Thursday, July 17, 2025
spot_img

TANZANIA NA KENYA ZAJADILI KUBORESHA UHUSIANO SEKTA YA NYUMBA NA MAKAZI

RIPOTA PANORAMA

Nairobi, Kenya

SERIKALI ya Tanzania na Serikali ya Kenya, leo zimeketi katika meza ya mazungumzo jijini Nairobi, Kenya kujadili namna ya kuboresha uhusiano katika uendelezaji wa sekta ya nyumba na maendeleo ya makazi.

Kikao hicho kiliwakutanisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Tanzania, Dk. Angeline Mabula na Waziri wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Kenya, Zachariah Mwangi Njeru.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mabula amesema Serikali ya Tanzania ipo makini kusimamia maendeleo ya sekta ya nyumba na makazi ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu mijini linalofikia asilimia 4.8 kwa sasa.Ā 

Amesema moja ya juhudi za Serikali ni utekelezaji wa mpango wa miaka 10 wa kurasimisha makazi holela ulioanza mwaka 2013 na ili kuwapatia Watanzania nyumba bora, Serikali ilianzisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ambalo kwa kushirikiana na wadau wengi wanaendelea kupunguza uhaba wa nyumba unaofikia nyumba milioni 3.8 hivi sasa.

Waziri Mabula amesema wizara yake iko mbioni kuanzisha mfuko wa kusaidia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kutafuta teknolojia itakayosaidia ujenzi wa nyumba nyingi kwa bei nafuu. 

Akizungumza kuhusu uimarishaji mipaka ya kimataifa, Waziri Mabula amesema Tanzania inaendelea kuweka alama za mipaka kwa kushirikiana na wataalamu wa Kenya na kwamba kazi hiyo inaenda vizuri.

Waziri wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Kenya, Njeru, yeye amesema nchi yake imeanzisha mpango kamambe wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ambao utawezesha ujenzi wa nyumba laki mbili kila mwaka.

Amesema mpango huo utashirikisha sekta binafsi na ili kufanya nyumba hizo kuwa na gharama nafuu, Serikali ya Kenya itaweka miundombinu ya umeme na maji na imeondoa asilimia 16 ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye vifaa vya ujenzi na uuzaji wa nyumba.

Amesema Serikali ya Kenya imeanzisha mfuko wa nyumba utakaochangiwa kwa asilimia tatu na kila mtumishi wa sekta ya umma na binafsi na asilimia tatu nyingine itachangiwa na kila mwajiri. 

Wakihitimisha mazungumzo yao, mawaziri hao wamekubaliana kuunda kamati ya wataalamu kutoka Tanzania na Kenya watakaosimamia utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo yaliyosainiwa mwaka, 2021 jijini Dar es Salaam. 

Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula akishiriki kikao cha mawaziri wa Afrika wanaosimamia nyumba na makazi kilichoketi jijini Nairobi, Kenya leo.

Wakati huo huo, kikao cha mawaziri wa Bara la Afrika wanaosimamia nyumba, makazi na mazingira kimekubaliana kuongeza uwekezaji wa fedha ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuweka mpango madhubuti wa kupunguza idadi ya watu mijini, kudhibiti uharibifu wa mazingira na kuwa na sauti moja kama Afrika ya kuondoa changamoto za makazi na mazingira. 

Akizungumza katika kikao hicho cha mawaziri wa Afrika, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula amesema Bara la Afrika linapaswa kuongeza vitendo zaidi katika kupunguza makazi holela, uharibifu wa mazingira na kuwapa uelewa wa kutosha wananchi ili kupunguza athari hizo.

Amesema Serikali ya Tanzania imekuwa na mipango madhubuti ya kuboresha makazi na kusaidia upatikanaji wa nyumba.

Mkutano wa Shirika la Makazi Duniani unaoendelea jijini hapa utafungwa kesho kwa kupitishwa maazimio kadhaa yanayolenga kuisaidia dunia kukabiliana na uhaba wa nyumba bora, kuondoa makazi holela na mabadiliko ya tabianchi kama yanavyosisitizwa na ajenda ya shirika hilo ya kuwa na malengo endelevu ya miji kufikia 2030.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya