*Wakubaliana kuimarisha uhusiano kuboresha makazi na nyumba
RIPOTA PANORAMA
Nairobi, Kenya
TANZANIA imeendelea kupiga hatua katika kuondoa changamoto ya rasilimali fedha inayozikabili nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Afrika unaosababisha Serikali hizo kushindwa kuwapatia wananchi wake makazi bora na nafuu.
Hayo yamesemwa leo jijini Nairobi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula kwenye kikao kati ya Tanzania na Shirika la Makazi Afrika.
Akisoma ujumbe wa Waziri Mabula katika kikao hicho, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. John Simbachawene amesema Tanzania ina ushirikiano na Taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwamo Shelter Afrique, zinazosaidia upatikanaji wa fedha na kuwa na ubia wa pamoja wa kusaidia kuwapatia wananchi makazi bora na nafuu.
Waziri Mabula amesema Shelter Afrique imeinufaisha Tanzania kwa kuipa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa taasisi za umma na sekta binafsi zinazojishughulisha na uendelezaji milki.
Amezitaja taasisi zilizonufaika na Shelter Afrique ni pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kampuni ya Utoaji Mikopo kwa Mabenki na Taasisi za Fedha kwa ajili ya mikopo wa nyumba Tanzania (TMRC) na Kampuni ya Integrated Property Investment (Tanzania Limited).
Amefafanua maeneo ya ushirikiano ambayo Tanzania ingependa shirika hilo la makazi Afrika liyape kipaumbele ni kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya nyumba kwa ajili ya miradi mbalimbali na kampuni mbalimbali za uendelezaji milki, utakaowezesha kukabiliana na upungufu wa nyumba za makazi.
Ametaja maeneo mengine ya kipaumbele kuwa ni pamoja na kusaidia kuleta wabia wa maendeleo katika uwekezaji ambao utasaidia kukuza ajira na uchumi.
Waziri Mabula aliwasilisha kwa shirika hilo nia ya Tanzania ya kuwa mwenyeji wa kongamano kubwa na maonyesho ya teknolojia mbalimbali zinazowezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kufanyika nchini Tanzania.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. John Simbachawene (wa nne kutoka kushotoi) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Menejimenti ya Shelter Afrique baada ya kumaliza mazungumzo ya namna ya kuisadia Tanzania katika sekta ya nyumba, makazi na uboreshaji mipango miji.
Akijibu maombi mbalimbali ya maeneo ya ushirikiano na shirika hilo yaliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania, Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Thierno- Habib Hann amesema wako tayari kushirikiana na Tanzania ili kuboresha makazi na nyumba kwa Watanzania.
Hann amesema maeneo yote ya kipaumbele yaliyowasilishwa na Tanzania ya ushirikiano ikiwemo kusaidia fedha za ujenzi wa nyumba, kusaidia kuleta wabia wa maendeleo katika uwekezaji ambayo yatasaidia kukuza ajira na uchumi wa nchi ni ajenda muhimu zinazosimamiwa na shirika hilo.
Amesema shirika hilo lipo tayari kuisaida Tanzania kuandaa mkutano wa makazi (African Urban Forum) uliopangwa kufanyika Agosti 2024, mkutano ambao licha ya kuitangaza Tanzania, utasaidia kuleta teknolojia mpya za ujenzi wa nyumba bora na kuziandaa Nchi za Afrika kuwa na ajenda ya pamoja itakayosaidia kushiriki katika Mkutano wa Makazi Duniani (WUF) utakaofanyika Cairo Misri, Oktoba 2024.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya alilishukuru shirika hilo kwa kuipatia NHC mkopo nafuu wa Dola za Marekani 14.5 milioni mwaka 2012, uliosaidia kujenga nyumba za gharama nafuu 1,780 katika maeneo mbalimbali nchini.
Akabainisha kuwa sekta ya nyumba nchini Tanzania ni muhimu kusaidiwa na shirika hilo kutokana na ukweli kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa itakuwa nchi ya tisa kwa idadi ya watu duniani ifikapo mwaka 2100, ambapo kwa taarifa za Umoja wa Mataifa itakuwa na watu milioni 286.
Meneja Habari na Uhusino wa NHC, Muungano Saguya (wa pili kushoto) akiwasilisha maeneo ya ushirikiano kati ya NHC na Shirika la Makazi Afrika katika kikao kilichofanyika jijini Nairobi, Kenya leo.
Saguya ameieleza Menejimenti ya Shelter Afrique kuwa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2022, Tanzania ina uhaba wa nyumba unaofikia milioni 3.8 hivi sasa na unaongezeka kwa nyumba laki tatu kila mwaka.
Amesema kuwa NHC ambayo ni chombo cha Serikali cha kujenga nyumba, iko tayari kuendelea kushirikiana na shirika hilo ili kupunguza uhaba wa nyumba nchini Tanzania.
Saguya ameihakikishia Menejimenti ya Shelter Afrique kuwa NHC imekuwa ikilipa mikopo yake kwa ufanisi mkubwa kutokana na uwezo wake mkubwa unaotokana na rasilimali zake zenye mtaji wa Shilingi trilion 5.4.
Aidha, ameongeza kuwa NHC ina nyumba zaidi ya 17,000 katika maeneo ya katikati ya miji yenye thamani kubwa, ina ardhi ya uendelezaji na miradi yake ina wanunuzi wa uhakika.
Ameliomba Shirika hilo kuleta wawekezaji wa sekta ya nyumba nchini Tanzania kwa kuwa Serikali imezindua sera ya ubia ya NHC iliyoboreshwa ambayo inalenga kuongeza uwekezaji wenye tija katika sekta hiyo.
Utekelezaji wa mazungumzo ya shirika hilo na Tanzania imekubalika uanze mapema ili kuisaidia Tanzania kunufaika na huduma za shirika hilo lenye wanachama kutoka nchi za Kiafrika 46, ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.