JULIUS MUKAMBI
Nairobi, Kenya
KASISI Paul Mackenzie, kiongozi wa Kanisa la Good News International la Kenya, kwa miaka mingi aliongoza ibada za vifo za mamia ya waumini wake waliofariki dunia kwa njaa, kiu na kunyongwa kwa utaratibu wa kuwafanyia ibada ya sherehe za harusi.
Tofauti kabisa na utaratibu wa kawaida wa maisha ya binadamu, Kwa Kasisi Mackenzie, kifo ni harusi. Hakujali namna au mazingira ya kifo, kwake yeye ibada ya mazishi ilikuwa sherehe ya harusi.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa muda wote alipokuwa Shakahola akiongoza kanisa lake huku akiwahubiri upotovu, waumini na wafuasi wake; nao wakiwa katika hali ya kupotoka hata kukubali kwa hiari yao kukikabili kifo cha njaa, kiu na kunyongwa, walipokufa, hakuwazika patupu, aliwafanyia ibada ya sherehe ya kufa; sherehe ya harusi ya kufa.
Ingawa waumini na wafuasi wake walikufa kwa mateso na maumivu makali ya njaa na kiu, kabla ya kuwazika aliwaaga kwa kuwafanyia ibada hiyo ya harusi kama ishara ya kuwatambua kuwa ni mashujaa wa imani aliyoiasisi yeye. Huyo ndiye Kasisi Mackenzie.
Wasaidizi wake, ambao aliwasambaza katika vijiji alivyovibuni kwenye pande kubwa la ardhi analolimiliki huko Shakahola, miongoni mwa kazi zao ilikuwa kuhakikisha wafuasi wa kasisi huyo wanatekeleza mfungo wa kutokula na kunywa hadi kifo kinapowafika; kisha wanachimba makaburi ya kuwazika wafu hao kwa mafungu kabla ya kumuita Kasisi Mackenzie kuongoza ibada ya mazishi; lakini tofauti na yeye, wasaidizi wake waliipa ibada hiyo jina la sherehe za makosa.
Utekelezaji wa mpango wa kifo kama njia ya kwenda kwa Mungu ambao Kasisi Mackenzie alikuwa amewapatia waumini wake, ulianza na watoto ambao walitakiwa kufa kwanza, kisha wanawake na mwisho wanaume.
Nao waumini hao, waliutii mpango huo na kuutekeleza kwa kile walichoamishwa naye kuwa baada ya kufa wanakwenda moja kwa moja kuonana na Mungu na kwamba walipaswa kufa mapema kabla ya kufika kwa mwisho wa duniani ambao umekaribia; na mwisho wa dunia utawadia Mungu akiwa na ghadhabu kubwa dhidi ya ulimwengu.
Katika kukiendea kifo, waliofanikiwa kufa kwa njaa walizikwa kwa utaratibu aliokuwa ameuweka wa wafu wengi kuzikwa kwenye kaburi moja na kwa wanye roho ngumu, waliokuwa wakichelewa kufa walikuwa wanasaidiwa kukienda kifo na wasaidizi wake wanaotajwa kuwa na maumbo makubwa, yenye misuli ya haja ambao waliwaua kwa kutumia kifaa chenye ncha butu na wakati mwingine kwa kuwanyonga na baada ya kuagwa naye Kasisi Mackenzie kwa ibada ya sherehe ya harusi, nao walizikwa kwa staili ile ile ya wafu wengi kuzikwa kwenye kaburi moja.
Haya yanabainishwa na vinywa vya baadhi ya waumini wake waliookolewa wakiwa hai lakini dhoofu wa miili kwa sababu ya njaa na kiu. Hata hivyo wengi wa waumini wa Kasisi Mackenzie waliookolewa na kifo, licha ya kuwa katika hali ya udhaifu, walikuwa wakikataa msaada wa kuepushwa na kifo na badala yake walitaka waachwe wafe; wakizingatia zaidi mafundisho yaliyowakaa vichwani mwao kutoka kwa Kasisi Mackenzie.
Kasisi Mackenzie sio jina geni kwa Wakenya. Kwa sasa ndiye kasisi aliyezua gumzo duniani licha ya kuwa korokoroni huku kazi ya kufukua makaburi ya mamia ya waumini wake aliowazika huko Shakahola, Akaunti ya Kilifi iliyopo Pwani mwa Kenya ikiendelea.
Kabla ya kukamatwa na kutiwa korokoroni, Kasisi Mackenzie aliliongoza Kanisa la Good News International ambalo msingi wa mahubiri yake ilikuwa waumini na wafuasi wa kanisa hilo kufunga kula na kunywa hadi kufa ili wakakutane na Mungu huko mbinguni kabla hajarejea duniani kuja kutoa hukumu kwa wema na wabaya.
Wakati wote wa uhai wa kanisa hilo, mamia ya watu walioamini imani hiyo walikufa kwa njaa na kiu hadi siku za karibuni kasisi huyo alipotiwa nguvuni kisha kugundulika kwa makaburi mengi yaliyozika mamia ya wafuasi wake.
Maafisa wa Serikali ya Kenya walioongoza kazi ya kufukua makaburi huko Shakahola wamethibitisha wafu wengi kuzikwa kwenye kaburi moja na kwa upande kwa maafisa wa afya wanaoifanyia uchunguzi miili ya wafu, wanasema wafu wengi walipoteza maisha kwa sababu ya njaa, kiu na kunyongwa.
Nje ya taarifa hizo, zipo pia taarifa nyingine zinazodai kuwa baadhi ya wafu waliokwisha fanyiwa uchunguzi wamegundulika miili yao kukosa baadhi ya viungo hivyo kuibua hisia kuwa huenda kasisi huyo alihusika pia na biashara haramu ya viungo vya binadamu.
Ikiwa ni takribani miezi miwili sasa baada ya kugundulika kwa makaburi ya halaiki ya wafu huko Shakahola, bado mamia ya watu wamekuwa wakifurika eneo hilo kutafuta walipo wapendwa wao ambao walitoweka nyumbani wakiwa na watoto.
Lakini mpaka sasa, baadhi ya waliookolewa wakiwa hai katika msitu wa Shakahola wameshindwa kueleza walipo watoto wao jambo linaloibua hofu kuwa huenda walikufa kwa njaa na kiu au walisaidiwa kukienda kifo kwa kunyongwa na wasaidizi wa Kasisi Mackenzie.
Kasisi Mackenzie tayari amekwishafikishwa katika Mahakama ya Shanzu akiwa na wasaidizi wake 17 na sauti yake kutoka kwenye viunga vya mahakama amekuwa akiielekeza kwa Mungu wake, akisema; ‘yote yanayomtokea ni sehemu ya majaribu ya dunia, lakini Yesu Kristu hatimaye atamuokoa.’
Akiwa nje ya viunga vya mahakama, Kasisi Mackenzie amekuwa akilalamika kuwa hajui ni kwanini anafikishwa mahakamani na haoni maendeleo ya kesi yake. “Ukweli ni kwamba sioni maendeleo yoyote, sina uhakika kwanini nipo hapa, nahisi nimekosewa, najua Yesu ninayemhudumia na kumuamini hatimaye atanisaidia.”
Hii siyo mara ya kwanza kwa Kasisi Mackenzie kukamatwa kutokana na mahubiri yanayokinzana na taratibu za kawaida za maisha ya binadamu. Amepata kukamatwa mara mbili akaachiwa na moja ya kesi zilizomfikisha mahakamani iliamriwa na mahakama alipe faini ya Shilingi 10,000 za Kenya.
Wakati Kasisi Mackenzie akilalama kutoelewa mwenendo wa kesi yake, kwa upande wa Serikali, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Profesa Kithure Kindiki ametoa msimamo wa Serikali kuwa kasisi huyo hataachiwa kwa sababu ameua watu wengi zaidi ya magaidi walivyoua watu miaka 10 iliyopita.
“Mackenzie hataondoka jela tena. Atazeeka huko. Tunamuomba Mungu ampe miaka mingi kushuhudia Kenya salama. Atabaki huko (jela) hadi kifo chake ambapo ataenda kwa shetani au Mungu endapo atatubu,” amesema Waziri wa Usalama wa Ndani.
“Hata kama mahakama itamuchia huru tutamrudisha huko. Wakati mwingine kwa kawaida tunaziambia mahakama zetu kwamba mtu ni muuaji lakini wanawaachia huru nadhani kwa kunukuu Katiba. Ataondoka tu gerezani akiwa amekufa,” hayo ni maneno ya Profesa Kindiki.
JULIUS KINDIKI NI MWANDISHI WA TANZANIA PANORAMA BLOG ALIYEKO NAIROBI, KENYA.