RIPOTA PANORAMA
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetoa vitambulisho vya Taifa kwa watoto ambao hawajazaliwa, wakimbizi na waombaji zaidi ya mmoja walioomba vitambulisho kwa kutumia cheti kimoja cha kuzaliwa.
Tathmini ya shughuli za NIDA katika utoaji vitambulisho vya Taifa iliyofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyomo kwenye ripoti yake kwa mwaka 2021/22 inaonyesha kuwa NIDA imeshindwa kuzalisha vitambulisho vya Taifa 7,188,098 na iko hatarini kusajili wahamiaji haramu.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, NIDA ilitoa nambari za vitambulisho vya Taifa (NINs) kwa watu 15 ambao walikuwa na umri chini ya miaka 18 na au ambao miaka yao ya kuzaliwa ni zaidi ya mwaka 2023 ikiwa ni pamoja na nambari za usajili 20430101654160000124, 20490401655180000119 na 20320701655050000127 kwa watu waliozaliwa mwaka 2043, 2049 na 2032 mtawalia.
Kwa mujibu wa kanuni ya 4 (2) ya kanuni za usajili ya utambulisho wa watu ya mwaka 2014, inaelekeza mtu ambaye ametimiza masharti yaliyotajwa kwenye sheria kufanya maombi ya usajili ndani ya siku 90 baada ya kufikisha umri wa miaka 18.
Mbali na hilo, tathmini ya CAG kwenye shughuli za NIDA za utoaji vitambulisho vya Taifa imebaini kuwa mamlaka hiyo ilitoa nambari za usajili wa vitambulisho vya Taifa kwa watu 21 waliiomba kwa kutumia cheti kimoja cha kuzaliwa.
“Kanuni ya 5 (5) (b) (i) ya kanuni za usajili na utambulisho wa watu ya mwaka 2016, inamtaka kila mtu anayeomba kusajiliwa, kuwasilisha cheti cha kuzaliwa au ushahidi wa maandishi wa kuzaliwa kwa afisa usajili.
“Hata hivyo, nilipitia taatifa za usajili wa NIDA na nilibaini kuwa nambari za vitambulisho vya Taifa (NINs) za watu 21 zilitolewa kwa kutumia cheti za kuzaliwa kimoja chenye nambari 292/2010 pekee,” anasema CAG.
Aidha, ukaguzi wa CAG kwa NIDA ulibaini kuwa mamlaka hiyo ilipanga bila mafanikio kuzalisha vitambulisho 10,043,868 kwa mwaka wa fedha 2021/22 na badala yake ilizalisha vitambulisho 2,855,770, hivyo kushindwa kufikia lengo kwa asilimia 72.
“Kifungu cha 2 (1) cha sheria ya uanzishwaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ya mwaka 2008, kinaitaka mamlaka kutoa vitambulisho vya Taifa kwa raia wa Tanzania wanaostahili, wakazi halali na wakimbizi.
“Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka ya usimamizi wa vitambulisho (IDM), NIDA ilipanga kuzalisha vitambulisho 10,043,868 katika mwaka wa fedha 2021/22. Hata hivyo ripoti hiyo ilionyesha kuwa ni vitambulisho 2,855,770 pekee vilivyozalishwa katika kipindi hiki hivyo kuacha pengo la uzalishaji wa vitambulisho vya Taifa 7,188,098 kutofikiwa (sawa na asilimia 72),” anasema CAG.
Anasema udhaifu uliobainika NIDA, kimsingi ulisababishwa na udhibiti wa ndani usioridhisha wa kuthibitisha taarifa zinazoingizwa kwenye mfumo pamoja na ukosefu wa kadi ghafi za kizazi cha pili uliosababisha upungufu wa uzalishaji wa vitambulisho.
CAG anasema iwapo udhaifu huo hautashughulikiwa haraka, NIDA inakabiliwa na hatari ya kusajili wahamiaji haramu na kushindwa kutoa vitambulisho kwa wananchi wanaostahili.
Anasema NIDA inapaswa kuboresha udhibiti wa ndani kwa ajili ya kuhakiki taarifa zilizoingizwa kwenye mfumo wa usajili na kuharakisha upatikanaji wa kadi ghafi za kizazi cha pili ili kuzalisha vitambulisho vya kutosha.