RIPOTA PANORAMA
MKATABA wa ubia wa kukuza na kuendesha soko la kibiashara la Darajani Corridor, lililopo Zanzibar baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mwekezaji, wenye thamani ya Shilingi bilioni saba una udhaifu.
Pamoja na udhaifu huo, ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenye mradi huo wa ubia baina ya CCM na mwekezaji ambaye hajatajwa na CAG, ulishindwa kukokotoa mgao wa faida baina ya wabia hao wawili kutokana na kukosekana kwa taarifa za kifedha.
Ripoti ya ukaguzi wa vyama vya siasa ya CAG kwa mwaka 2021/22, inaeleza kuwa ukaguzi wake ulishindwa kuthibitisha mgawanyo wa faida katika mradi huo wa ubia unaoonyesha faida itakayopatikana miaka 15 ya kwanza, mgawanyo wake utakuwa asilimia 70 kwa 30 na miaka kumi inayofuata, mgawanyo wa faida utakuwa asilimia 60 kwa 40.
Aidha, CAG anaeleza kuwa ukaguzi wake kwenye mkataba huo wa ubia, uligundua haukuwa na kifungu cha ukaguzi wa gharama za mradi baada ya kukamilika hivyo kuwepo hatari ya gharana zilizokadiriwa kutokuwa sahihi.
“Wakati wa ukaguzi wangu, nilibaini kuwa mnamo mwezi Januari 2022, Chama Cha mapinduzi (CCM) na mwekezaji walitia saini mkataba wa ubia ili kukuza na kuendesha soko la kibiashara la Darajani Corridor lililopo Zanzibar kwa kipindi cha miaka 25, kuanzia Januari, 2022 hadi Januari 2047.
“Gharama za mradi zilikadiriwa kuwa Shilingi bilioni saba na mgawanyo wa faida kati ya Chama Cha Mapinduzi na mwekezaji ulikuwa asilimia 70 kwa 30 kwa miaka 15 ya kwanza na asimilia 60 kwa 40 kwa miaka 10 iliyobakia, mtawalia.
“Hata hivyo, sikuweza kukokotoa msingi wa kuamua mgao huo. Aidha, mkataba wa ubia haukuwa na kifungu cha ukaguzi wa gharama za mradi baada ya mradi kukamilika jambo ambalo linaweza kuathiri usahihi wa gharama zilizokadiriwa,” anaeleza CAG katika ripoti yake.
Akizungumzia kile kilichoelezwa na uongozi wa CCM kuhusu udhaifu na dosari hizo kwenye mkataba, CAG anasema uongozi wa CCM ulisema mgao wa faida utazingatia faida halisi itakayopatikana.
“Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi ulieleza kuwa mgao wa faida utazingatia faida halisi itakayopatikana. Hata hivyo, mkataba wa ubia hauhitaji mwekezaji kuandaa na kuwasilisha taarifa za kifedha.
“Kutokuwepo kwa taarifa za kifedha kutafanya iwe vigumu kujua faida halisi itakayopatikana na kutia shaka ya usawa na usahihi wa mgao wa faida halisi itayopatikana,” anaeleza CAG.
Ripoti ya CAG inaeleza zaidi kuwa wakati wa ukaguzi, alibaini kanuni za fedha za Chama Cha Mapinduzi zinaelekeza kuwepo kwa msimamizi wa mradi kwa mradi wowote unaotekelezwa na chama hicho lakini katika mradi huo hakuna msimamizi.
“Aidha, nilibaini kuwa kanuni za fedha za Chama Cha Mapinduzi zinahitaji uteuzi wa msimamizi wa mradi kwa mradi wowote unaotekelezwa na Chama Cha Mapunduzi. Msimamizi wa mradi anawajibika kufuatilia na kuripoti maendeleo ya mradi kwa bodi ya wadhamini ya chama.
“Hata hivyo, wakati wa ukaguzi hakukuwa na msimamizi wa mradi aliyeteuliwa ili kusimamia utekelezaji wa mradi huu. Hii inamaanisha kuwa bodi ya wadhamini ya chama haikuwa na taarifa za kutosha kuhusu maendeleo ya mradi.
“Kukosekana kwa taarifa za utekelezaji wa mradi kunaweza kusababisha matumizi mabaya ya rasilimali za chama na kushindwa kugundua vitendo vya udanganyifu kwa wakati,” anaeleza CAG.
Akiendelea, anaeleza kuwa uwekezaji uliofanywa na CCM una upungufu kwa sababu hakuna taarifa za kifedha na hakuna usimamizi wa mradi, mambo ambayo yanadhoofisha uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya chama.
Anasema ni vigumu kuthibitisha kama uwekezaji huo una manufaa au una mashaka katika utekelezaji wake na kwamba bodi ya wakurugenzi inapaswa kukutana na menejimenti kujadili maendeleo ya mradi huo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema alipoulizwa alisema chama chake kilitoa taarifa kwa umma baada ya CAG kusoma ripoti yake na kuahidi kuitoa kwa Tanzania PANORAMA Blog jambo ambalo hakulitekeleza na hata alipokumbushwa tena kuitoa taarifa hiyo kama alivyoahidi, hakuitoa.