*Shirika hilo kuanzisha ofisi nchini Tanzania
RIPOTA PANORAMA
Nairobi, Kenya
SERIKALI imesaini hati ya makubaliano ya kuboresha ushirikiano kati yake na Shirika la Makazi Duniani (UN- Habitat), Jijini Nairobi, Kenya leo.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Maimunah Mohd Sharif na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Lubala Mabula.
Hati ya makubaliano hayo imelenga kuboresha ushirikiano baina ya Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Shirika la Makazi Duniani katika maeneo mbalimbali.
Maeneo hayo ni pamoja na kutoa utaalamu maalumu kwa kuzingatia viwango vya Shirika la Makazi Duniani, kuchangia na kuweke vipaumbele vya Serikali katika kuwezesha uboreshaji wa makazi holela na kuwezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
Maeneo mengine ya makubaliano ya hati hiyo ni kusaidia matumizi jadidifu ya nishati katika majengo, kupitia na kuandaa sera mpya za miji, kuanzisha kituo cha taarifa ya makazi na kuboresha mifumo ya kitaasisi na uendelezaji wa miji midogo.
Aidha, makubaliano hayo yataliwezesha shirika hilo kuisaidia Tanzania kujenga uwezo katika ngazi ya Taifa, mikoa na Serikali za Mitaa katika utekelezaji wa ajenda mpya ya miji na kuwezesha upatikanaji wa wadau wa maendeleo,
Makubaliano hayo pia yatawezesha mifumo ya Umoja wa Mataifa na wadau muhimu katika kuchangia utekelezaji wa ajenda mpya ya miji na kutengeneza njia na mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa ajenda mpya ya miji na maendeleo endelevu, hasa lengo la 11 na kutoa taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wake.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula na Mkurugenzi Mtendaji wa UN-HABITAT, Maimunah Sharif wakisani hati ya makubaliano ya ushirikiano jijini Nairobi, kenya leo.
Kadhalika, Hati hiyo imeweka makubaliano ya kuwezesha Shirika la Makazi Duniani kuanzisha ofisi yake nchini Tanzania ili kurahisisha utekelezaji wa makubaliano hayo.
Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Waziri Mabula amelishukuru shirika hilo kwa misaada mbalimbali linayoipatia Tanzania na amelipongeza kwa uamuzi wake wa kuanzisha ofisi Tanzania.
Amesema Serikali ipo tayari kuwapatia jengo la kuanzisha Ofisi za UN- Habitat nchini Tanzania na ametoa wito kwa shirika hilo kusaidia kuwajengea uwezo Watanzania kwa kuwapa mafunzo na ajira ya muda mfupi na mrefu ili kuwajengea uwezo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Maimunah Sharif alisema kuwa malengo endelevu ya makazi na nyumba yatafikiwa haraka kwa kuwa na ofisi ya kudumu katika Tanzania na nchi nyingine wanachama wa shirika hilo.
Amesema kuwa shirika hilo linafanya maandalizi kamambe ya kuanzisha ofisi zake nchini Tanzania ili kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo na litaanza utekelezaji wa kuondoa makazi holela ili kuwa na miji salama na iliyopangwa.
Ameihakikishia Tanzania kuwa shirika hilo lipo tayari kutoa mafunzo na ajira za muda mfupi ili kuwajengea Watanzania uwezo wa kusaidia utekelezaji wa makubalino yaliyofikiwa.
Kufunguliwa kwa ofisi za shirika la makazi la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kutaharakisha maendeleo endelevu ya sekta ya makazi na nyumba na kutoa ajira kwa Watanzania.