilingi bilioni 1.34 zilionyesha kupokelewa na watumishi mbalimbali kupitia hati za malipo zilizosainiwa huku jumla ya Shilingi milioni 611.55 zikishindwa kuthibitishwa kuwa zimepokelewa na watumishi husika,” anasema CAG katika ripoti yake.
Kuhusu TANAPA kuwalipa watumishi wake posho zaidi ya viwango vilivyoidhinishwa, CAG anafafanua kuwa shirika hilo limeweka miongozo ya matumizi yenye kumbukumbu nambari BE.38/340/01/01 na kumbukumbu nambari BE/38/340/01/02.
CAG anasema miongozo hiyo imeweka viwango vya posho za kazi na posho za honoraria, zilizotakiwa kuanza kutumika Mei mosi, 2017 na Julai 9, 2018 mtaliwa.
“Pamoja na utoaji wa miongozo hiyo, nilibaini kuwa Hifadhi za Taifa Tanzania ililipa posho mbalimbali za wafanyakazi jumla ya Shilingi milioni 38.72 zaidi ya viwango vilivyoainishwa katika miongozo hiyo.
“Pia nilibaini kuwa malipo haya yalifanyika kwa wafanyakazi mbalimbali kwa fedha taslimu badala ya akaunti za benki katika miaka ya fedha 2019/20 na 2020/21. Ninapendekeza menejimenti ya Hifadhi za Taifa Tanzania kuhakikisha udhibiti wa malipo kwa kuzingatia viwango halisi, na kama ilivyoainishwa katika miongozo,” anasema CAG.
Katika hatua nyingine, vyanzo vya habari vilivyozungumza na Tanzania PANORAMA Blog mkoani Mwanza, vimedai kuwa vita ya vigogo ndani ya mamlaka hiyo, vinavyoenda mbali zaidi kwa kuyahusisha majina ya baadhi ya viongozi wakubwa vinaitafuna na kudumaza ufanisi wake, jambo linalotishia kutimia kwa malengo ya Serikali ya ustawi wa sekta ya utalii nchini.
“CAG amebainisha utafunaji huo wa fedha, umesikia kuna hatua yoyote imechukuliwa. Fedha inatafunwa kweli kweli, wamejijengea uzio wanajua hakuna wa kuwagusa, uliza kama kuna hatua zimechukuliwa kama alivyosema CAG.
“lakini tatizo kubwa ni vita inayoitwa ya vigogo. Sisi sasa tuko huku mikoani na tunayo mengi ya kusema. Kwa sababu tumejiridhisha na kazi yenu maana tunawafuatilia sana na uzuri ninyi PANORAMA taarifa zenu zinasambaa sana. Tutasema kwa sababu sasa mnaaminika ili umma ujue hali ilivyo,” kilisema chanzo kimojawapo cha habari.
Tanzania PANORAMA Blog imemuuliza Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA,William Mwakilema (pichani juu) hatua zilizochukuliwa kutekeleza yaliyomo kwenye ripoti ya CAG, lakini Kamishna Mwakalema hakujibu chochote.
USIKOSE KUUNGANA NA TANZANIA PANORAMA BLOG KUSOMA HABARI ZA KINA KUHUSU YANAYODAIWA KUFICHIKA TANAPA