RIPOTA PANORAMA
NDEGE ya Tanzania iliyokuwa ikitengenezwa nchini Canada, ilikamatwa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Haki ya Ontario ya Canada baada ya kutoa hukumu ya kukazia hukumu ya Mahakama Kuu ya Haki ya Uingereza na Wales.
Mahakama Kuu ya Haki ya Uingereza na Wales iliihukumu Serikali ya Tanzania kuilipa Kampuni ya Wallis Trading Inc, Dola za Marekani 40,180,887.51 pamoja na riba iliyolimbikizwa ya ukodishaji ndege ya kampuni hiyo, aina ya Airbus A320 – 310 kwa muda wa miezi 72.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/22, mwaka 2007 Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Ndege ya Tanzania, Air Tanzania Limited, ilisaini mkataba na Kampuni ya Wallis Trading Inc wa kukodisha na kuendesha ndege yake kwa malipo ya Dola za Marekani 315,000 kwa mwezi na akiba ya matengenezo.
Ripoti inaeleza kuwa majukumu ya Air Tanzania chini ya ukodishaji wa uendeshaji, yalitokana na dhamana iliyotolewa na Serikali Aprili 2, 2008.
Kwa mujibu wa ripoti, kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2013, Serikali ya Tanzania ilishindwa kuilipa kampuni hiyo na hivyo deni lilikua hadi kufikia Dola za Marekani 45,103,838.85 na mwaka huo wa 2013, Serikali ya Tanzania iliingia makubaliano mapya na Kampuni ya Wallis Trading Inc ambapo iliilipa Dola za Marekani 26,115,436.75 na kubakiza deni la Dola za Marekani 18,988,410,10.
Ripoti inaeleza kuwa mwaka 2017, Kampuni ya Wallis Trading Inc ilikimbilia mahakamani ambako ilifungua kesi ya madai ya Dola za Marekani 30,114,230,73 dhidi ya Serikali ya Tanzania katika Mahakama Kuu ya Haki ya Uingereza na Wales.
Kwamba msingi wa kesi hiyo ulikuwa Serikali ya Tanzania kushindwa kulipa deni lililobakia la kukodisha na kuendesha ndege kutoka Kampuni ya Wallis Trading Inc pamoja na riba na ilipofika mwaka 2020, Mahakama Kuu ya Haki ya Uingereza na Wales ilitoa hukumu iliyoitaka Serikali ya Tanzania kulipa Dola za Marekani 40,180,887.51 pamoja na riba iliyolimbikizwa.
“Hata hivyo, Serikali haikutekeleza agizo la mahakama na mnamo Aprili 2021, Wallis Trading Inc iliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Haki ya Ontario nchini Canada ikitaka kutambulika na kutekelezwa kwa hukumu hiyo ya Mahakama ya Uingereza.
“Mnamo tarehe 29 Aprili, 2021, Wallis Trading Inc ilikamata ndege ya Serikali, De Havilland Canada Limited 8-402 Q400 ambayo ilikuwa ikiundwa nchini Canada. Kutokana na hali hiyo, Serikali iliingia mkataba na Wallis Trading Inc tarehe 7, Julai 2021 na kuahidi kulipa fedha za Canada, jumla ya CAD 60,921,953.56, sawa na Dola za Marekani 48,679,146.56 ifikapo tarehe 22 Julai, 2021,” inaeleza ripoti.
Kuhusu utekelezaji wa ahadi hiyo, ripoti inaeleza kuwa Serikali ya Tanzania ilitekeleza wajibu wake chini ya mkataba uliowekwa, Julai 14, 2021 kwa kuilipa Kampuni ya Wallis Trading Inc, Dola za Marekani 48,679,146.56 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 112.47.
Akitoa tathmini yake kuhusu hilo, CAG anasema Serikali ilipata hasara ya Dola za Marekani 29,690,736.46 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 68.60 kwa sababu ya kushindwa kulipa deni lililoiva la Dola za Marekani 18,988,410.10 Oktoba, 2013 hivyo kusababisha ongezeko la riba na ada za kisheria zilizofikia Dola za Marekani 48,679,146.56.
“Hasara iliyoipata Serikali ilichangiwa zaidi na kutofanya maamuzi kwa watendaji wenye dhamana ya kusimamia shughuli za Serikali ipasavyo na hivyo kusababisha mzigo mkubwa kwa fedha za walipa kodi.
“Malipo hayo yasiyokuwa na tija yangeweza kuepukwa na fedha hizo zingeweza kutumika kwa mipango mbadala ya Serikali,” inaeleza ripoti.