RIPOTA PANORAMA
BENKI ya Biashara ya DCB ya jijini Dar es Salaam ambayo Serikali ndiye mwanahisa mkubwa ikimiliki asilimia 63 ya mtaji wote, kwa takribani miaka 20 sasa haijawahi kupeleka taarifa zake za fedha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukaguliwa.
Kutokaguliwa kwa hesabu za benki hiyo kumefichuliwa na CAG kwenye ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/22; ripoti ambayo inayoishauri Serikali kupitia Hazina kutekeleza uzingatiaji wa kifungu cha 30(b) na (e) cha sheria ya ukaguzi wa umma ya mwaka 2008 inayozitaka taasisi zote ambazo Serikali imewekeza fedha zake za zile ambazo ni mwanahisa mkubwa, kuwasilisha hesabu zao ofisini kwake kwa ajili ya kukaguliwa.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 143, kifungu cha 9(a) iii & iv cha sheria ya ukaguzi wa umma, kama kilivyokaririwa na CAG kwenye ripoti yake, kinaelekeza matakwa ya kisheria kwa taasisi ambazo Serikali imewekeza fedha zake na zile ambazo ni mwanahisa mkubwa kuwasilisha taarifa za fedha ofisini kwake kwa ukaguzi.
Hata hivyo, alipoulizwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Isdori Msaki ni kwanini benki yake inakinzana na matakwa ya Katiba ya Nchi kwa kutotekeleza ibara ya 143, kifungu cha 9(a) iii&iv cha sheria ya ukaguzi wa umma, alisema atapanga ratiba ya kuonana kuhusu hilo, kisha akasema yuko nje ya nchi na baadaye akasema hayo ni mambo ya kiserikali na pia majibu anayo aliyeandika ripoti husika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Isdory Msaki
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, Benki ya Biashara ya DCB ilipata usajili Septemba 6, 2001 na Aprili 2002 ilianza biashara kama taasisi ya kifedha ya kanda hadi Juni 12, 2003 ilipopewa leseni ya kufanya biashara ya benki, ikijulikana kwa jina la Dar es Salaam Community Bank (DCB)
Ripoti inaeleza kuwa wanahisa wa benki hiyo ni Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ambayo ina idadi ya hisa 2,281,502 zenye thamani ya Shilingi 570,375,500 na umiliki wake ni asilimia mbili.
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo inatajwa kwenye ripoti kuwa na hisa 2,887,367 zenye thamani ya Shilingi 725,002,250 na umiliki wake ni asilimia 2.96 huku Halmashauri ya Manisapaa ya Temeke ikiwa na idadi ya hisa 3,422,252 zenye thamani ya Shilingi 855,563,000 na umiliki wake ni asilimia 3.49.
Mwanahisa mwingine anayetajwa na ripoti ya CAG ni Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambayo idadi ya hisa zake ni 5,625,019 zikiwa na thamani ya Shilingi 1,406,254,750 na umiliki wake ni asilimia 5.74 na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) una hisa 6,000,000 ambazo thamani yake ni Shilingi 1,500,000,000 na umiliki wake ni asilimi 6.12.
Halmashauri ya Jiji la Ilala nayo ni mwanahisa aliyetajwa kwenye ripoti ikiwa na idadi ya hisa 7,866,895 ambazo thamani yake ni Shilingi 1,989,356,500 huku umiliki wake ukiwa asilimia 8.12 na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ina hisa 10,228,320 ambazo zina thamani ya Shilingi 2,608,023,500 na umiliki wake ni asilimia 10.65.
Kwenye orodha hiyo, kuna Mfuko wa Uwekezaji (UTT) ambao idadi ya hisa zake ni 23,211,479, zikiwa na thamani ya Shilingi 5,802,869,750, zinazoipa umiliki wa asilimia 23.69 na wanahisa wengine 7,335, wana hisa 36,134,115 ambazo thamani yake ni Shilingi 9,033,528,750 zinazowapa umiliki wa asilimia 36.89.
“Halmashauri za Dar es Salaam kwa pamoja zinamiliki asilimia 33 ya mtaji wote wa benki hiyo, ambapo pamoja na mashirika ya Serikali kwa ujumla wanamiliki asilimia 63 ya mtaji wote.
“Hii ina maana kwamba Serikali kupitia vyombo na mamlaka zake inauthibiti wa maslahi katika endeshaji wa benki hiyo kwa kuwa vyombo hivyo vinamilikiwa na Serikali kupitia Msajili wa Hazina. Kwa muktadha huu, DCB inamilikiwa na Serikali kupitia Halmashauri za Serikali za Mitaa, UTT na NHIF.
“Hata hivyo, benki hii hapo awali ilianzishwa kama benki ya binafsi iliyosajiliwa chini ya sheria ya makampuni na kwa hivyo hakuna sheria ya Bunge ya kuanzishwa kwake.
“Kwa sababu hiyo, benki hii haimo kwenye mashirika yanayosimamiwa na Msajili wa Hazina na hivyo haijawahi kuwasilisha taarifa za fedha ofisini kwangu kwa ajili ya ukaguzi kwa mujibu wa ibara ya 143 ya Katiba na kifungu cha 9(a)iii&iv cha sheria ya ukaguzi wa umma namba 11 ya mwaka 2008,” anaeleza CAG katika ripoti yake.
CAG anaandika zaidi akiishauri Serikaki kupitia Hazina kuhusu hesabu za DCB Benki, kutekeleza uzingatiaji wa kifungu cha 30(b) na (e) cha sheria ya ukaguzi wa umma ya mwaka 2008 ambacho kinazitaka taasisi zote ambazo Serikali imewekeza fedha zake na zile ambazo Serikali ndiyo mwanahisa mkubwa kuwasilisha hesabu zao kwake kwa ajili ya ukaguzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa DCB Benki, Msaki ambaye Mei 22, 2023, pamoja na mambo mengine aliulizwa kuhusu mwenendo wa benki anayoiongoza kukinzana na matakwa ya Katiba ya Nchi, alisema atapanga ratiba ya kuonana na PANORAMA kulizungumzia suala hilo lakini wiki hiyo aliyoulizwa alikuwa amebanana.
Mei 31, 2023 alipotafutwa tena alisema yupo nje ya nchi mpaka jumamosi ya Juni 3, 2023 ndipo atakuwa ofisini na alipoelezwa kuwa anaweza kujibu maswali aliyoulizwa kwa njia ya simu au kwa njia ya barua pepe, alisema; “hapana, haya ni mambo ya kiserikali na pia majibu anayo aliyeandika hiyo taarifa.”
Alipoelezwa kuwa aliyeandika ripoti iliyofichua mwenendo wa benki yake kukinzana na Katiba ya Nchi ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mkurugenzi Mtendaji Msaki alisema huyo huyo ndiye anayepaswa kujibu.