RIPOTA PANORAMA
SHILINGI bilioni 1.4 za mfuko wa tuzo na tozo wa Jeshi la Polisi, zimetumiwa vibaya na jeshi hilo kwa kuchepushwa na kutumiwa kwenye matumizi yasiyohusiana na mfuko.
Fedha zilizotumiwa vibaya ni pamoja na Shilingi bilioni moja zilizotolewa kwenye mfuko wa tuzo na tozo wa Jeshi la Polisi zikiwa zimekusudiwa kulipa fidia polisi 223 waliopata majareha wakiwa wanatekeleza majukumu yao, huku kukiwa hakuna askari polisi aliyepa majeraha kwa kiwango hicho cha kustahili kulipwa fidia.
Sambamba na kashfa hiyo, Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, naye alijitwalia Shilingi milioni 34.90 kwa kutumia hati saba za malipo. Fedha hizo alizichepusha kutoka kwenye fungu la Shilingi milioni 446.03 lililoidhinishwa mwezi Machi na Mlipaji Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya kulipa mafao kwa maafisa wa polisi wanaostahili.
Ubadhirifu huo wa fedha nyingi ndani ya Jeshi la Polisi umefichuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/22 ambayo inajumuisha ukaguzi maalumu wa kiuchunguzi alioufanywa kwenye Jeshi la Polisi.
Katika ripoti yake hiyo ya ukaguzi maalumu alioufanya kwenye Jeshi la Polisi, CAG anasema kati ya Julai 2018 na Novemba 2021, jeshi hilo lililotoa Shilingi bilioni 26.52 kwenye mfuko wa tuzo na tozo kwa ajili ya matumizi mbalimbali yaliyoainishwa na sheria ya uanzishwaji wa mfuko, pamoja na kutoa mafao kwa askari polisi waliopata majereha wakati wakitekeleza majukumu yao.
Mfuko wa tuzo na tozo wa Jeshi la Polisi ulianzishwa kwa mujibu wa amri za jumla za polisi (GPO) na huendeshwa kupitia utoaji huduma za ulinzi kwa taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi.
Fedha zinazokusanywa kwenye mfuko huo zimelengwa kusaidia familia za askari polisi waliofariki, kutoa zawadi kwa maafisa wa polisi waliopona kwenye mashambulizi ya silaha na kugharamia matumizi mengine yenye manufaa kwa polisi.
Hata hivyo, ni sharti kwamba malipo kutoka kwenye mfuko huo kuidhinishwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.
“Kwa mujibu wa kanuni ya 4(1) ya kanuni za fidia za Jeshi la Polisi na Magereza za mwaka 2010, afisa wa polisi ambaye anapata majeraha mabaya au kifo wakati akitekeleza wajibu wake, anastahili fidia kulingana na kiwango cha jeraha au kifo.
“Jeshi la Polisi Tanzania liliweka kiwango cha malipo ya fidia ya Shilingi milioni 15 kwa afisa wa polisi atakayefariki kutokana na majeraha atakayoyapa wakati wa kutekeleza majukumu yake. Malipo hayo hutolewa kwa ndugu wa karibu au mrithi wa afisa aliyefariki,” anasema CAG.

Msemaji wa Jeshi la Polisi. Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) David Misime
Akiendelea, CAG anasema kati ya fedha zilizotolewa kwenye mfuko, kiasi cha shilingi bilioni moja kililipwa kwa walengwa 223 waliopata majeraha wakati wakitekeleza majukumu yao.
Anasema katika ulipaji huo viwango vya fidia vilitofautiana kutoka Shilingi milioni 1.05 hadi kiwango cha juu cha Shilingi milioni 15. Tofauti hiyo ya kiwango cha malipo inakinzana na miongozo ya ulipaji fidia inayoelekeza kulipa Shilingi milioni 15 kwa kila mfidiwa.
CAG anasema baada ya uchunguzi kufanyika, iligundulika kuwapo udanganyifu katika malipo hayo kwani hakukuwa na afisa yeyote aliyepata majeraha wakati akitekeleza majukumu yake kiasi cha kustahili malipo ya fidia.
“Hata hivyo, baada ya uchunguzi zaidi, iligundulika kuwa hakukuwa na afisa yeyote wa Jeshi la Polisi aliyepata majeraha kwa kiwango ambacho alistahili malipo ya fidia. Hii inathibitisha uwapo na ubadhirifu wa fedha katika mfuko wa tuzo na tozo,” anasema.
CAG anaendelea kuanika ubadhirifu wa fedha za mfuko huo kwa kueleza kuwa, Mhasibu Mkuu Jeshi la Polisi alitumia hati za malipo saba kuchepusha Shilingi milioni 34.90 kutoka kwenye fungu la Shilingi milioni 446.03 zilizokuwa zimeidhinishwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kulipa mafao ya maafisa wa polisi wanaostahili.
“Tukio jingine la matumizi mabaya linahusisha kuidhinishwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali utoaji wa kiasi cha Shilingi milioni 446.03 mnamo Machi, 2021 ili kulipa mafao ya maafisa wa polisi wanaostahili.
“Hata hivyo, iligundulika kuwa mnamo mwezi Juni, 2021, Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi alitumia hati za malipo saba kuchepusha kiasi cha Shilingi milioni 34.90 katika kiasi kilichoidhinishwa na kufanya matumizi yasiyoendana na malengo yaliyokusudiwa na mfuko.
“Kulingana na matokeo ya uchunguzi, ukaguzi ulithibitisha kuwa Jeshi la Polisi Tanzania lilitumia vibaya kiasi cha Shilingi bilioni 1.04 kutoka kwenye mfuko wa tuzo na tozo kutokana na uchepushaji na matumizi yasiyohusiana na dhumuni la mfuko.
“Aidha, Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, alichangia kwa kiasi kikubwa katika usimamizi mbovu wa fedha za mfuko kwa kugeuza matumizi ya fedha za mfuko bila ya kuzingatia maelekezo ama vibali vilivyotolewa na mlipaji mkuu wa Serikali,” anasema CAG.
Anasema hatua za haraka za kinadhimu na kisheria zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya wote waliohusika na usimamizi mbovu wa matumizi ya fedha za mfuko wa tuzo na tozo katika jeshi la polisi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) David Misime alipozungumzia hilo, alisema bila kufafanua kuwa, maelekezo yalikwishatolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia walielekeza taarifa na majibu wapi pa kufukisha.